Saturday, May 2, 2015

MKE WA RIO FERDINAND AFARIKI KWA SARATANI.

NAHODHA wa zamani wa kimataifa wa Uingereza, Rio Ferdinand ametangaza kufiwa na mke wake aitwaye Rebecca aliyekuwa akisumbuliwa na maradhi ya saratani. Rebecca mwenye umri wa miaka 35 ambaye ni mama wa watoto watatu alifariki dunia katika hospitali ya Royal Marsden iliyopo jijini London baada ya kuugua maradhi hayo kwa kipindi kifupi. 
Ferdinand ambaye anakipiga katika klabu ya Queens Park Rangers-QPR alitangaza taarifa huku akiishukuru familia yake na wachezaji wenzake kuwa karibu naye katika kipindi chote cha kuuguza. 
Beki huyo wa zamani wa Manchester United amesema daima atamkumbuka mkewe huyo kwa upendo wake na zawadi kubwa aliyomuachia ya watoto wao watatu.

WACHEZAJI WA LOKEREN WAJIPANGA KUTOA HESHIMA KWA GREGORY MERTENS.

WACHEZAJI wa klabu ya Lokeren walitoa heshima zao kwa mchezaji mwenzao Gregory Martens wakati waliporejea uwanjani tena jana, siku moja baada ya beki huyo kufariki dunia akiwa na umri wa miaka 24. Kabla ya mchezo huo wa Ligi Kuu ya Ubelgiji maarufu kama Pro League waliocheza dhidi ya timu ya Westerlo, kikosi cha Lokerene kilijipanga huku wote wakiwa na fulana zenye jina la Gregory huku wachezaji wengine wakishindwa kujizuia na kulia. Hata hivyo, pamoja na majonzi hayo Lokeren walichapwa mabao 4-3 na Westerlo katika mchezo huo. Mertens alianguka uwanjani wakati kikosi cha wachezaji wa akiba wa Lokeren kilipokuwa kikicheza na Genk Jumatatu iliyopita na kufariki kwa moyo wake kushindwa kufanya kazi baada ya siku kadhaa za usaidizi wa mashine.

WENGER AHOFIA KUMKOSA SANCHEZ MSIMU UJAO.

MENEJA wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger anategemea Alexis Sanchez kuwepo katika mchezo wa fainali ya Kombe la FA lakini anahofu mshambuliaji huyo anaweza kukosa mwanzo wa msimu ujao. Wenger amesema kuna makubaliano ya kuizuia Chile kumuita nyota wake huyo mapema kwa ajili ya michuano ya Copa America ambayo watakuwa wenyeji. Hatua hiyo inamaanisha Sanchez atakuwepo kwa ajili ya mchezo huo wa FA ambao watavaana na Aston Villa katika Uwanja wa Wembley Mei 30 mwaka huu lakini mafanikio ya Chile katika michuano hiyo ambayo itamalizika Julai 4 yanaweza athari. Wenger amesema kama Chile watafika mbali katika michuano hiyo inamaanisha watamkosa Sancheza mwanzoni mwa msimu. Sanchez mwenye umri wa miaka 26 amekuwa mchezaji muhimu katika kikosi cha Arsenal msimu huu akiwa amefunga mabao 18 toka aliponunuliwa kwa paundi milioni 32 kutokea Barcelona baada ya michuano ya Kombe la Dunia.

DROGBA AANZA KUCHONGA.

MSHAMBULIAJI mkongwe wa Chelsea, Didier Drogba amekiri kuwa yeye pamoja na wachezaji wenzake walikuwa wakijua mapema mwezi Machi kuwa tayari wameshaukaribia ubingwa wa Ligi Kuu. Chelsea inaweza kutangaza ubingwa kama wakifanikiwa kuichapa Crystal Palace katika mchezo wa kesho. Akihojiwa Drogba amesema walijua mapema kuwa watakuwa mabingwa wakati aliponyakuwa taji la Kombe la Ligi Machi mosi mwaka huu taji ambalo pia walishinda wakiwa mbioni kushinda taji la kwanza ligi wakiwa chini umiliki wa Roman Abramovic mwaka 2005. Mkongwe huyo mwenye umri wa miaka 37 aliendelea kudai kuwa msimu wa 2004-2005 ulikuwa tofauti kidogo kwasababu walikuwa na wachezaji wengi waliokomaa na wenye uzoefu zaidi kulinganisha na mwaka huu. Drogba amefanikiwa kushinda taji la Ligi Kuu akiwa na Chelsea mwaka 2005, 2006 na 2010.

BALE FITI KUIVAA SEVILLA.

MENEJA wa Real Madrid, Carlo Ancelotti amesema wanatarajiwa Gareth Bale kuwepo katika mchezo wa La Liga dhidi ya Sevilla baada ya kupona majeruhi. Winga huyo wa kimataifa wa Wales, amekuwa akizumbuliwa na majeruhi hayo kwa wiki kadhaa na sasa anaweza kurejea katika mchezo unahesabika kuwa kwa mgumu kwa timu hiyo kuliko michezo yao yote minne iliyobakia msimu huu. Akihojiwa Ancelotti amesema Bale amekuwa akifanya mazoezi na kikosi cha kwanza na anadhani atakuwepo katika mchezo dhidi ya Sevilla. Kocha aliendelea kudai kuwa Benzema kwasasa yuko fiti kuliko baadhi ya wachezaji kwani amepumzika vyema na anaweza kuwasaidia katika mchezo huo muhimu.

VIWANJA VYA KOMBE LA DUNIA VYAKAMILIKA MIEZI BAADA YA MICHUANO HIYO.

HATIMAYE baadhi ya viwanja vya Kombe la Dunia nchini Brazil vimekamilika miezi 10 baada ya michuano hiyo kumalizika. Viwanja hivyo vilivyokamilika kufikia jinsi vilivyotakiwa ni Uwanja wa Itaquerao uliopo jijini Sao Paulo na Arena da Baixada uliopo Curitiba. Pamoja na kutokamilika kwake viwanja hivyo vyote vilitumika wakati wa Kombe la Dunia ambalo lilibebwa na Ujerumani. Brazil ilitumia zaidi ya dola bilioni 3 kwa ajili ya ujenzi wa viwanja vya michuano hiyo huku waandamanaji wakipinga kiasi kikubwa wa cha fedha zilizotumika katika ujenzi huo.

BAADA YA KUPIMA UZITO JANA USIKU SASA MAYWEATHER NA PACQUAIO WAKO TAYARI KUZICHAPA.

MABONDIA mahiri Floyd Mayweather na Manny Pacquiao wamepima uzito jana mbele ya mashabiki 11,500 waliohudhuria shughuli hiyo kuelekea katika pambano la kihistoria linalotarajiwa kufanyika jijini Las Vegas leo usiku au alfajiri ya kuamkia kesho kwa saa za hapa nyumbani. Viingilio kwa mashabiki waliofurika kushuhudia mabondia hao wakipima uzito vilikuwa dola ingawa tiketi hizo zilikuja kulanguliwa mpaka dola 800. Pambano linalotajwa kuingiza fedha nyingi katika historia linakadiriwa kutengeneza zaidi ya dola milioni 400. Mayweather wa Marekani na Pacquiao wa Philippines watakuwa wakishindania mikanda ya dunia ya WBC, WBA na WBO uzito wa welter. Akihojiwa Mayweather amecheza mapambano 47 bila kupigwa, amesema anaamini uwezo wake na mbinu zake hivyo lazima ataibuka kidedea katika pambano hilo. Kwa upande wake Pacquiao ambaye ameshinda mapambano 57 na kupigwa matano katika mapambano 64 aliyocheza, amesema ni jukumu lake kubwa kuwapa furaha mashabiki haijalishi kama mashabiki wake au wa mpinzani wake.