SHIRIKISHO la Soka la Ulaya-UEFA limedai kutoa jumla ya euro milioni 150 kwa klabu ambazo ziliruhusu wachezaji wake kwa ajili ya mechi za kufuzu pamoja na michuano yenyewe ya Euro 2016. Rais wa UEFA, Aleksander Ceferin amesema kuwa klabu 641 kutoka mataifa wanachama 54 wamenufaika na malipo hayo ambayo yamefanywa chini ya makubaliano ya kufidia klabu ambazo zimekuwa zikilalalamika mara kwa mara muda ambao wachezaji wao wamekuwa wakitumia katika timu zao za taifa. Kwa mechi za kufuzu kiasi cha euro 3,536 kimelipwa kwa kila klabu ambayo moja ya wachezaji wake wamekuwa wakijumuishwa katika kikosi cha wachezaji 23 cha timu ya taifa na hiyo haijalishi kama mchezaji atakuwa amecheza au la. Kwa michuano ya Euro 2016, kiasi cha euro 7,321 kwa kila siku na kila mchezaji kililipwa kwa klabu husika. Mwenyekiti wa Umoja wa Vilabu barani Ulaya-ECA, Karl-Heinz Rummenigge amesema klabu zimekuwa zikifanya kazi kubwa kuwakuza wachezaji hivyo ni haki yao kutambuliwa kwa kazi yao hiyo.
No comments:
Post a Comment