Friday, March 24, 2017

RUNGU LA UEFA LAINGUKIA ARSENAL NA BAYERN.

KLABU za Arsenal na Bayern Munich zimelimwa adhabu na Shirikisho la Soka la Ulaya-UEFA kufuatia mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya baina ya timu hizo uliochezwa mwanzoni mwa mwezi huu. Arsenal wakiwa nyuma ya mabao 5-1 waliyofungwa katika mchezo wa mkondo wa kwanza nchini Ujerumani, walipokea kipigo kingine kama hicho kwenye Uwanja wa Emirates Machi 7 mwaka huu na kutolewa nje ya michuano hiyo. Klabu zote mbili zimelimwa adhabu na UEFA kwa matukio mawili tofauti ambapo Arsenal wao wametozwa faini ya euro 5,000 baada ya mashabiki kadhaa kuvamia uwanjani wakati Bayern wao wametozwa faini ya euro 3,000 kufuatia vitu vilivyorushwa na mashabiki wao uwanjani. Kipigo hicho cha Arsenal kwenye mchezo huo kiliongeza shinikizo kwa mashabiki wake kumtaka meneja Arsene Wenger kuondoka kufuatia kutofanya vyema kwenye mechi zao kadhaa huku wakitolewa katika hatua ya 16 ya michuano hiyo kwa mara ya saba mfululizo.

No comments:

Post a Comment