WACHEZAJI wa timu ya taifa ya Ghana maarufu kama Black Stars wanadaiwa kununua zaidi ya tiketi 4,000 kwa ajili ya mashabiki waliohudhuria mchezo wao wa kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Uganda Ijumaa iliyopita. Pamoja na kwamba ulikuwa mchezo wa nyumbani wa kufuzu, wizara ya michezo ya Ghana iliweka kiingilio kikubwa kwa ajili ya mchezo huo na kupelekea wachezaji wapatao wanne kununua tiketi ili kuwasaidia wale wasiokuwa na uwezo wa kumudu kiingilio hicho. Wachezaji wanaodaiwa kununua tiketi hizo ni Mubarak Wakaso aliyenunua tiketi 500 wakati beki wa kati anayecheza soka huko Ujerumani Baba Rahman na mshambuliaji wa Lorient Majeed Waris nao pia walinunua tiketi 500 kila mmoja. Wengine ni ndugu wawili Andre na Jordan Ayew ambao walinunua jumla ya tiketi 1,000 huku wachezaji wengine nao wakidaiwa kununua tiketi ambazo hazikutajwa idadi yake. Ghana walianza kampani yao hiyo ya mwisho ya kufuzu michuano hiyo kwa wasiwasi kufuatia kung’ang’aniwa sare ya bila kufungana na Uganda.
No comments:
Post a Comment