Tuesday, April 25, 2017

KIPIGO CHA BARCELONA CHAMCHANGANYA RONALDO, AMPIGA "BITI" MPENZI WAKE.

MSHAMBULIAJI nyota wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo amemuagiza mpenzi wake kuacha kumuandalia sherehe kufuatia kipigo cha mabao 3-2 walichopata kutoka kwa mahasimu wao wa La Liga Barcelona. Ronaldo angeweza kuwa na siku nzuri mwishoni mwa wiki iliyopita wakati Madrid walipoiklaribisha Barcelona katika El Clasico, hata hivyo mambo hayakuwa mazuri kama yalivyotegemewa baada ya Lionel Messi kuibuka nyota wakati Barcelona wakiondoka na ushindi huo mnono. Badala ya kufurahia ushindi wa Madrid katika sherehe iliyoandaliwa na mpenzi wake Georgina Rodriguez, Ronaldo alitoka uwanjani akiwa kichwa chini baada ya kipigo hicho. Taarifa kutoka nchini Ureno zinadai kuwa, Rodriguez alikuwa ameandaa sherehe ya baada ya mechi nyumbani kwa Ronaldo jijini Madrid lakini shughuli hiyo ilibidi isitishwe kufuatia matokeo ya mwisho. Mbali na kusitisha sherehe hiyo fupi lakini Ronaldo mwenyewe anadaiwa kwenda mbali zaidi kwa kumkataza mpenzi wake huyo kumuandalia sherehe kama hizo siku za usoni. Wawili hao wamekuwa pamoja kwa miezi saba sasa, na walionekana pamoja katika sherehe za utoaji tuzo za FIFA Januari mwaka huu sambamba na mtoto wa Ronaldo, Crstiano Jr.

No comments:

Post a Comment