Tuesday, April 2, 2013
RONALDO AMHIMIZA NEYMAR KUTIMKIA ULAYA.
MSHAMBULIAJI nyota wa zamani wa kimataifa wa Brazil, Ronaldo de Lima amemtaka nyota anayechipukia wa nchi hiyo Neymar kuangalia uwezekano wa kutafuta klabu Ulaya ili kuongeza uzoefu zaidi kabla ya michuano ya Kombe la Dunia 2014. Neymar mwenye umri wa miaka 21 ambaye kwasasa amekuwa anacheza katika klabu ya Santos amekuwa akihusishwa na tetesi za kuhitajika katika klabu za Bayern Munich ya Ujerumani na Barcelonaya Hispania lakini mwenyewe amekuwa akisisitiza kubakia nchini kwake mpaka mkataba wake utakapomalizika 2014. Ronaldo amesema hakuna shaka kwamba Neymar ni mzuri na atakuwa mmoja wa wachezaji bora duniani wakati atakapoamua kucheza soka Ulaya kwani ana kipaji cha hali ya juu. Nguli huyo mwenye umri wa miaka 36 amedai kuwa muda mzuri wa Neymar kwenda Ulaya ni kabla ya michuano ya Kombe la Dunia 2014 kwani itamsaidia kukomaa kiuchezaji na kupata uzoefu zaidi wa kuingoza Brazil.
Monday, April 1, 2013
MANCHESTER UNITED WASULUBIWA DARAJANI NA CHELSEA.
CHAMPIONS LEAGUE: NI BARCA VS PSG, BAYERN VS JUVENTUS.
LIGI ya Mabingwa Ulaya hatua ya robo fainali inatarajiwa kuanza kutimua vumbi tena leo wakati timu nne zitakapojitupa dimbani katika mechi zao za kwanza za kutafuta tiketi ya kucheza nusu fainali ya michuano hiyo. Katika mchezo wa kwanza Barcelona wakiongozwa na nyota wake Andres Iniesta na Lionel Messi tayari wamewasili jijini Paris, Ufaransa kuikabili Paris Saint Germain ambao wanajivunia nyota wao Zlatan Ibrahimovic na David Beckham ambao imewasajili hivi karibuni. Mbali na mchezo huo pia kutakuwa na mchezo mwingine wa kukata na shoka kati ya vinara wa Ligi Kuu nchini Ujerumani timu ya Bayern Munich ambao watakuwa wenyeji wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu nchini Italia, Juventus katika Uwanja wa Alianz Arena. Juventus watakuwa na kibarua kizito kuidhibiti safu ya ushambuliaji ya Bayern ambayo imeonyesha kuwa katika kiwango cha juu baada ya kuibugiza Hamburger SV kwa mabao 9-2 katika mchezo wa ligi.
BERCELONA HAWATUTISHI - MOURA.
MCHEZAJI nyota wa klabu ya Paris Saint-Germain-PSG ya Ufaransa, Lukas Moura ana matumaini makubwa ya kikosi chake kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa kwa kuing’oa Barcelona, akisisitiza kuwa wapinzani wao hao sio bora kama watu wengi wanavyosema. Barcelona ni mojawapo ya timu zinazopewa nafasi kubwa ya kunyakuwa taji la michuano hiyo ya Ulaya msimu huu lakini Moura ambaye ni raia wa Brazil anaamini kuwa timu hiyo ina udhaifu mkubwa ambao watautumia wakati watakapokutana kesho. Moura amesema amekisifu kikosi cha Barcelona kwa kusheheni nyota wakali na kucheza soka la kuvutia duniani lakini hana shaka kwamba kocha wao Carlo Ancelotti atawapa mbinu kabambe ili kuhakikisha wanatumia vyema udhaifu wa wapinzani wao ili kuhakikisha wanaibuka kidedea. Nyota huyo ambaye alikuwa akicheza klabu ya Santos kabla ya kutua PSG pia amedai kumhusudu nyota wa zamani wa klabu hiyo na Barcelona Ronaldinho na ana matumaini ya kufuata nyayo zake.
BALOTELLI AENDELEZA VITUKO VYAKE ITALIA.
NYOTA wa zamani wa klabu ya Manchester City mwenye vituko vingi, Mario Balotelli ameonyesha kushindwa kupigwa picha akiwa amelala katika sehemu ya kuwekea mizigo katika treni walioyokuwa wakisafiri nayo. Katika picha hiyo Balotelli alionekana akiwa na nyota wenzake wa klabu yake ya AC Milan M’Baye Niang na Stephan El Shaarawy wote wakiwa wameacha viti vilivyopo katika treni hiyo na kukwea juu kwenye mizigo. Balotelli alihamia Milan Januari baada ya kucheza katika klabu ya Manchester City kwa misimu miwili na nusu na toka arejee nyumbani kwao amekuwa akicheza kwa kiwango cha juu baada ya kufunga mabao matano katika mechi sita za Serie A. Nyota huyo pia alifunga mabao yote ya timu yake ya taifa ya Italia iliyoshinda mabao 2-0 katika mchezo wa kufuzu michuano ya Kombe ya Dunia dhidi ya Malta wiki iliyopita.
BOLT ANG'ARA COPACABANA.
MWANARIADHA nyota wa mbio fupi Usain Bolt ameshindwa kufikia rekodi yake ya dunia aliyoweka katika mbio za mita 150 wakati alipofungua msimu kwa ushindi kwenye masshindano yaliyofanyika kwenye ufukwe wa Copacabana jijini Rio de Janeiro, Brazil. Bolt ambaye ni bingwa mara sita wa medali za dhahabu katika michuano ya olimpiki alishinda mbio hizo kwa kutumia muda wa sekunde 14.42 lakini alishindwa kuifikia rekodi yake aliyoweka mwaka 2009 jijini Manchester, Uingereza ya sekunde 14.41. Akihojiwa mara baada ya mashindano hayo Bolt amesema hayo ni mashindano yake ya kwanza na anashukuru kuanza msimu mpya vyema huku akisubiri kwa hamu mchuano ya olimpiki 2016 iakayofanyika katika jiji hilo. Katika mashindano hayo Bruno Lins wa Brazil alishika nafasi ya pili kwa kutumia sekunde 14.91 akifuatiwa na Alex Quinones wa Ecuador na Daniel Bailey wa Antigua na Barbuda waliomaliza katika nafasi ya tatu na nne.
MURRAY AKWEA MPAKA KATIKA NAFASI YA PILI KWA UBORA DUNIANI.
MCHEZA tenisi nyota kutoka Uingereza, Andy Murray amefanikiwa kumfunga David Ferrer wa Hispania na kunyakuwa taji la michuano ya wazi ya Sony iliyokuwa ikifanyika jijini Miami, Florida nchini Marekani. Katika mchezo huo Murray alimfunga Ferrer kwa 2-6 6-4 7-6 ushindi ambapo pia umempandisha mpaka katika nafasi ya pili katika orodha za ubora duniani kwa upande wa wanaume. Akihojiwa mara baada ya mchezo huo Murray ambaye hilo ni taji lake la pili alikiri kuwa ulikuwa mchezo mgumu na yoyote kati yao angeshinda kwasababu wote walikuwa wamechoka katika dakika za mwishoni. Mara ya mwisho Murray ambay yuko nyuma Novak Djokovic anayeshika namba moja katika orodha hizo, kushika nafasi ya pili ilikuwa ni mwaka 2009 wakati Roger Federer akiwa namba moja.
Subscribe to:
Posts (Atom)









