MSHAMBULIAJI wa Bordeaux, Jeremy Menez amefanyiwa upasuaji baada ya kipande cha sikio lake la kulia kukatika katika mchezo wa kirafiki kujiandaa na msimu mpya dhidi ya Fc Lorient jana. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 29 ambaye amejiunga na Bordeaux akitokea AC Milan siku tatu zilizopita, alipata majeruhi hayo kufuatia kugongana kwa bahati mbaya na kiungo wa Lorient Didier Ndong dakika ya 15 ya mchezo. Katika taarifa iliyotolewa na mtandao wa klabu hiyo, Jeremy anadaiwa kufanyiwa upasuaji kwa ajili ya kushona sikio lake. Taarifa hiyo iliendelea kudai kuwa muda wa Jeremy kurejea uwanjani utategemea jinsi sikio lake litakavyopona. Bordeaux ambao walimaliza katika nafasi ya 11 katika msimamo wa Ligue 1 msimu uliopita, wanatarajia kuanza kampeni zao kwa kupepetana na St Etienne Agosti 13 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment