Tuesday, July 1, 2014

KOMBE LA DUNIA 2014: NEYMAR FITI KUIKABILI COLOMBIA.

MSHAMBULIAJI nyota wa Brazil, Neymar anategemewa kuwa fiti kwa ajili ya mchezo wa robo fainali ya michuano ya Kombe la Dunia dhidi ya Colombia utakaochezwa Ijumaa hii. Neymar mwenye umri wa miaka 22, alipata majeruhi ya paja la mguu wa kushoto na goti lake la kulia katika mchezo wa mtoano dhidi ya Chile ambao walishinda kwa changamoto ya mikwaju ya penati. Ofisa habari wa Shirikisho la Soka la Brazil, Rodrigo Paiva amesema majeruhi ya goti la Neymar ndio yaliyokuwa yakihofiwa sana lakini daktari wa timu Jose Luiz Runco amedai mashabiki hawapaswi kuwa na hofu kwani atakuwa fiti kwa ajili ya mchezo unaofuata. Paiva aliongeza kuwa Neymar anaweza kupumzishwa kufanya mazoezi kama itahitajika ikiwa ni juhudi za kumuweka fiti kabla ya mchezo wa Ijumaa.

KOMBE LA DUNIA 2014: KILA WA ALGERIA ADAI RAMADHANI HAIKUWA SABABU YA WAO KUTOLEWA NA UJERUMANI.

GOLIKIPA wa timu ya taifa ya Algeria, Rais M’Bolhi amesisitiza kuwa kipigo cha mabao 2-1 walichpata kutoka kwa Ujerumani katika muda nyongeza hakuhisiani na wachezaji wenzake kuwa katika mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani. Golikipa huyo ambaye alikuwa nyota wa mchezo huo kutokana na kuokoa michomo mingi sana ya Ujerumani katika muda wa kawaida kabla ya Andre Schurrle na Mesut Ozil hawajafunga mabao katika muda wa nyongeza na kuifanya Algeria kuondolewa katika michuano ya Kombe la Dunia inayoendelea nchini Brazil. Akihojiwa mara baada ya mchezo huo M’Bolhi amesema hadhani kama wachezaji kuwepo katika mfungo kulichangia wao kufungwa katika mchezo huo kwani walijiandaa kucheza kwa muda wowote ambao ungehitajika. M’Bolhi aliendelea kudai kuwa hakuna mtu yoyote ambaye aliamini kwamba wanaweza kucheza vyema kama walivyofanya ni bahati mbaya iliyowakuta na kuwafanya wakubali kufungwa mabao mawili katika muda wa nyongeza.

KOMBE LA DUNIA 2014: CAMEROON KUFANYIWA UCHUNGUZI TUHUMA ZA UPANGAJI MATOKEO.

MAOFISA wa Cameroon wanafanyia uchunguzi madai kuwa wachezaji wake saba walihusika na suala la upangaji matokeo katika michuano ya Kombe la Dunia inayoendelea nchini Brazil. Kamati ya nidhamu ya Shirikisho la Soka la Cameroon-Fecafoot inafanyia kazi tuhuma hizo za upangaji matokeo katika mechi tatu za hatua ya makundi walizocheza. Tuhuma hizo zimetolewa na gazeti moja la Ujerumani na Fecafoot wamenuia kuzifanyia kazi na kama ikigundulika kuna ukweli wahusika wote watachuliwa hatua stahiki. Cameroon alitandikwa katika mechi zao zote tatu katika kundi A, kikiwemo kipigo cha mabao 4-0 kutoka kwa Croatia.

KOMBE LA DUNIA 2014: KLINSMANN AIKOSOA FIFA KWA KUMTEUA MWAMUZI WA ALGERIA KUCHEZESHA MECHI YAO.

KOCHA wa timu ya taifa ya Marekani, Jurgen Klinsmann amelikosoa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA kwa kumteua mwamuzi wa Algeria kuchezesha mchezo wao wa hatua ya mtoano wa Kombe la Dunia dhidi ya Ubelgiji baadae leo. Marekani walifunga bao la ushindi katika dakika za majeruhi kwenye michuano hiyo miaka minne iliyopita na kuwafanya kuongoza kundi lao mbele ya Uingereza na Klinsmann amesema uteuzi wa mwamuzi huyo Djamel Haumoudi hajaridhika nao. Klinsmann amesema hajaridhika na uamuzi huo kutokana na ukweli kuwa waliifunga Algeria katika michuano ya Kombe la Dunia iliyopita. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa anajua mwamuzi huyo amechezesha mechi mbili zilizopita vizuri hivyo ni mategemeo yake na mchezo huo ataumudu vyema.

HATIMAYE SUAREZ AOMBA RADHI KWA UPUUZI WAKE.

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Uruguay na klabu ya Liverpool Luis Suarez ameibuka na kumuomba radhi beki wa Italia Giorgio Chiellini kufuatia tukio la kumng’ata wakat timu zilipokutana katika mechi za mwisho za makundi katika michuano ya Kombe la Dunia inayoendelea nchini Brazil. Suarez alitumia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter kuomba radhi kutokana na tukio hilo baada ya kutulia nyumbani na familia yake na kugundua kuwa hakufanya kitendo cha uungwana na hatarudia tena. Nyota huyo aliendelea kuandika kuwa anajutia sana tukio hilo na anamuomba radhi Chiellini huku akikiri kutorudia tena kitendo hicho. Shirikisho la Soka Duniani-FIFA lilimpa adhabu Suarez ya kutojishughulisha na mambo yoyote yahusuyo mchezo wa soka kwa muda wa miezi minne sambamba na kumfungia mechi tisa za kimataifa pamoja na faini ya paundi 65,000. Katibu mkuu wa FiFa Jerome Valcke alimtaka Suarez atafute matibabu ya kisaikolojia wakati akitumikia adhabu hiyo ili asiweze kurudia tena kitendo hicho ambacho amekifanya zaidi ya mara mbili kwa nyakati tofauti.

KOMBE LA DUNIA 2014: KESHI AAMUA KUACHIA NGAZI BAADA YA KIPIGO CHA UFARANSA.

KOCHA wa timu ya taifa ya Nigeria, Stephen Keshi amejiuzulu wadhfa wake huo mara baada ya imu hiyo kuondolewa katika michuano ya Kombe la Dunia kwa kufungwa mabao 2-0 na Ufaransa. Kocha huyo mwenye umri wa miaka 52 alichukua mikoba ya kuinoa Super Eagles mwaka wa 2011 na akaiongoza timu hiyo kutwaa Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka jana. Nahodha wa timu hiyo Joseph Yobo aliyejifunga bao la pili kwenye mchezo huo naye pia ametangaza kustaafu. Chini ya uongozi wake Super Eagles imefuzu kwa mara ya kwanza hatua ya mtoano katika michuano hiyo toka walipofanya hivyo mwaka 1998, licha ya migomo ya mara kwa mara ya wachezaji wake wakidai malimbikizo ya posho zao. Kujiuzulu kwa Keshi kunafanya idadi ya makocha waliojiuzulu kufuatia matokeo duni ya timu zao katika michuano ya Kombe la Dunia kufikia sita. Makocha wengine waliondoka ni pamoja na Luis Suarez wa Honduras, Carlos Queiroz wa Iran, Alberto Zaccheroni wa Japan , Cesare Prandelli wa Italia na Sabri Lamouchi wa Ivory Coast.

KOMBE LA DUNIA 2014: FIFA YAMSIMAMISHA OFISA HABARI WA BRAZIL.

OFISA habari wa Shirikisho la Soka la Brazil, Rodrigo Paiva amesimamishwa na Shirikisho la Soka Duniani-FIFA kufuatia tukio la kumpiga mchezaji wa Chile Mauricio Pinilla wakati wa mchezo baina ya timu hizo uliochezwa Jumamosi iliyopita. Paiva anatarajiwa kuukosa mchezo wa Ijumaa wa robo fainali utakaikutanisha Brazil na Colombia kutokana na FIFA kuendelea na uchunguzi wa tuhuma za kumpiga Pinilla katika muda wa mapumziko. Paiva amejitetea kuwa alikuwa akijilinda kwa kumsukuma mchezaji huyo wakati alipomkaribia, wakati wakienda katika vyumba vya mapumziko. Katika mchezo huo Brazil ilifanikiwa kuifunga Chile kwa changamoto ya mikwaju ya penati baada ya timu hizo kutoka sare ya kufungana bao 1-1 katika muda wa kawaida na wa nyongeza.