Friday, May 5, 2017

CHINA YAFANYA KUFURU KWA KOCHA MANZANO.

KOCHA Gregorio Manzano wa Hispania amekuwa mmoja kati ya mameneja wanaolipwa zaidi duniani baada ya kukubali kwenda kuinoa klabu ya Guizhou Zhicheng inayoshiriki Ligi Kuu ya China. Kwa mujibu wa taarifa kutoka China, kocha huyo wa zamani wa Sevilla na Atletico Madrid, amesaini mkataba wenye thamani ya euro milioni 8 kwa mwaka huku kibarua chake kikubwa kikiwa ni kuhakikisha Guizhou Zhicheng haishuki daraja. Manzano alikaririwa akidai kuwa mmiliki wa klabu hiyo Wen Wei anataka kuhakikisha timu yake haishuki daraja kwa gharama yeyote na ana matumaini hatamuangusha kutimiza malengo yake hayo. Klabu hiyo ambayo imepoteza mechi zake tatu za mwanzo wa msimu mpya, ilifanikiwa kupata ushindi wake wa kwanza wa mabao 3-1 dhidi Guangzhou R&F Ijumaa hii. Manzano sasa analingana na meneja wa Chelsea Antonio Conte ambaye naye analipwa kiasi kama hicho kwa mwaka.

No comments:

Post a Comment