Tuesday, January 5, 2016

MAELFU YA MASHABIKI WAJITOKEZA KUMLAKI ZIDANE WAKATI AKIANZA KAZI KUINOA MADRID.

MAELFU ya mashabiki wa Real Madrid wamejitokeza katika uwanja wa mazoezi wa Valdebebas kumlaki na kumkaribisha meneja mpya Zinedine Zidane wakati akianza kibarua chake cha kukinoa kikosi cha kwanza. Zidane mwenye umri wa miaka 43 alitangazwa kuwa mbadala wa Rafa Benitez katika klabu hiyo jana, hatua ambayo imeonyesha kuwavuta mashabiki. Nguli huyo wa soka wa zamani wa Ufaransa, anakiandaa kikosi chake kwa ajili ya mchezo wa kwanza akiwa meneja dhidi ya Deportivo La Coruna katika Uwanja wa Santiago Bernabeu Jumamosi hii. Madrid kwasasa wanashikilia nafasi ya tatu katika msimamo wa La Liga, alama mbili nyuma ya mahasimu wao Barcelona na nne nyuma ta vinara Atletico Madrid. Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa mikoba hiyo, Zidane amesema atafanya kazi kwa bidii na wachezaji wote na anadhani mambo yatakwenda sawa kama akipata ushirikiano wa kutosha. Akiwa mchezaji Zidane amewahi kushinda Kombe la Dunia akiwa na Ufaransa mwaka 1998, pamoja na La Liga mwaka 2003 na Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2002 akiwa na Madrid. Pia amewahi kushinda mataji mawili ya Serie A katika kipindi cha miaka mitano aliyoichezea Juventus.

BARCELONA YATHIBITISHA KUSAJILI 77 BAADA YA KUTOKA KIFUNGONI.

KLABU ya Barcelona imeanza kufanya usajili kwa kishindo baada ya kumaliza adhabu yao ya kutosajili waliyopewa na Shirikisho la Soka Duniani-FIFA. Barcelona walifungiwa kutosajili kwa miezi 14 na FIFA kufuatia kukutwa na hatia ya kuvunja sheria katika usajili wa wachezaji chini ya miaka 18 waliofanya. Lakini sasa adhabu hiyo imekwisha na Barcelona sasa wameingia tena katika usajili kwa kuwaandikisha wachezaji wapya 77 katika vikosi mbalimbali vya timu hiyo kulingana na umri. Katika orodha hiyo wapo wachezaji wenye majina makubwa walioandikishwa akiwemo Arda Turan aliyetoka Atletico Madrid na Aleix Vidal katika timu ya Sevilla. Jana zaidi ya mashabiki 10,000 walijitokeza katika uwanja wa mazoezi kuishuhudia timu yao pamoja na kuwakaribisha Turan na Vidal.

ROONEY ALAMBA TUZO UINGEREZA.

NAHODHA wa kimataifa wa Uingereza na klabu ya Manchester United, Wayne Rooney amechaguliwa kwa mara nyingine kuchukua tuzo ya mchezaji bora wa mwaka jana wa nchi hiyo. Nyota huyo alipata asilimia 37 ya kura zote zilizopigwa na mashabiki wa nchi hiyo na kumfanya kushinda tuzo hiyo kwa mara ya nne. Rooney aliifungia Uingereza mabao matano mwaka jana, na kumpita Sir Bobby Charlton kwa kuweka rekodi ya ufungaji wakati wa mechi za kufuzu michuano ya Euro 2016. Kwa upande mwingine golikipa wa Stoke City, Jack Butland naye amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwaka kwa wachezaji wa chini ya umri wa miaka 21. Wawili hao watakabidhiwa zawadi zao kabla ya mchezo ujao wa Uingereza Machi mwaka huu.

AC MILAN YAMSAJILI TENA BOATENG.

KIUNGO wa kimataifa wa Ghana, Kevin-Prince Boateng amesajiliwa tena na klabu ya AC Milan kama mchezaji huru. Boateng amerejea San Siro kwa mkataba wa miezi sita mpaka mwishoni mwa msimu huu lakini ana nafasi ya kuongezewa mwingine. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 28 mzaliwa wa Ujerumani, ambaye mara ya kwanza aliiwakilisha Milan kati ya mwaka 2010 hadi 2013 amekuwa akifanya mazoezi na Milan toka Septemba mwaka jana. Boateng alisimamishwa katika klabu yake ya Schalke ya Ujerumani kutokana na makosa ya utovu wa nidhamu hivyo kumfanya kutocheza mechi yeyote toka kuanza kwa msimu huu.

STURRIDGE AANZA MWAKA NA MAJANGA.

MSHAMBULIAJI wa Liverpool, Daniel Sturridge anatarajiwa kuukosa mchezo wa mkondo wa kwanza wa Kombe la Ligi dhidi ya Stoke City baadae leo kufuatia kupata majeraha madogo akiwa mazoezini. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 26, amekuwa akisumbuliwa na majeruhi ya mara ya mara ambayo yamemfanya msimu uliopita kucheza mechi 19 na msimu huu mechi sita pekee. Meneja wa Liverpool, Jurgen Klopp ana mshambuliaji mmoja pekee Christian Benteke ambaye yuko fiti huku Divock Origi na Danny Ings nao pia wakiwa majeruhi. Kwa upande wa Stoke, Geoff Cameron atakuwepo katika mchezo wa kesho pamoja na kutolewa nje Jumamosi iliyopita. Beki huyo wa kimataifa wa Marekani alionyeshwa kadi nyekundu katika mchezo Ligi Kuu ambao Stoke walifungwa mabao 2-1 na West Bromwich Albion.

KUKOSA NAMBA NDIO KULIMUONDOA VILLA BARCELONA.

MSHAMBULIAJI wa zamani wa Barcelona, David Villa amekiri aliondoka katika klabu hiyo kutokana na kukosa nafasi ya kutosha ya kucheza lakini amebainisha kuwa alikuwa na mapenzi makubwa na timu hiyo. Villa ambaye kwasasa anakipiga katika klabu ya New York City FC, alihamia Atletico Madrid mwaka 2013 baada ya kucheza kwa misimu mitatu Camp Nou na kufanikiwa kushinda mataji mawili ya La Liga na moja la Ligi ya Mabingwa Ulaya. Akihojiwa Villa amekiri kuwa kikubwa kilichochangia kuondoka Barcelona ni kupoteza nafasi yake katika kikosi cha kwanza. Villa amesema alipenda kucheza mara zote hivyo alipopoteza nafasi yake ya kuanza kwenye kikosi cha kwanza aliamua kuondoka ili kutafuta mahali ambapo atapata muda huo zaidi.

SEVILLA WAMNG'ANG'ANIA IMMOBILE.

RAIS wa Sevilla, Jose Castro amesisitiza na kuamuru kuwa mshambuliaji Ciro Immobile hatauzwa pamoja na ofa kadhaa zilizotolewa na klabu za Italia. Immobile alijiunga na Sevilla akitokea Borussia Dortmund katika kipindi cha majira ya kiangazi mwaka jana lakini amefunga mabao mawili pekee toka awasili. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 25 alifunga mabao 22 katika msimu wa 2013-2014 wakati akiwa Torino kabla ya kuhamia Ujerumani, ingawa hata hivyo pamoja na kukosa mafanikio bado ameendelea kuwindwa na vilabu vya nyumbani kwao. Castro amesema wamepokea ofa kadhaa kutoka Italia kwa ajili ya Immobile lakini hawana mpango wowote wa kumuuza hivi sasa.