HATIMAYE uongozi wa klabu ya Yanga umeweka wazi ujio wa kocha mkuu wa timu hiyo George Lwandamina toka Zambia anayekuja kurithi mikoba ya mholanzi Hans Van De Pluijm anayekuwa mkurugenzi wa benchi la Ufundi. Akizungumza katika mahojiano ya moja kwa moja na kituo cha Redio cha EFM, Makamu mwenyekiti wa Yanga Clement Sanga amesema kuwa ni kweli wameingia mkataba na George Lwandamina aliyekuwa akiifundisha Zesco United nchini Zambia na rasmi ataanza kuinoa timu hiyo mzunguko wa pili wa ligi kuu. Sanga mbali na kuweka wazi suala hilo ambalo lilikuwa ni gumzo kwa vyombo vya habari nchini, pia ametoa maelezo ya kina kwa mustakabali wa aliyekuwa kocha mkuu wa klabu hiyo Hans Van Pluijm na kusema kuwa bado wataendelea kuwa nae kama mkurugenzi wa benchi la ufundi kwani ni mwalimu mzoefu na anaijua vyema Yanga hivyo ushauri wake na uzoefu utakuwa chachu ya mafanikio katika benchi letu la ufundi na klabu kiujumla. Hans Van Pluijm ameridhia nafasi hiyo baada ya uongozi wa klabu hiyo kukaa nae chini na kumwomba aendelee kubaki klabuni kwa nafasi hiyo adhimu kwa maendeleo ya klabu hiyo kimbinu na kiufundi na mabadiliko hayo hayana maana kwamba kiwango cha kocha wa awali kilikuwa kibaya bali uongozi katika hatua ya kuiboresha klabu yake umeamua kuleta changamoto mpya ili kujiweka bora zaidi katika michuano mbalimbali inayoikabili timu hiyo.
No comments:
Post a Comment