MACHO na masikio ya wapenzi wa soka duniani kote mwishoni mwa wiki hii yataelekezwa huko katika jiji Manchester ambao kutakuwa na mchezo mkali wa Ligi Kuu utakaowakutanisha timu mbili mahasimu kutoka hapo. Mbali na uhasimu wa timu hizo za Manchester United na Manchester City lakini pia kutakuwa na ladha nyingine kutoka kwa mameneja Jose Mourinho na Pep Guardiola ambao nao wamekuwa mahasimu kwa kipindi kirefu kidogo. Katika mchezo huo utakaofanyika katika Uwanja wa Old Trafford, timu zote mbili zitaingia uwanjani zikiwa na rekodi nzuri ya kuanza vyema msimu mpya wa ligi wakiwa wameshinda mechi zao tatu za mwanzo. Hata hivyo pamoja matokeo hayo, United wao watakwenda katika mchezo wa kesho wakiwa na rekodi nzuri zaidi dhidi ya City katika mechi 171 walizowahi kukutana huko nyuma, ambapo wameshinda 71 dhidi ya 49 za wapinzani wao. Mchezo wa mwisho United kuitambia City ulikuwa ni ule uliofanyika Machi mwaka huu katika Uwanja wa Etihad ambapo United walishinda bao 1-0. Mchezo huo ambao unatarajiwa kuwa mgumu ni wa kwanza kukutana kwa mameneja wote wawili toka mwaka 2013 katika mchezo wa Super Cup ya Ulaya kati ya Chelsea na Bayern Munich ambapo Guardiola aliibuka kidedea kwa kushinda kwa matuta baada ya timu hizo kutoka sare ya mabao 2-2. Mameneja hao wana historia ndefu kwani wameshawahi kukutana mara 16 wakiwa na timu tofauti katika kipindi cha miaka saba iliyopita. Kulinganisha na historia ya timu hizo, upande huu ni tofauti kidogo kwani katika mara hizo 16 walizokutana Guardiola ndio ameibuka kidedea kwa kushinda mechi saba, wakitoa sare mechi sita huku Mourinho yeye akishinda mechi tatu pekee. Wakati Mourinho Inter Milan walikutana na Guadiola aliyekuwa Barcelona mara nne, mbili Guardiola akishinda, sare moja huku Mourinho naye akiambulia ushindi mara moja. Wakati Mourinho akiwa Real Madrid walikutana na Guardiola aliyekuwa Barcelona tena mara 11, tano kati ya hizo Guardiola akiibuka kidedea, sare nne na Mourinho akiambulia ushindi mara mbili katika kipindi chote alichokuwa Hispania. Mara ya mwisho mameneja hao kukutana ilikuwa Agosti 30 mwaka 2013, ambapo Guardiola akiwa na Bayern Munich aliibuka kidedea kwa changamoto ya mikwaju ya penati baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Chelsea ya Mourinho.
No comments:
Post a Comment