Thursday, August 11, 2016

SOKA OLIMPIKI: BRAZIL WASONGA, ARGENTINA, MEXICO NJE.

MICHUANO ya soka ya Olimpiki kwa upande wa wanaume imeendelea tena jana na leo alfajiri kwa timu mbalimbali kujitupa katika viwanja tofauti kumalizia mechi zao za mwisho za makundi. Wenyeji Brazil baada ya kubanwa kwa sare tasa katika mechi zao mbili za kwanza jana walicharuka kwa kuibamiza Denmark kwa mabao 4-0 katika mchezo wao kundi A ambao moja kwa moja uliwavusha katika hatua robo fainali ya michuano hiyo. Denmark pamoja na kufungwa lakini nao walisonga mbele baada ya Iraq kutoa sare ya bao 1-1 dhidi ya Afrika Kusini katika mchezo mwingine wa kundi hilo. Katika michezo mingine Nigeria imekuwa timu pekee ya Afrika kutinga hatua hiyo wakiwa vinara wa kundi B pamoja na kufungwa mabao 2-0 na Colombia ambao nao wamesonga mbele wakishika nafasi ya pili. Kundi C mabingwa watetezi Mexico nao walijikuta wakitolewa kufuatia kukubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Korea Kusini huku Ujerumani wakimaliza nafasi ya pili ya kundi hilo kwa kuishindilia Fiji kwa mabao 10-0. Vigogo wengine wa soka Argentina nao walijikuta wakitolewa katika michuano hiyo kufuatia kukubali sare ya bao 1-1 dhidi ya Honduras waliosonga mbele wakishika nafasi ya pili katika kundi D huku Ureno wakimaliza vinara kwa kupata sare ya bao 1-1 dhidi ya Algeria.

No comments:

Post a Comment