Monday, March 2, 2015

FEYENOORD YAANZA MAWINDO YA KOCHA MPYA.

KLABU ya Feyenoord inatarajia kuanza kutafuta kocha mpya baada ya Fred Rutten kutangaza kuwa anataka kuondoka katika klabu hiyo mwishoni mwa msimu huu. Rutten mwenye umri wa miaka 52 alichukua mikoba ya kuinoa ya timu hiyo kutoka kwa Ronald Koeman na kupewa mkataba wa mwaka mmoja kiangazi mwaka jana. Hata hivyo, kocha huyo amekuwa na akitofautiana na uongozi wa Feyenoord kuhusiana na mipango ya maendeleo. Akihojiwa Rutten amesema wote wamekuwa na malengo sawa lakini linafika suala la utekelezaji ili waweze kusonga mbele ndipo wanapotofautiana ndio maana ameamua kuachia ngazi mwishoni msimu.

MEIER AMGWAYA ROBBEN KATIKA MBIO ZA KUGOMBEA KIATU CHA DHAHABU BUNDESLIGA.

MSHAMBULIAJI wa klabu ya Eintracht Frankfurt, Alexander Meier hana shaka kuwa mshambuliaji wa Bayern Munich Arjen Rooben atakuja kuwa mfungaji bora wa Bundesliga msimu huu. Nyota huyo wa kimataifa wa Uholanzi kwasasa ndio anaongoza orodha ya wafungaji akiwa na mabao 17 katika mechi 19 alizocheza lakini Meier anamfuata kwa karibu akiwa nyuma yake kwa tofauti ya bao moja. Hata hivyo, Meier hadhani kama anaweza kupambana dhidi ya mshambuliaji huyo na ana hofu anaweza kubakia katika nafasi hiyohiyo ya pili. Nyota huyo amesema itakuwa ngumu kumshika Robben kwasababu katika mchezo mmoja ana uwezo wa kufunga bao moja au mawili. Robben na Meier ndio wachezaji pekee walioko katika mbio za kugombea taji la mfungaji bora wa Bundesliga msimu huu.

MALI MABINGWA WAPYA WA AFRIKA KWA VIJANA CHINI YA UMRI WA MIAKA 17.

MALI wametawadhwa mabingwa wapya wa michuano ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 baada ya kufanikiwa kuichapa Afrika Kusini kwa mabao 2-0 katika mchezo wa fainali uliofanyika huko Niemey Jumapili hii. Mabao ya kipindi cha pili yaliyofungwa na Siaka Bagayoko na Aly Malle yalitosha kuihakikishia Mali ushindi muhimu. Hiyo ni mara ya kwanza katika historia kwa Mali kunyakuwa taji hilo la mashindano ya vijana. Mara ya mwisho Mali kukaribia kunyakuwa taji hilo ilikuwa ni mwaka 1997 wakati walipomaliza kama washindi baada ya kufungwa na Botswana. Kwa kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo, Mali, Afrika Kusini, Guinea na Nigeria wote wamefuzu michuano ya Kombe la Dunia kwa vijana wa umri huo ambayo itafanyika nchini Chile Octoba mwaka huu.

INTER TADAI HATA EURO MILIONI 40 HAZIWEZI KUMNG'OA ICARDI.

MKURUGENZI wa michezo wa Inter Milan, Piero Ausilio amesisitiza kuwa hata euro milioni 40 hazitarajiwa kutosha kumng’oa Mauro Icardi katika klabu hiyo. Icardi mwenye umri wa miaka 22 amekuwa katika kiwango kizuri msimu huu akiwa amefunga mabao 14 katika mechi 24 za Serie A walizocheza. Hata hivyo, pamoja na vilabu mbalimbali kuanza kumuwinda nyota huyo, Inter inamuona kama mchezaji muhimu kwao na hawana mpango wowote wakumuuza hivi sasa. Ausilio amesema kwasasa wanatengeneza timu ambayo itadumu kwa kipindi kirefu hivyo hawana mpango wa kuuza wachezaji wao muhimu wanaochipukia. Nyota huyo wa kimataifa wa Argentina ambaye amewahi pia kucheza katika timu za Sampdoria na Barcelona ana mkataba na Inter unapomalizika Juni mwaka 2018.

HENRY AIPIGIA CHAPUO CHELSEA KUPATA MATAJI ZAIDI.

MSHAMBULIAJI wa zamani wa klabu ya Arsenal, Thierry Henry anaamini Chelsea wana uwezo wa kuongeza mataji zaidi msimu huu baada ya kunyakuwa taji la Kombe la Ligi jana. Chelsea jana walifanikiwa kuichapa Tottenham Hotspurs kwa mabao 2-0 katika fainali iliyofanyika katika Uwanja wa Wembley. Henry ambaye kwasasa anafanya kazi kama mchambuzi wa soka amesema anadhani Chelsea wanaweza kuongeza mataji zaidi likiwemo la Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Ulaya. Henry aliendelea kudai kuwa wana ubora ambao unahitajika kufanya hivyo ndio maana haoni sababu ya kushindwa kufikia malengo hayo.

ROONEY AMKINGIA KIFUA DI MARIA.

NAHODHA wa Manchester United, Wayne Rooney amesema Angel Di Maria atarejea katika kiwango chake pamoja na hivi sasa kuonekana kuwa chini ya kiwango. Baada ya kuanza vyema alipotua Old Trafford, Di Maria ambaye alisajiliwa kwa kitita cha paundi milioni 59.7 kutoka Real Madrid hivi karibuni ameshindwa kuonyesha cheche zake kama alivyozoeleka. Rooney mwenye umri wa miaka 29 amesema Di Maria ni mchezaji bora na hakuna mchezaji anayepoteza kiwango kwa usiku mmoja. Rooney aliendelea kudai kuwa ana uhakika kuwa Di Maria atarejea katika kiwango chake na kuendelea kuifanyia mazuri timu hiyo.

MOURINHO ATAKA MATAJI ZAIDI CHELSEA.

MENEJA wa klabu ya Chelsea, Jose Mourinho amedhamiria kutafuta mataji zaidi baada ya kunyakuwa taji la Kombe la Ligi jana ikiwa ni la kwanza kwa kocha huyo toka achukue mikoba ya kuinoa timu hiyo kwa mara ya pili. Mabao yaliyofungwa na Joh Terry na linguine la kujifunga la Kyle Walker yalitosha kuipa ushindi wa mabaop 2-0 Chelsea dhidi ya Tottenham Hotspurs katika mchezo wa fainali uliofanyika katika Uwanja wa Wembley. 
Taji hilo linakuwa la 21 kwa Mourinho toka aanze kufundisha soka. Akihojiwa Mourinho amesema anajiona kama mtoto aliyeshinda kwa mara ya kwanza kwani mara zote imekuwa ngumu kwake kuishi bila mataji. Mourinho ambaye kwa mara ya kwanza amewahi kuinoa Chelsea mwaka 2004 hadi 2007 kabla ya kurejea tena mwaka 2013, hilo linakuwa taji lake la saba akiwa na timu hiyo.