Thursday, February 9, 2017

TANZANIA YAPOROMOKA NAFASI MBILI.

TANZANIA imeshuka kwa nafasi mbili katika viwango vipya vya ubora duniani vinavyotolewa na Shirikisho la Soka Duniani-FIFA kila mwezi. Mwezi uliopita Tanzania ilikuwa nafasi ya 156 lakini katika viwango vipya vilivyotolewa mapema leo vinaonyesha kushuka mpaka nafasi ya 158 duniani na 48 Afrika na kuwafanya kuendelea kushika nafasi ya mwisho kwa nchi za Afrika Mashariki. Uganda bado wanaendelea kuongoza kwa Afrika Mashiriki wakiwa nafasi ya 17 kwa Afrika na 75 duniani wakifuatiwa na Kenya waliopo nafasi ya 20 Afrika na 87 duniani wakati Rwanda wako nafasi ya 27 Afrika na 100 duniani na Burundi nafasi ya 40 Afrika na 138 duniani. Kwa upande wa Afrika Misri wamekuwa vinara kwa kukwea kwa nafasi 12 na kutua kileleni wakiwa nafasi ya 23, wakifuatiwa na Senegal walioko nafasi ya 31 huku mabingwa wa michuano ya Mataifa ya Afrika Cameroon nao wakikwea kwa nafasi 29 mpaka nafasi ya 33 duniani. Kwa upande wa orodha za jumla hakuna mabadiliko sana katika nafasi tano za juu kwani Argentina bado wameendelea kuwa vinara wakifuatiwa na Brazil katika nafasi ya pili huku mabingwa wa dunia Ujerumani wakiwa nafasi ya tatu. Mabingwa wa Amerika Kusini Chile wapo nafasi ya nne na Ubelgiji ndio wanakamilisha tano bora kwenye orodha hizo.

No comments:

Post a Comment