Friday, August 5, 2016

MESSI AACHWA ORODHA YA MWISHO YA WACHEZAJI BORA ULAYA.


MSHAMBULIAJI nyota wa Barcelona, Lionel Messi ameachwa katika orodha ya mwisho ya tatu bora katika kuwania tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka wa Ulaya, akiwaacha Cristiano Ronaldo, Gareth Bale na Antoine Griezmann katika kinyang’anyiro hicho. Messi pia anaonekana hayupo hata katika nne bora katika orodha ya wachezaji 10 walioteuliwa kutokana na mchezaji mwenzake wa Barcelona Luis Suarez kumshusha mpaka nafasi ya tano. Ronaldo ndio anayepewa nafasi kubwa ya kutwaa tuzo hiyo kufuatia kuingoza Real Madrid kutwaa taji lake la 11 la michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita kabla ya kwenda kuisaidia Ureno kutwaa taji la Ulaya mwezi uliopita. Kwa upande wa Bale yeye pia ametoa mchango mkubwa kwa mafanikio ya Madrid waliyopata msimu uliopita huku akiisaidia nchi yake ya Wales kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano ya Ulaya. Griezmann yeye amekuwa na msimu mzuri pamoja na kutoshinda taji kwani timu yake ya Atletico Madrid ilipoteza mchezo wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya huku wakipoteza tena mchezo katika hatua hiyo akiwa na Ufaransa katika michuano ya Ulaya lakini aliibuka kidedea kwa kuwa mfungaji bora akiwa na mabao sita. Tuzo hiyo ambayo Messi alishinda mwaka jana, hupigiwa kura na waandishi kutoka nchi wanachama wa Shirikisho la Soka la Ulaya-UEFA ambapo mshindi wa mwaka huu anatarajiwa kutangazwa Agosti 25 siku ambayo ratiba ya makundi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya itapangwa.

No comments:

Post a Comment