Thursday, March 9, 2017

TANZANIA YAKWEA NAFASI MOJA VIWANGO FIFA.

TANZANIA imepanda kwa nafasi moja katika viwango vipya vya ubora duniani vinavyotolewa na Shirikisho la Soka Duniani-FIFA kila mwezi. Mwezi uliopita Tanzania ilikuwa nafasi ya 158 lakini katika viwango vipya vilivyotolewa mapema leo vinaonyesha kupanda mpaka nafasi ya 158 duniani na 48 Afrika na kuwafanya kuendelea kushika nafasi ya mwisho kwa nchi za Afrika Mashariki. Uganda bado wanaendelea kuongoza kwa Afrika Mashiriki wakiwa nafasi ya 16 kwa Afrika na 74 duniani wakifuatiwa na Kenya waliopo nafasi ya 21 Afrika na 88 duniani wakati Rwanda wako nafasi ya 24 Afrika na 93 duniani na Burundi nafasi ya 41 Afrika na 139 duniani. Kwa upande wa Afrika Misri wameendelea kuwa vinara kwa kukwea kwa nafasi mbili zaidi hadi nafasi ya 20, wakifuatiwa na Senegal walioko nafasi ya 28 huku mabingwa wa michuano ya Mataifa ya Afrika Cameroon nao wakikwea kwa nafasi moja mpaka nafasi ya 32 duniani. Kwa upande wa orodha za jumla hakuna mabadiliko yeyote katika nafasi tano za juu kwani Argentina bado wameendelea kuwa vinara wakifuatiwa na Brazil katika nafasi ya pili huku mabingwa wa dunia Ujerumani wakiwa nafasi ya tatu. Mabingwa wa Amerika Kusini Chile wapo nafasi ya nne na Ubelgiji ndio wanakamilisha tano bora kwenye orodha hizo.

1 comment: