MSHAMBULIAJI wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo anaripotiwa kumtaka wakala wake Jorge Mendes kuhakikisha anafanya mipango ya yeye kurejea Manchester United. Nyota huyo wa kimataifa wa Ureno bado ameendelea kuhusishwa na tetesi za kurejea Old Trafford baada ya kufanya maamuzi ya kutaka kuondoka Madrid. Ronaldo amekuwa akituhumiwa kukwepa kodi nchini Hispania inayokadiriwa kufikia paundi milioni 13, hivyo kuamua kuondoka La Liga. Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na gazeti la The Sun, nyota huyo anataka kurejea United na amemtaka wakal wake kuhakikishia anafanikisha suala hilo. Ronaldo alijiunga na United mwaka 2003 akiwa na umri wa miaka 18 na kufanikiwa kufunga mabao 118 katika mechi 292 alizoichezea timu hiyo kwa kipindi cha miaka sita. Mwaka 2009 alihamia Madrid na kuja kuwa mfungaji bora wakati wote wa timu hiyo kwa kufunga mabao 406 katika mechi 394 alizocheza mpaka sasa. Taarifa zingine zilizotoka mapema leo zimedai kuwa United wako tayari kutoa kitita cha paundi milioni 175 kwa ajili ya usajili huo kipindi hiki cha kiangazi pamoja na kumruhusu David de Gea kwenda Madrid.
No comments:
Post a Comment