MENEJA wa klabu ya AC Milan ya Italia, Massimiliano Allegri ataendelea kubakia San Siro baada ya kufanya mazungumzo na rais wa klabu hiyo Silvio Berlusconi na Mtendaji Mkuu Adriano Galliani. Mustakabali wa Allegri katika klabu hiyo ulikuwa mashakani katika wiki za karibuni baada ya kocha huyo mwenye umri wa miaka 45 kuisaidia timu hiyo kupata nafasi ya kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa katika mechi ya mwisho huku mahasimu wao AS Roma wakiripotiwa kutaka kumchukua kocha huyo. Hata hivyo hatimaye Allegri na viongozi wa klabu hiyo walikaa chini na kufanya mazungumzo baada ya mara kadhaa kikao chao kuahirishwa kutokana na sababu mbalimbali. Allegri alichukua mikoba ya kuinoa klabu hiyo mwaka 2010 na kuiongoza kushinda taji la Ligi Kuu nchini Italia katika msimu wake wa kwanza.
Monday, June 3, 2013
MOURINHO KUTEULIWA MENEJA MPYA WA CHELSEA WIKI HII.
JOSE Mourinho anategemea kuchaguliwa kuwa meneja mpya wa klabu ya Chelsea mwishoni mwa wiki hii baada ya kuondoka rasmi katika klabu ya Real Madrid ya Hispania. Mourinho ambaye ni raia wa Ureno amemaliza amekuwa na msimu mbaya na Madrid baada ya kushindwa kuelewana na baadhi ya wachezaji wa timu hiyo na viongozi wa benchi lake la ufundi huku akishindwa kutwaa taji lolote msimu huu. Mourinho aliwahi kuzungumzia nia yake ya kwenda mahali ambapo anapendwa baada ya Madrid kuenguliwa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na Borussia Dortmund. Akihojiwa mara ya kumalizika kwa mechi yake ya mwisho akiwa Madrid, Mourinho amesema anategemea kwenda jijini London kufanya mazungumzo na ni mategemeo yake atatajwa kama meneja mpya wa klabu hiyo mwishoni mwa wiki. Mara ya kwanza Mourinho kuinoa Chelsea ilikuwa ni mwaka 2004 baada ya kuingoza Porto kushinda taji la Ligi ya Mabingwa, na kushinda mataji mawili ya Ligi Kuu, moja ya FA na mawili ya Kombe la Ligi kabla ya kuondoka mwaka 2007.
ALVES AMFAGILIA NEYMAR KUNG'ARA BARCELONA.
BEKI wa kimataifa wa Brazil na klabu ya Barcelona, Dani Alves amedai kuwa mshambuliaji mpya wa klabu hiyo Neymar atang’ara na hatahitaji muda mrefu wa kuzoea mazingira mapya msimu ujao. Neymar mwenye umri wa miaka 21 anatarajia kuondoka klabu ya Santos kwenda Barcelona baada ya kukubalia kusaini mkataba wa miaka mitano na klabu hiyo ambapo Alves anaamini nyota huyo atapata mafanikio akiwa Camp Nou. Alves amesema nyota huyo ana kipaji cha hali ya juu ndio maana Barcelona wakaamua kumsajili kutoka Santos na ni mategemeo yao atazoea mazingira ya Barcelona haraka kwasababu atakuwa akifanya kitu anachokipenda nacho ni kucheza soka. Neymar anatarajiwa kufanyiwa vipimo vya afya na Barcelona leo kabla ya kumalizia taratibu za uhamisho wake.
WENGER AKIRI KUMTAKA ROONEY.
MENEJA wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger amekiri kuwa na nia ya kumsajili mshambuliaji nyota wa klabu ya Manchester United Wayne Rooney. Wenger amekuwa akifuatilia nyendo za nyota huyo aliyeomba kuondoka mwishoni mwa msimu huu huku klabu za Chelsea na Paris Saint-Germain nazo pia zikionyesha nia ya kutaka saini ya mchezaji huyo. Akihojiwa na luninga ya Al Jazeera, Wenger amesema Rooney ni aina ya mchezaji ambaye timu yoyote kubwa duniani itahitaji huduma yake ndio maana wanafuatilia nyendo zake kama akishindwa kubakia United watajaribu kumsajili. Arsenal inategemewa kutumia kiasi cha paundi milioni 80 kwa ajili ya usajili katika kipindi hiki cha majira ya kiangazi huku wakijipanga kusaini mkataba mpya wa jezi zao na kampuni ya Puma. Kwa mujibu wa ripoti zilizotoka jana, PSG wao wamepanga kumpa Rooney mshahara wa paundi milioni 350,000 kwa wiki baada ya kukatwa kodi ili kumshawishi nyota huyo kwenda Ufaransa.
Sunday, June 2, 2013
TAIFA STARS, SUDAN ZATOKA SULUHU.
Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) imetoka sare ya bila kufungana na Sudan (Nile Crodcodile) katika mechi ya kujipima nguvu iliyochezwa leo (Juni 2 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Addis Ababa nchini Ethiopia. Mechi hiyo iliyochezeshwa na mwamuzi Bamlak Tessema wa Ethiopia ilikuwa sehemu ya maandalizi kwa timu zote ambazo wikiendi ijayo zinacheza mechi za mchujo za Kombe la Dunia. Wakati Stars itakuwa ugenini nchini Morocco, Sudan itacheza nyumbani dhidi ya Ghana. Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager ilicheza vizuri mechi hiyo, hasa kipindi cha pili ambapo ilifanikiwa kutengeneza nafasi kadhaa za kufunga lakini ama washambuliaji walipiga nje au mipira yao kuokolewa na kipa Ehab Abdelfatahh wa Sudan. Washambualiji wa Stars akina Khamis Mcha, Mrisho Ngasa na Amri Kiemba wakiongozwa na John Bocco walilitia msukosuko mara kwa mara lango la Sudan ambalo lilikuwa chini ya beki wa kati Nadir Eltayeb ambaye alifanya kazi ya ziada dakika ya 72 kuokoa mpira uliokuwa ukielekea wavuni. Stars katika mechi hiyo iliwakilishwa na Juma Kaseja, Nadir Haroub/Vicent Barnabas, Shomari Kapombe, Kelvin Yondani, Aggrey Morris, Frank Domayo, Mrisho Ngasa, Salum Abubakar, John Bocco/Haruni Chanongo, Amri Kiemba/Khamis Mcha na Simon Msuva/Athuman Idd. Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Joram Biswaro amewataka wachezaji wa Taifa Stars kuhakikisha wanaipeleka timu hiyo kwenye fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwakani nchini Brazil. Timu inaondoka kesho alfajiri kwenda Morocco kwa kupitia Cairo, Misri ambapo inatarajia kuwasili Casablanca saa 8 mchana.
PEREZ ACHAGULIWA KUIONGOZA MADRID KWA KIPINDI KINGINE TENA.
FLORENTINO Perez amechaguliwa kwa kipindi kingine tena kama rais wa klabu ya Real Madrid katika mkutano wa uchaguzi uliofanyika mapema leo. Zoezi la uteuzi wa majina lilimalizika Jumamosi usiku wakati muda wa kuchukua fomu za kugombea nafasi hiyo ulipomalizika bila ya kutokea mgombea yoyote wa kushindana na Perez. Kutokana na hilo bodi ya uchaguzi ya klabu hiyo ilimpitisha na kumpigia kura kama mgombea pekee kwenye uchaguzi huo na baadae kutoa taarifa kupitia katika mtandao wake. Perez mweye umri wa miaka 66 ameiongoza klabu hiyo toka mwaka 2000.
DJOKOVIC AFIWA NA KOCHA WAKEWA ZAMANI.
MCHEZAJI tenisi namba moja kwa ubora duniani, Novak Djokovic amefanikiwa kusonga mbele kwenye michuano ya wazi ya Ufaransa baada ya kumchakaza mchezaji anayechipukia Grigor Dimitrov. Djokovic alifanikiwa kumfunga Dimitrov kwa 6-2 6-2 6-3 kabla ya kupewa taarifa mbaya za kifo cha kocha wake wa zamani Jelena Gencic ambaye alifariki akiwa na umri wa miaka 77. Gencic ambaye amewahi pia kufanya kazi na Monica Seles na Gora Ivanisevic, ndio alikuwa kocha wa kwanza wa Djokovic akiwa na miaka sita ambapo alimfundika kwa kipindi cha miaka mitano. Kwa kuonyesha jinsi gani alivyoguswa na msiba huo Djokovic alishindwa kuzungumza na vyombo vya habari baada ya mchezo wa jana ambapo anatarajia kurejea uwanjani tena Jumatatu kukwaana na Philipp Kohlschreiber wa Ujerumani.
Subscribe to:
Posts (Atom)






