Tuesday, April 11, 2017

BAUZA ATIMULIWA ARGENTINA.

CHAMA cha Soka cha Argentina, AFA kimemtimua kocha wa timu ya taifa ya nchi hiyo Edgardo Bauza baada ya kuongoza mechi nane pekee. Argentina wanashikilia nafasi ya tano katika msimamo wa kundi la timu 10 za kufuzu Kombe la Dunia kwa nchi za Amerika Kusini ambapo timu nne pekee ndio zitakazopata nafasi ya kwenda Urusi kwenye michuano hiyo. Timu inayomaliza kwenye nafasi ya tano italazimika kwenda kucheza hatua ya mtoano dhidi ya timu kutoka bara la Oceania. Bauza mwenye umri wa miaka 59, aliteuliwa kuiongoza nchi hiyo Agosti mwaka jana na kufanikiwa kushinda mechi tatu, sare mbili na kupoteza tatu. Rais wa AFA, Claudio Tapia amesema walifikia uamuzi huo kwani timu hiyo haichezi vyema na kila mtu anafahamu hilo. Mechi ya mwisho ya Bauza ilikuwa ni dhidi ya Bolivia ambapo Argentina walipigwa mabao 2-0 mjini La Paz ikiwa ni saa chache baada ya nahodha wao Lionel Messi kufungiwa kwa kumtolea lugha chafu mwamuzi. Argentina imebakiwa na mechi nne za kufuzu huku mchezo wao ujao ukiwa dhidi ya Uruguay wanaoshikilia nafasi ya tatu Agosti 31 mwaka huu. Mara ya mwisho Argentina kushindwa kufuzu michuano hiyo ilikuwa mwaka 1970.

No comments:

Post a Comment