MENEJA wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger amesisitisha kuwa kikosi chake hakiko katika msukumo wowote na kuwataka wachezaji wake kupuuza madai kwamba timu hiyo haiwezi kushinda taji la Ligi Kuu nchini Uingereza msimu huu. Arsenal wako kileleni mwa msimamo wa ligi kwa tofauti ya alama nne ambapo wanatarajiwa kuwakaribisha Hull City katika Uwanja wa Emirates baadae leo. Wakosoaji wanadai kuwa Arsenal haiwezi kuendelea kuwa katika kiwango cha juu walichoanza nacho kwa msimu wote lakini Wenger anaamini kuwa klabu hiyo ina nafasi nzuri ya kushinda taji hilo. Wenger amesema hakuna msukumo wowote ila wana nia ya kushinda taji hilo ndio maana wako kileleni hivi sasa na kitu cha muhimu kwao ni kuhakikisha wanaendelea kucheza kwa kwa umoja na kwa kiwango bora.

Wednesday, December 4, 2013
VIWANJA VITATU VYA KOMBE LA DUNIA KUSHINDWA KUKAMILIKA KWA WAKATI.
SHIRIKISHO la Soka Duniani-FIFA limedai kuwa viwanja vitatu vinavyojengwa kwa ajili ya michuano ya Kombe la Dunia 2014 nchini Brazil vitavuka muda uliopangwa katika kukamilika kwake. Viwanja hivyo ambavyo ni Arena Pantanal kilichopo katika mji wa Cuiaba, Arena da Baixada uliopo Curitiba na Arena Corinthians uliopo jijini Sao Paulo ndivyo vinavyotarajiwa kuvuka muda wa mwisho ambao ni Desemba 31 mwaka huu. Rais wa FIFA, Sepp Blatter alitoa rambirambi kwa familia zilizopoteza ndugu zao katika ajali iliyoua watu wawili katika Uwanja wa Corinthians mwezi uliopita lakini akadai kuwa uwanja huo utakuwa tayari kwa ajili ya mechi ya ufunguzi itakayochezwa Juni 12 mwakani. Blatter aliongeza kuwa tatizo la viwanja hivyo kutokamilika kwa wakati ni dogo hivyo wanaweza kulifumbia macho. Blatter amesema viwanja vyote hivyo na vingine vitakavyotumika kwa ajili ya michuano hiyo vitakuwa vimekamilika ifikapo Februari mwakani.
JUVENTUS YAPIGWA FAINI.
KLABU ya Juventus imepigwa faini ya paundi 4,140 baada ya watoto wa shule kukutwa na hatia ya kuimba kwa lugha isiyo ya kiungwana. Watoto hao wapatao 12,200 walikuwa wamekaa nyuma ya goli katika mchezo wa Jumapili dhidi ya Udinese nafasi ambayo hukaliwa na mashabiki waitwao Ultras ambao nao walifungiwa kwa ushangiliaji wa kidhalilishaji. Wanafunzi walikuwa wakimtukana golikipa wa Udinese Zeljko Brkic kila unapopigwa mpira wa adhabu kuelekea langoni mwake. Kocha wa Udinese Francesco Guidolin alielezea masikitiko yake kuhusiana na tukio hilo na kudai kuwa linachafua sura ya mchezo wa soka nchini humo.
Tuesday, December 3, 2013
ZANZIBAR YAPUMULIA MASHINE MICHUANO YA CECAFA CHALENJI.
KENYA, Harambee Stars imeungana na Ethiopia kutinga Robo Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge baada ya kuifunga Zanzibar mabao 2-0 Uwanja wa Afrah, Nakuru. Mabao ya Harambee leo yamefungwa na beki wa Azam FC ya Dar es Salaam, Joackins Atudo kwa penalti dakika ya sita na mshambuliaji wa AFC Leopards ya Kenya, Allan Wanga dakika ya 60. Kwa ushindi huo, Kenya imetimiza pointi saba baada ya awali kuifunga Sudan Kusini 3-1 na kutoa sare ya bila kufungana na Ethiopia. Zanzibar ambayo sasa inabaki na pointi zake tatu, itatazama mustakabali wake wa kwenda Robo Fainali katika nafasi mbili za best losers. Rwanda ambayo haina pointi hadi sasa inaweza kuungana na timu moja ya kundi B pamoja na Zanzibar kuwania kufuzu katika nafasi za best losers, iwapo itaifunga Eritrea katika mchezo wake wa mwisho. Zambia, Tanzania Bara na Burundi timu mbili kati ya hizo zitafuzu moja kwa moja baada ya matokeo ya mechi za mwisho kesho na moja itaingia kwenye kapu la best losers.
Picha kwa hisani ya Bin Zubery.
Picha kwa hisani ya Bin Zubery.
MESSI, RONALDO WAGAWANA TUZO HISPANIA.
MSHAMBULIAJI nyota wa klabu ya Barcelona, Lionel Messi ametajwa kuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu nchini Hispania maarufu kama La Liga katika msimu wa 2012-2013 huku nyota wa Real Madrid Cristiano Ronaldo akipigiwa kura kama mchezaji mwenye thamani zaidi. Nyota huyo wa Barcelona ameshinda tuzo hiyo kwa mara ya tano mfululizo na pia kuchukua zawadi ya mshambuliaji bora, wakati mchezaji mwenzake Andres Iniesta kama mmoja wa viungo bora kwa mara ya nne kwa misimu mitano. Akipokea zawadi hiyo Ronaldo mwenye umri wa miaka 28 alishukuru wachezaji wenzake wa Madrid kwani bila wao kumsaidia asingeweza kupata zawadi hiyo. Tuzo hizo zimekuja ikiwa zimebaki siku zoezi la upigaji kura kusitishwa kwa ajili ya kuchagua mchezaji bora wa mwaka wa dunia ambapo Ronaldo na Franck Ribery ndio wanaopewa nafasi kubwa ya kutwaa tuzo hiyo.
TUNISIA YANYOOSHA MIKONO KWA FIFA.
SHIRIKISHO la Soka nchini Tunisia limesema halitakata rufani juu ya uamuzi wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA kutupilia mbali madai yao dhidi ya Cameroon ya kuchezesha wachezaji wasiostahili katika mchezo wa mtoano wa kufuzu Kombe la Dunia. Baada ya kupoteza kwa jumla ya mabao 4-1, Tunisia walilalamika Cameroon kuwatumia wachezaji Joel Matip na Eric-Maxim Choupo-Moting ambao wote wamezaliwa nchini Ujerumani wakiwa na baba Mcameroon na mama Mjerumani. Hata hivyo FIFA ilitupilia mbali madai hayo kwakuwa Cameroon hawakukiuka sheria yoyote kwa kuwachezesha wachezaji hao hivyo kuithibitisha Cameroon kushiriki m ichuano hiyo itakayofanyika mwakani. Vyombo vya habari jijini Tunis vimedai kuwa maofisa wa shirikisho hilo wameshindwa kupeleka suala hilo katika Mahakama ya Kimataifa ya Michezo-CAS kwasababu chombo hicho hakiwezi kuenda kinyume na maamuzi ya FIFA.
KOSCIELNY HURU KUCHEZA KOMBE LA DUNIA.
BEKI wa kimataifa wa Ufaransa, Laurent Koscielny anaweza kuanza katika kikosi cha nchi hiyo kitakachoshiriki michuano ya Kombe la Dunia baada ya kufungiwa mechi moja kutokana na kadi nyekundu aliyopata katika mchezo wa mtoano dhidi ya Ukraine. Msemaji wa FIFA aliliambia shirika la habari la AFP kuwa Koscielny alipewa adhabu hiyo ambayo tayari ameshaitumikia katika mchezo wa mkondo wa pili hatua ya mtoano ambapo Ufaransa ilishinda kwa jumla ya mabao 3-2. Beki huyo alipewa kadi nyekundu kwa vurugu mwishoni mwa mchezo wa mkondo wa kwanza ambao Ukraine iliifunga Ufaransa mabao 2-0 jijini Kiev na kulikuwa na wasiwasi kuwa angeweza kuongezewa adhabu zaidi itakayomfanya kushindwa kushiriki michuano ya Kombe la Dunia. Hata hivyo taarifa hizo itakuwa ahueni kwa kocha Didier Deschamps ambaye sasa anaweza kumjumuisha beki huyo katika kikosi chake kitakachokwenda nchini Brazil.
Subscribe to:
Posts (Atom)