Thursday, February 9, 2017

UEFA YAWEKA UKOMO WA UONGOZI.

KAMATI ya utendaji ya Shirikisho la Soka la Ulaya-UEFA imepitisha kwa kauli moja ukomo wa urais wa shirikisho hilo kuwa vipindi vitatu viakavyokuwa na jumla ya miaka 12. Marais waliopita wa shirikisho hilo walikuwa hawana ukomo huku Lennart Johansson akiongoza kwa kipindi cha miaka 17. Rais wa sasa wa UEFA Aleksander Ceferin ambaye alichukua nafasi ya Michel Platini wa Ufaransa Septemba mwaka jana, ameahidi mageuzi katika shirikisho hilo. UEFA imesema sehemu ya mageuzi hayo yaliyopitishwa na kamati ya utendaji ni ukomo wa uongozi wa rais pamoja na wajumbe wa kamati ya utendaji ambapo sasa watatumikia vipindi vitatu pekee kwa miaka minne kila kipindi. Mabadiliko mengine ni kuruhusu nafasi mbili za ujumbe katika kamati ya utendaji kuwa wawakilishi kutoka Chama cha Vilabu Ulaya-ECA. Mabadiliko hayo sasa yanahitaji kupitishwa katika Mkutano Mkuu wa UEFA utaofanyika Aprili 5 huko Finland.

No comments:

Post a Comment