Monday, March 3, 2014

MESSI HAWEZI KUMFIKIA MARADONA - ENRIQUE.

MCHEZAJI wa zamani wa kimataifa wa Argentina, Hector Enrique anaamini kuwa mshambuliaji wa Barcelona Lionel Messi hataweza kufikia kiwango alichokuwa nacho Diego Maradona enzi zake. Messi mwenye umri wa miaka 26 ambaye anatajwa kama mchezaji bora kabisa kuwahi kutokea katika historia ya soka akiwa ameshinda tuzo za Ballon d’Or mara nne huku akivunja rekodi za ufungaji katika klabu yake lakini Enrique hadhani kama nyota huyo anaweza kufikia kiwango kama cha Maradona. Enrique amesema Messi hamfikii Maradona hata kidogo, ingawa anampenda na angefurahi kama mwanae angecheza hata kwa asimilia moja kwa uwezo kama wa Messi lakini Maradoka walikuwa mchezaji wa kipekee. Nguli aliendelea kudai kuwa hakutatokea mchezaji kama Maradona tena hata kama Messi akifanikiwa kushinda mataji matatu ya Kombe la Dunia. Enrique alikuwepo katika kikosi cha Argentina kilichonyakuwa taji la michuano ya Kombe la Dunia mwaka 1986 akiwa sambamba na Maradona.

EL HADARY ATAMANI KUCHEZA KOMBE LA DUNIA 2018.

GOLIKIPA mkongwe wa kimataifa wa Misri, Essam El Hadary amedai kuwa anategemea kucheza michuano ya Kombe la Dunia itakayofanyika nchini Urusi mwaka 2018. El Hadary alirejea katika kikosi cha timu ya taifa ya nchi hiyo baada ya kukosekana kwa mwaka mmoja kwa kushindwa kuelewana na kocha wa zamani Bob Bradley. Akihojiwa El Hadary amesema ndoto zake ni kucheza michuano hiyo ya Urusi na hajali umri wake kwasababu anajua atafanya vyema akienda huko. Kipa huyo anayejulikana nchini humo kwa jina la utani la High Dam alizaliwa mwaka 1973 huko Damietta na sasa anakipiga katika klabu ya Ligi Kuu ya Wadi Degla. El Hadary mwenye umri wa miaka 41 hivi sasa aliendelea kudai kuwa amecheza soka toka mwaka 1993 na anajua kama ukicheza kwa juhudi basi lazima utapata nafasi.

MAYWEATHER AZIDI KUMKEJELI KHAN.

BONDIA Floyd Mayweather wa Marekani ameendeleza vita vya maneno na Amir Khan wa Uingereza kwa kudai kuwa atapigana na bondia huyo bingwa wa zamani wa dunia kama akifanikiwa kupiga Adrien Broner katika pambano lao. Khan mwenye umri wa miaka 27 alimshambulia Mayweather kwa kuchagua chaguo rahisi wakati alipochagua kupigana na Marcos Maidana badala yake. Mayweather aliwataka mashabiki wake kumchagulia bondia wa kupigana naye kwa kupiga kura na katika kura hizo Khan ndio aliibuka na asilimia kubwa ya kura lakini Mmarekani huyo akaamua kumchagua Maidana aliyepata kura chache. Mayweather aliandika katika mtandao wake wa kijamii wa twitter kuwa kama Khan akifanikiwa kumchapa Broner katika pambano lao ndipo naye atakapopambana naye.

TAARIFA MBALIMBALI KUTOKA TFF LEO.

KIKOSI CHA TAIFA STARS CHATUA WINDHOEK
Kikosi cha Taifa Stars kimeondoka leo alfajiri kwenda Windhoek, Namibia kwa ajili ya mechi ya kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) dhidi ya wenyeji itakayochezwa Machi 5 mwaka huu. Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager ina msafara wa watu 25 unaoongozwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Timu imefikia hoteli ya Safari jijini humo. Mechi hiyo itachezwa kwenye Uwanja wa Sam Nujoma, na kikosi cha Taifa Stars kipo chini ya Kaimu Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Salum Madadi ambaye ana leseni A ya ukocha inayotambuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF). Namibia (Brave Warriors) inayofundishwa na kocha Ricardo Mannetti imeingia kambini jana (Machi 2 mwaka huu) kwa ajili ya mechi hiyo ambayo tiketi zake zilianza kuuzwa Februari 28 mwaka huu.



MECHI YA YANGA, AHLY YAINGIZA MIL 488
Mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Yanga na Al Ahly kutoka Misri iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam mwishoni mwa wiki imeingiza sh. 448,414,000. Mapato hayo yametokana na watazamaji 50,202 waliokata tiketi kushuhudia pambano hilo kwa viingilio vya sh. 7,000, sh. 13,000, sh. 25,000 na sh. 35,000. Yanga ilishinda mechi hiyo kwa bao 1-0. Mgawo wa mapato hayo ulikuwa kama ifuatavyo; Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ni sh. 68,402,135.59, gharama za kuchapa tiketi ni sh. 10,343,219, waamuzi na kamishna sh. 14,665,930 na matangazo sh. 15,679,000. Uwanja sh. 50,898,557.31, gharama za mchezo sh. 33,932,371.54, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)/Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) sh. 33,932,371.54 wakati Yanga ilipata mgawo wa sh. 220,560,415.01. Nayo mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya Simba na Ruvu Shooting iliyochezwa jana (Machi 2 mwaka huu) imeingiza sh. 20,610,000 ambapo kila klabu ilipata mgawo wa sh. 4,402,492 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 3,143,898.31.



MECHI YA MLALE, LIPULI YARUDISHWA NYUMA
Mechi ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kati ya Mlale JKT na Lipuli iliyokuwa ichezwe Machi 9 mwaka huu Uwanja wa Majimaji mjini Songea sasa itachezwa Machi 5 mwaka huu. Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imefanya mabadiliko hayo ili kuipunguzia gharama timu ya Lipuli ya Iringa ambayo jana (Machi 2 mwaka huu) ilicheza mechi mjini Songea dhidi ya Majimaji.

BOSI WA BIRMIGHAM AKUTWA NA HATIA YA KUCHAKACHUA FEDHA.

MMILIKI wa klabu ya Birmingham City ya Uingereza, Carson Yeung amekutwa na hatia na mahakama ya Hong Kong kwa makosa matano ya kuchakachua fedha ambazo zimemfanya kuwa tajiri. Yeung ambaye amekana makosa hayo ya kuchakachua kiasi cha dola milioni 93 kati ya Januari mwaka 2001 na Desemba 2007, anatarajiwa kuhumiwa Ijumaa na anaweza akahukumiwa miaka saba jela. Tajiri huyo ambaye alikuwa mtaalam wa kutengenza nywele watu matajiri na maarufu huko Hong Kong aliiambia mahakama kuwa ametengeneza utajiri wake kupitia shughuli za kutengeneza nywele, kununua hisa, kununua nyumba, kucheza kamari pamoja na uwekezaji mwingine. Jaji aliyekuwa akisikiliza kesi iliyochukua muda wa siku 50 amesema amemkuta na hatia Yeung kwa kuidanganya mahakama jinsi alivyopata utajiri wake kwa kupitia utengenezaji nywele na kamari.

NYOTA WA NIGERIA AANGUKA UWANJANI HUKO UTURUKI.

MSHAMBULIAJI wa klabu ya Olympiakos Michael Olaitan anaendelea vizuri katika hospitali aliyolazwa nchini Ugiriki baada ya kuanguka katika kipindi cha kwanza katika mchezo dhidi ya mahasimu wao wa jiji la Athens Panathiakos. Nyota huyo wa kimataifa wa Nigeria mwenye umri wa miaka 21 alikuwa akikokota mpira wakati alipoanguka na kuzimia. Mapema katika mchezo huo meneja wa Panathiakos Yannis Anastasiou naye alianguka baada ya kupigwa kitu kilichorushwa kutoka kwa mashabiki. Olaitan ambaye aliisadia Olympiakos kuichapa Manchester United mabao 2-0 katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa barani Ulaya uliochezwa Februari 25 mwaka huu, alizinduka kabla hajapelekwa hospitalini kwa matibabu zaidi.

MOYES ANAHITAJI MUDA - FERGUSON.

KLABU ya Manchester United imekua ikisuasua katika msimu wake wa kwanza bila kocha wake wa zamani Sir Alex Ferguson huku kocha mpya wa klabu hiyo David Moyes akiwa na hatihati ya kushindwa kufuzu michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya. Pamoja na mwenendo mbaya wa timu hiyo ambao umepelekea mashabiki wengi kukiri kuwa Moyes hakustahili kibarua hicho hali ni tofauti kwa Ferguson ambaye anaamini kuwa kuyumba katika msimu wa kwanza ni jambo la kawaida. Akihojiwa wakati wa utoaji tuzo za filamu za Oscar huko jijini Los Angeles, Marekani kocha huyo mstaafu mwenye umri wa miaka 72 amesema hana shaka kwamba timu itakuja kubadilika na kwasasa sasa hivi ni mapema sana na kuna mambo mengi yamebadilika. Ferguson aliendelea kudai kuwa Moyes anahitaji muda kwani ameinoa klabu hiyo kwa miaka 27 hivyo kuja kwa meneja mpya itachukua muda kidogo lakini watarudi katika hali yao ya kawaida. Kocha huyo amejiwekea heshima ya kuwa kocha mwenye mafanikio zaidi katika soka nchini Uingereza katika miaka yake 27 aliyokaa Old Trafford ambapo alifanikiwa kunyakuwa mataji 13 ya Ligi Kuu na mawili ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya.