MENEJA wa Real Madrid, Zinedine Zidane amemtakia kila la heri Paul Pogba baada ya kukamilisha uhamisho wake kwenda Manchester United na kuongeza kuwa chochote kinaweza kutokea kwa timu yake kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili. Pogba ambaye amekamilisha usajili uliovunja rekodi ya dunia wa pandi milioni 89.3 kwenda Old Trafford akitokea Juventus, alikuwa akihusishwa na tetesi za kwenda Madrid huku Zidane akieleza jinsi anavyomhusudu nyota huyo. Akihojiwa kuelekea mchezo wao wa Super Cup ya Ulaya dhidi ya Sevilla baadae leo, Zidane amesema anamtakia kila heri Pogba katika timu yake mpya. Wakati United wakifanya kufuru katika usajili kiangazi hiki kwa kuwasajili Pogba, Zlatan Ibrahimovic na Henrikh Mkhitaryan, Madrid wameonyesha kuwa kimya zaidi kuliko kawaida yao. Mpaka sasa Madrid wamefanikiwa kumsajili tena Alvaro Morata kutoka Juventus na kuwauza Jese Rodriguez na Denis Cheryshev kwenda Paris Saint-Germain na Villarreal.

No comments:
Post a Comment