Wednesday, April 26, 2017

UWANJA WA AMSTERDAM ARENA KUPEWA JINA LA CRUYFF.

Yohan Cruyff
UWANJA wa Amsterdam Arena unatarajiwa kubadilishwa na kupewa jina la nguli wa zamani wa Uholanzi Johan Cruyff. Cruyff mmoja kati ya wanasoka bora kabisa na mwenye ushawishi zaidi na kocha aliyekuwa na maono, alifariki dunia zaidi ya mwaka mmoja uliopita baada ya kupambana miaka mitano na maradhi ya saratani ya mapafu, akiwa na umri wa miaka 68. Katika taarifa ya maafisa wa uwanja huyo iliyotumwa katika tovuti yao, imedai kuwa wamefikia uamuzi huo kwa kuupa jina la Johan Cruyff uwanja huo kutokana na mchango mkubwa aliotoa akiwa mchezaji na kocha. 
Mtoto wake wa kiume, Jordi amesema familia yao imefarijika kwa utambuzi huo ambao unatarajiwa kufanyika ndani ya kipindi cha miezi sita ijayo. Amsterdam Arena wenye uwezo wa kubeba mashabiki 54,000 ulijengwa mwaka 1996 na unamilikiwa kwa ushirikiano na klabu ya Ajax, halmashauri ya mji wa Amsterdam na kampuni inayosimamia uwanja huo.

No comments:

Post a Comment