Monday, December 1, 2014

GRANT KUANIKA MIPANGO GHANA JUMATANO.

KOCHA mpya wa timu ya taifa ya Ghana, Avram Grant ameanza kazi rasmi leo huku akitegemewa kuweka mikakati yake katikati ya wiki. Jumatano kocha huyo wa zamani wa Chelsea raia wa Israel anatarajiwa kuzungumza na wanahabari ili kuweka maono na mipango yake kwa soka la Ghana. Mkataba rasmi wa kocha huyo unaanza kufanya kazi leo lakini Chama cha Soka cha Ghana kimethibitisha kuwa tayari kocha huyo ameshatua na ataanza rasmi kibarua chake hicho kesho. Moja ya kibarua atakachokuwa nacho Grant mwenye umri wa miaka 59 ni kusaidia kujenga shule ya soka ya kitaifa na pia kusaidia mafunzo ya makocha wazawa wan chi hiyo. Grant ana wiki sita za kukiandaa kikosi kipya cha Ghana kwa ajili ya michuano ya Mataifa ya Afrika itakayofanyika huko Guinea ya Ikweta mapema mwakani.

SHABIKI MMOJA AFARIKI KATIKA VURUGU HISPANIA KABLA YA MCHEZO WA ATLETICO NA DEPORTIVO.

SHABIKI mmoja amefariki dunia baada ya vurugu kati ya mashabiki kabla ya mchezo wa La Liga kati ya Atletico Madrid dhidi ya Deportivo La Coruna jana. Shabiki huyo wa Deportivo anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 43aliondolewa katika mto karibu na Uwanja wa Vincente Calderon unaomilikiwa na Atletico akiwa amepatwa na mshituko wa moyo, baridi yabisi na majeraha ya kichwani na kufia hospitalini. Watu saba wangine walitibiwa majeraha madogo madogo akiwemo polisi mwanamke kutokana na vurugu hizo. Watu 20 walikamatwa na polisi huku wengine 100 walioanzisha vurugu hizo nao wakitambuliwa. Vurugu hizo zimelaaniwa vikali na vilabu vyote viwili pamoja na maofisa wa La Liga. Baadae katika mchezo huo Atletico walishinda kwa mabao 2-0 ukiwa ni ushindi wao watano mfululizo na kuwasogelea vinara wa La Liga Real Madrid kwa tofauti ya alama nne.

APPIAH AMTEUA SWAHIBA WAKE KUMSAIDIA KAZI HUKO SUDAN.

KOCHA wa zamani wa timu ya taifa ya Ghana, Kwesi Appiah amemteua rafiki yake wa siku nyingi Prince Owusu kuwa msaidizi wake katika kibarua chake kipya huko nchini Sudan. Mara baada ya kuteuliwa kuwa kocha wa klabu ya Al-Khartoum Appiah aliamua kumvuta Owusu kuwa msaidizi wake baada ya wawili hao kufanya kazi pamoja kwa kipindi kirefu sasa. Owusu sio mgeni sana nchini Sudan kwani mara kadhaa amekuwa akiteuliwa kwenda huko kwa ajili ya mafunzo mafupi ya makocha. Wawili hao wanatarajiwa kusafiri kuelekea nchini Sudan Desemba 10 mwaka huu tayari kuanza kazi yao hiyo mpya. Al-Khartoum iko katika nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu nchini humo na wanatarajiwa kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho mwakani.

GERRARD KUPEWA MKATABA MPYA - RODGERS.

MENEJA wa klabu ya Liverpool, Brendan Rodgers amesema timu hiyo tayari imeshamuofa mkataba mpya kiungo na nahodha wao Steven Gerrard. Kocha huyo pia alikanusha tetesi za kutoelewana na Gerrard ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu. Akizungumza kabla ya mchezo wao wa kesho wa Ligi Kuu dhidi ya Leicester, Rodgers amesema hakuna ugomvi wowote kati yake na Gerrard na kudai hayo yanayosemwa hayana ukweli wowote. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa Gerrard atapewa muda wa kufikiria ofa hiyo mpya lakini amedai pesa haitakuwa tatizo. Rodgers amesema amekuwa akifurahia kila dakika kufanya kazi na Gerrard na ni matumaini yake ataendelea kuitumikia klabu hiyo.

ENRIQUE AKEMEA VURUGU ZA MASHABIKI BAADA YA MESSI KUPIGWA CHUPA.

MENEJA wa klabu ya Barcelona, Luis Enrique amesema vilabu nchini Hispania vinapambana dhidi ya mashabiki wanaojaribu kufanya vurugu wakati wa mechi. Kauli hiyo ya Enrique imekuja kufuatia Lionel Messi kupigwa na chupa ya plastiki wakati akishangilia ushindi dhidi ya Valencia katika mchezo wa La Liga uliochezwa jana. Messi hakuumia katika tukio lakini Enrique amesema kinachotokea ndani ya uwanja kinaweza kuzuiliwa. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa unaweza kuwa na mtu yeyote ambaye anatamani kuanzisha vurugu lakini wanapamabna na kupinga matukio hayo.

BOTAFOGO YASHUKA DARAJA BRAZIL.

KLABU kongwe ya Botafogo yenye maskani yake jijini Rio de Janeiro imeteremka daraja baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Santos jana. Ushindi huo wa Santos unaifanya klabu hiyo kuporomoka daraja kwa mara ya pili katika historia yake ya miaka 110 toka ianzishwe. Mara ya kwanza kushuka daraja kabla ya kupanda ilikuwa ni mwa 2003. Huku kukiwa kumebaki mechi moja kabla ya Ligi Kuu ya Brazil haijamalizika Botafogo wanashikilia nafasi ya pili kutoka mkiani katika msimamo wa timu 20 wakiwa wamejikusanyia alama 33. Kabla ya mchezo wa jana Botafogo walikuwa wakihitaji alama sita ili kujinasua katika mstari wa kushuka daraja lakini kipigo cha jana kimefuta matumaini hayo. Klabu ya Cruzeiro ndio waliotawadhwa mabingwa wa Ligi Kuu ya nchi hiyo kwa pili mfululizo wiki iliyopita.

ORODHA YA WATAKAOGOMBEA TUZO YA MCHEZAJI BORA WA MWAKA WA AFRIKA HADHARANI.

SHIRIKISHO la Soka barani Afrika-CAF limetangaza orodha ya wachezaji watano watakaogombea tuzo ya mchezaji ya mchezaji bora wa mwaka wa Afrika. Kabla ya kufanya mchujo CAf ilitoa majina majina ya wachezaji ya wachezaji 25 wa Afrika wanaocheza ligi mbalimbali duniani kote. Watano waliopenya ni pamoja na Vincent Enyeama na Ahmed Musa wa Nigeria, Asamoah Gyan wa Ghana, Pierre-Emerick Aubemeyang wa Gabon na na nyota nayeshikilia tuzo hiyo kwasasa Yaya Toure kutoka Iviry Coast. Majina hayo yatachujwa tena na kubakia matatu kabla ya sherehe za utoaji tuzo za CAF zitakazofanyika jijini Lagos Januari 8 mwaka huu. Mbali na orodha hiyo CAF pia iliteua orodha ya wachezaji watano ambao wanasakata kabumbu ndani ya bara la Afrika watakaogombea tuzo hiyo.