Thursday, August 4, 2016

ZIDANE AMVUTIA PUMZI RONALDO.

MENEJA wa Real Madrid, Zinedine Zidane amesema hatakuwa na haraka ya kumrejesha uwanjani Cristiano Ronaldo kipindi ambacho amekuwa akiuguzi majeruhi ya goti aliyopata wakati akiitumikia Ureno katika michuano ya Ulaya. Ronaldo aliumia goti katika mchezo wa fainali ambao Ureno walishinda bao 1-0 katika muda wa nyongeza dhidi ya Ufaransa katika michuano hiyo mwezi uliopita na Madrid mpaka sasa hawajapata tarehe ya kurejea kwa nyota huyo. Akiulizwa kuhusu Ronaldo mara baada ya mchezo wao wa kirafiki walioshinda bao 1-0 dhidi ya Bayern Munich, Zidane amesema kwasasa Ronaldo bado ni majeruhi hivyo hawana haraka ya kumrejesha mpaka hapo atakapopona vyema. Ronaldo ambaye alifunga mabao 51 katika mechi 48 za mashindano yote alizocheza msimu uliopita, yuko likizo nchini Marekani na anatarajiwa kukosa mchezo wa Super Cup ya Ulaya dhidi ya Sevilla utakaofanyika Agosti 9 mwaka huu. Nyota huyo pia anahofiwa kuukosa mchezo wa ufunguzi wa La Liga ambapo Madrid watafungua dimba na Real Sociedad Agosti 21.

No comments:

Post a Comment