Thursday, November 17, 2016

KOCHA AIPONZA KLABU HUKO BRAZIL.

KLABU ya Gremio ya Brazil imeadhibiwa baada ya binti wa kocha Renato Gaucho kuingia uwanjani baada ya timu hiyo kushinda mchezo wao wa nusu fainali ya Kombe la Ligi nchini humo. Binti huyo Carolina Portaluppi mwenye umri wa miaka 22, alikwenda kukaa katika benchi la ufundi mwishoni mwa mchezo huo kabla ya kuingia uwanjani kuungana na wachezaji kushangilia. Mahakama ya Michezo nchini humo imeambia klabu hiyo kuwa watacheza mechi yao ya fainali ya mkondo wa pili ugenini kama adhabu ya tukio hilo. Katika hukumu yake mahakama hiyo ilidai kuwa hawahoji mapenzi ya baba kwa binti yake lakini tukio lililofanyika haliruhusiwi ndio maana imechukuliwa hatua hiyo. Klabu hiyo pia imelimwa faini ya dola 6,995, wakati gaucho ameonywa kuwa anaweza kuchukuliwa hatua zaidi. Mara baada ya maamuzi hayo, mashabiki wenye hasira walianza kumshambuliaji binti huyo katika mitandao ya kijamii huku wengine wakimtetea. Baada ya kuichapa Cruzeiro kwa jumla ya mabao 2-0 katika mechi mbili za nusu fainali walizokutana, Gremio sasa watachuana na Atletico Maneiro katika fainali ya mikondo miwili baadae mwezi huu.

No comments:

Post a Comment