KOCHA wa timu ya taifa ya Marekani, Jurgen Klinsmann ameeleza masikitiko yake kufuatia kikosi chake kupokea kipigo cha pili mfululizo katika mechi za kufuzu Kombe la Dunia Amerika Kaskazini na Kati-CONCACAF. Mabao yaliyofungwa na Joel Campbell aliyefunga mawili, Johan Venegas na Christian Balonos yalitosha kuipa Costa Rica ushindi wa mabao 4-0 na kuifanya marekani kupoteza mchezo wake wa pili mfululizo baada ya ule waliyofungwa nyumbani na Mexico. Akihojiwa Klinsmann amesema kipigo hicho cha leo alfajiri kimemuumiza zaidi kuliko vyote alivyowahi kupata katika kipindi cha miaka mitano aliyoinoa timu hiyo. Marekani ilikuwa haijawahi kupoteza mchezo wa kufuzu kwa kufungwa kufungwa mabao manne toka walipowahi kutandikwa mabao 5-1 na Mexico Novemba mwaka 1980. Kwasasa Marekani inashikilia mkia katika kundi lao la kufuzu lenye timu sita huku Costa Rica wakiongoza kwa alama sita baada ya kushinda mechi zao mbili.
No comments:
Post a Comment