MSHAMBULIAJI nyota wa kimataifa wa Ureno na klabu ya Real Madrid, Cristiano Ronaldo ndiye mwanasoka anayelipwa zaidi kwa msimu huu wa 2016-2017, akikunja kitita cha euro milioni 87 na kumzidi hasimu wake nyota wa Argentina na Barcelona Lionel Messi anayepata euro milioni 76.5. Kwa mujibu wa taarifa hizo zilizotolewa na jarida maarufu la France Football, Neymar ndiye anayefuatia kwenye nafasi ya tatu akikunja kitita cha euro milioni 55.5 mbele ya nyota wa Wales na Real Madrid Gareth Bale anayepata euro milioni 41. Anayefuatia kwenye orodha hiyo ni nyota mwingine wa kimataifa wa Argentina Ezequial Lavezzi anayepokea kitita cha euro milioni 28.5 katika klabu ya Hebei Fortune ya China. Meneja wa Manchester United Jose Mourinho ndiye meneja anayelipwa zaidi akikunja kitita cha euro milioni 28 kwa mwaka ambapo kiwango hicho kinajumuisha mshahara, marupurupu na kipato cha matangazo mwaka msimu huu.
No comments:
Post a Comment