MABINGWA wa soka Tanzania Bara, Yanga wamepangwa kucheza na klabu ya MC Alger ya Algeria katika hatua ya mtoano ya timu 32 za bora katika michuano ya Kombe la Shirikisho katika ratiba iliyopangwa Makao Makuu ya Shirikisho la Soka la Afrika, Cairo, Misri. Ratiba hiyo ilijumuisha timu 16 zilizovuka hatua ya mtoano ya Kombe la Shirikisho dhidi ya timu 16 zilizotolewa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Yanga iliangukia katika michuano hiyo kufuatia kutolewa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kufuatia sare ya bila kufungana na Zanaco ya Zambia mwishoni mwa wiki iliyopita na kuwafanya kutolewa kwa bao la ugenini kufuatia sare ya bao 1-1 waliyopata katika mchezo wa awali uliofanyika jijini Dar es Salaam. Katika hatua hiyo Yanga inatarajiwa kuanza mchezo wake wa mkondo wa kwanza nyumbani kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam huku mchezo wa marudiano ukitarajiwa kuchezwa wiki moja baadae huko Algeria. Kwa mujibu wa ratiba iliyotoka leo mechi za mkondo wa kwanza zinatarajiwa kuchezwa kati ya Aprili 7 na 9 huku zile za marudiano zikichezwa kati Aprili 14 na 16.
No comments:
Post a Comment