Friday, February 24, 2017

KINA SAMATTA WAPANGWA WENYEWE KWA WENYEWE EUROPA LEAGUE.

RATIBA ya michuano ya Europa League hatua ya 16 bora imepangwa mapema leo huku klabu ya KRC Genk anayocheza mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta ikipangwa kucheza na Gent zote kutoka Ubelgiji. Genk ilitinga hatua hiyo baada ya kuiondosha Astra Giurgiu ya Romania kwa jumla ya mabao 3-2 katika mechi mbili walikutana katika hatua ya 32 bora. Samatta alifanikiwa kucheza mechi zote mbili kw dakika zote akiisaidia timu yake ya Genk kutoka sare ya mabao 2-2 ugenini dhidi ya Astra kabla ya kuja kushinda bao 1-0 jana nyumbani. Timu zingine katika ratiba hiyo ni Manchester United waliopangwa kucheza na Rostov FC ya Urusi, Schalke 04 watapambana na Borussia Monchengladbach zote za Ujerumani huku Celta Vigo ya Hispania wao wakivaana na FC Krasnodar ya Urusi. Wengine ni Apoel Nicosia ya Cyprus watavaana na Anderlecht ya Ubelgiji, Lyon ya Ufaransa watacheza na AS Roma ya Italia, Olympiakos ya Ugiriki dhidi ya Besiktas ya Uturuki na FC Copenhagen ya Denmark watachuana na Ajax Amsterdam ya Uholanzi. Mechi za mkondo wa kwanza za michuano hiyo zinatarajiwa kuchezwa Machi 9 huku zile za marudiano zikichezwa Machi 16.

No comments:

Post a Comment