KLABU ya Tottenham Hotspurs, imethibitisha kuwa itautumia Uwanja wa Wembley kuanzia msimu wa 2017-2018 kama uwanja wake wa nyumbani wakati ujenzi wa uwanja wao mpya ukiendelea. Uwanja mpya wa klabu hiyo unatarajiwa kuingiza mashabiki wapatao 61,000 na unajengwa pembeni ya uwanja wao wa sasa wa White Hart Lane. Spurs imecheza mechi zake za Ligi ya Mabingwa Ulaya na Europa League katika Uwanja wa Wembley msimu huu lakini amefanikiwa kushinda mechi moja kati ya nne. Mwenyekiti wa klabu hiyo, Daniel Levy amesema wakati ni mzuri katika historia ya klabu hiyo, kwani wanakwenda Wembley kwa msimu mmoja halafu wanahamia katika moja ya viwanja bora kabisa duniani. Levy aliendelea kudai kuwa uwanja huo ambao pia utakuwa ukitumika kwa ajili ya mechi za Ligi ya Soka ya Marekani-NFL, utakuwa muhimu kwa maendeleo na mafanikio yao ya baadae. Uwanja huo mpya unatarajiwa kujengwa kwa kitita cha paundi milioni 750 lakini unatarajiwa kutengeneza ajira karibu 3,500 katika eneo hilo wakati utakapomalizika.
No comments:
Post a Comment