Thursday, April 6, 2017

TANZANIA YAKWEA VIWANGO FIFA.

TANZANIA imepanda kwa nafasi 22 katika viwango vipya vya ubora duniani vinavyotolewa na Shirikisho la Soka Duniani-FIFA kila mwezi. Mwezi uliopita Tanzania ilikuwa nafasi ya 157 lakini katika viwango vipya vilivyotolewa mapema leo vinaonyesha kupanda mpaka nafasi ya 135 duniani na 39 Afrika na kufanya kujisogeza mpaka nafasi ya nne wakiipita Burundi kwa nchi za Afrika Mashariki. Uganda bado wanaendelea kuongoza kwa Afrika Mashiriki wakiwa nafasi ya 15 kwa Afrika na 72 duniani wakifuatiwa na Kenya waliopo nafasi ya 16 Afrika na 78 duniani wakati Rwanda wako nafasi ya 33 Afrika na 117 duniani na Burundi wao wapo nafasi ya 41 Afrika na 141 duniani. Kwa upande wa Afrika Misri wameendelea kuwa vinara wakipanda nafasi moja zaidi hadi nafasi ya 19, wakifuatiwa na Senegal walioko nafasi ya 30 kufuatia kuteleza kwa nafasi mbili huku mabingwa wa michuano ya Mataifa ya Afrika Cameroon nao wakiteleza nafasi moja mpaka nafasi ya 33 duniani. Kwenye orodha za jumla Brazil wamekwea kileleni wakiiondoa Argentina iliyoanguka kwa nafasi moja mpaka ya pili, wa tatu ni mabingwa wa Dunia Ujerumani wakifuatiwa na mabingwa wa Amerika Kusini Chile na Colombia ndio wanahitimisha tano bora.

No comments:

Post a Comment