Friday, February 3, 2017

MADRID, BAKU WAKIPIGANA VIKUMBO UENYEJI WA FAINALI ZA CHAMPIONS LEAGUE 2019.

SHIRIKISHO la Soka la Ulaya-UEFA limethibitisha kuwa miji ya Madrid na Baku ndio inayoshindania uenyeji wa fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2019. Muda wa mwisho kwa vyama vya soka kutuma maombi yao ilikuwa Januari 27 mwaka huu huku Baku mji mkuu wa Arzebaijan wakipeleka maombi yao kupitia Uwanja wa Olimpiki na Hispania wao wakipeleka uwanja mpya wa Atletico Madrid unaotarajiwa kumalizika mwaka huu wa Metropolitano. Azerbaijan ambayo inapatikana kaskazini mwa Iran, haijawahi kuandaa fainali hizo na klabu zao hazijawahi kufikia hatua ya makundi ya michuano hiyo toka walipopewa uanachama wa UEFA mwaka 1994. Kwa upande wa Madrid wenyewe ni moja kati ya miji mikubwa kwa michuano hiyo, kufuatia Real Madrid kutwaa kutwaa taji hilo mara 11, wakati Atletico ni klabu pekee iliyofanikiwa kufika fainali tatu bila kutwaa taji. Wakati Uwanja wa Santiago Berbabeu ukiwa imewahi kuandaa fainali hizo mara nne, ya mwisho ikiwa mwaka 2010 ambao Inter Milan iliichabanga Bayern Munich kwa mabao 2-0, Atletico wao hawajawahi kuwa wenyeji. Uwanja huo mpya wa Atletico unaondelea na matengenezo unatarajiwa kubeba mashabiki 73,000 pindi utakapokamilika.

No comments:

Post a Comment