Monday, May 2, 2016

MECHI YA NDANDA NA YANGA YARUDISHWA NYUMA.

Mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kati ya Ndanda FC ya Mtwara na Young Africans umerudishwa nyuma kwa siku moja na sasa itachezwa Mei 14, 2016 badala ya Mei 15, 2016 kama ratiba ya awali inavyosomeka. Taarifa ya Bodi ya Ligi Kuu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imesema sababu za kurudisha nyuma mchezo huo Na. 218 utakaofanyika Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara ni kuipa timu ya Young Africans nafasi ya kujiandaa na kusafiri kwenda nchini Angola kwenye mchezo wa kimataifa wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika. Mbali ya mechi hiyo, kuna michezo miwili ambayo imesogezwa mbele kwa siku moja. Mechi hizo ni kati ya Simba na Mwadui ambayo sasa itachezwa Mei 8, 2016 badala ya Mei 7, 2016. Sababu za mchezo huo kusogezwa mbele ni kwamba Mei 7, 2016 kutakuwa na mchezo wa kimataifa utakaozikutanisha Young Africans dhidi ya Esperanca ya Angola kuwania Kombe la Shirikisho. Mchezo mwingine uliosogezwa mbele ni kati ya Kagera Sugar dhidi ya Azam FC ambao sasa utafanyika Mei 8, 2016 badala ya Mei 7, 2016. Sababu za mchezo huo kusogezwa mbele ni Uwanja wa Kambarage Shinyanga. Mei 7, 2016 uwanja huo utakuwa na mchezo kati ya Stand United ya Shinyanga dhidi ya Coastal Union ya Tanga. Kadhalika Ligi Kuu Tanzania Bara, inatarajiwa kuendelea kesho Mei 3, 2016 kwa mchezo mmoja ambao Young Africans ya Dar es Salaam itakuwa mgeni wa Stand United kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga. Jumatano Mei 4, 2016 Azam FC ya Dar es Salaam itakuwa mwenyeji wa JKT Ruvu ya Pwani kwenye Uwanja wa Azam, Chamazi nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam. Michezo hiyo itaanza saa 10.000 jioni na kurushwa moja kwa moja na vituo vya televisheni ya Azam.

RONALDO AMSIFIA ZIDANE.

MSHAMBULIAJI mahiri wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo anadhani wachezaji wa timu hiyo wanathaminika zaidi toka Zinedine Zidane aitwae mikoba ya kuwaongoza na ana matumaini Mfaransa huyo atapewa mkataba mrefu zaidi. Madrid walianza kampeni zao kwa kusuasua chini Rafa Benitez ambaye alitimuliwa mapema Januari kufuatia matokeo mabaya na maswali juu ya uhusiano wake na kikosi. Toka Zidane ametwaa mikoba hiyo, Madrid wamekwea mpaka kutofautiana alama moja na vinara Atletico Madrid na Barcelona katika La Liga na wanaweza kupata tiketi ya kucheza ya kucheza fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kama wakifanikiwa kuifunga Manchester City Jumatano hii. Ronaldo ambaye ni mmoja ya wachezaji waliotajwa kutokuwa na furaha chini Benitez amesema kwasasa anafurahia maisha chini ya Zidane. Akihojiwa Ronaldo amesema anadhani wanajisikia kuthaminika zaidi chini ya Zidane, wanafahamu kuwa anahitaji muda zaidi lakini kwa kipindi kifupi mambo yamekuwa mazuri hivyo anampongeza.

GUARDIOLA KATIKA KIBARUA KIZITO KESHO.

MENEJA wa Bayern Munich, Pep Guardiola anajua kuwa anatakiwa kuwaziba midomo wakosoaji wake kwa kubadili matokeo na kuhakikisha anapata ushindi katika mchezo wa marudiano ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Atletico Madrid kesho. Katika mchezo wa mkondo wa kwanza uliofanyika kule Vicente Calderon, Bayern walichapwa bao 1-0 ambalo lilifungwa kwa jitihada binafsi za nyota wa Atletico Saul Niguez. Akiwa amewahi kushinda mataji 14 katika kipindi cha miaka minne aliyokuwa Barcelona na sita mpaka sasa katika muda wa miaka aliokaa Bayern, Guardiola ana matumaini ya kuondoka Ujerumani kwa kutwaa taji hilo katika fainali itakayofanyika Mei 28 jijini Milan. Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita Bayern wamekuwa wakikwama katika hatua ya nusu fainali kwenye michuano hiyo kwa kutolewa na timu za Hispania, mara ya kwanza wakitolewa na Real Madrid na msimu uliopita Barcelona. Kutolewa tena katika hatua hiyo na timu ya Hispania hakutachukuliwa vyema haswa kutokana na uamuzi wa Guardiola alioufanya katika mchezo wa mkondo wa kwanza kumuweka benchi Thomas Muller ambaye ndio mfungaji wa timu hiyo aliyefunga mabao mengi kwa timu hiyo kwenye michuano hiyo. Hata hivyo Bayern wataingia katika mchezo huo wakiwa na rekodi nzuri ya kushinda mechi zao zote tano za michuano hiyo wlaizocheza nyumbani lakini walihitaji muda wa nyongeza kutoka nyuma wakiwa wamefungwa mabao 2-0 na kuichapa Juventus kwa mabao 4-2 katika hatua ya 16 bora.

WENGER: NILITEGEMEA MAANDAMANO MAKUBWA ZAIDI.

MENEJA wa Arseal, Arsene Wenger alikuwa akitegemea kuwepo maandamano makubwa zaidi wakati wa mchezo walioshinda bao 1-0 dhidi ya Norwich City Jumamos iliyopita. Wenger anatarajiwa kutimiza mwaka wa 20 akiiongoza Arsenal itakapofika Octoba mwaka huu, lakini mara ya mwisho kutwaa taji la Ligi Kuu ilikuwa mwaka 2004 na baadhi ya mashabiki walishikilia mabango yaliyokuwa na ujumbe wa kutaka mabadiliko katika Uwanja wa Emirates. Akihojiwa Wenger amesema alitegemea uwanja mzima kuwa rangi nyeupe za mabango ya waandamanaji katika mchezo huo. Meneja huyo aliongeza kuwa lengo lilikuwa ni kuwapa furaha mashabiki hao kwa asilimia 100 lakini kwa bahati mbaya ameshindwa kutimiza hilo. Ushindi huo umefanya Arsenal kukwea katika nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu ambapo sasa wanahitaji alama mbili pekee ili wakihakikishie nafasi ya kucheza michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao. Jumapili hii Arsenal watakuwa na kibarua kizito pale watakaposafiri kuifuata Manchester City katika mchezo wa ligi utakaofanyika Uwanja wa Etihad.

VARDY AKWAA TUZO YA WAANDISHI.

MSHAMBULIAJI wa Leicester City, Jamie Vardy ametangazwa kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka kwa msimu wa 2015-2016 ambayo inatolewa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo-FWA. Nyota huyo wa kimataifa wa Uingereza amepokea zawadi hiyo baada ya mchezaji mwenzake Riyad Mahrez naye kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka ambayo inatolewa na Chama cha Wachezaji wa Kulipwa-PFA wiki iliyopita. Vardy ambaye amefunga mabao 22 msimu huu yalioisaidia Leicester kukaribia kutwaa taji lao la kwanza la ligi, alichukua tuzo hiyo akiwashinda wachezaji wenzake N’Golo Kante na Mahrez. Kulikuwa na jumla ya wachezaji 12 wa Leicester walioteuliwa katika orodha hiyo akiwemo Danny Drinkwater, Danny Simpson, Wes Morgan na Kasper Schmeichel. Mara baada ya kupokea tuzo hiyo Vardy aliwashukuru wachezaji wenzake kwa ushirikiano mkubwa waliokuwa nao kuanzia mwanzo wa msimu huu mpaka sasa hivi.

MADRID WANAVYOMNYIMA RAHA PELLEGRINI.

MENEJA wa Manchester City, Manuel Pellegrini amesema angeweza kufanya tena hivyo baada ya kutumia kikosi dhaifu katika mchezo wao dhidi ya Southampton, huku akijipanga kwa ajili ya mchezo wao dhidi ya Real Madrid Jumatano hii. Pellegrini alifanya mabadiliko nane katika kikosi chake alichokitumia katika mchezo wa nusu fainali ya mkondo wa kwanza ya Ligi ya Mabingwa Ulaya Jumanne iliyopita waliopata sare ya bila kufungana na Madrid. Mabadiliko hayo yalimtokea puani Pellegrini kwani alijikuta walitandikwa mabao 4-2 na Southampton katika Uwanja wa St Mary. Akihojiwa pellegrini amesema kama wangeweza kucheza Jumamosi angeweza kutaka kikosi chake kamili lakini alifanya hivyo jana kwasababu kuna mchezo wa Jumatano ambao aliupa kipaumbele. Pellegrini aliwapumzisha baadhi ya nyota wake akiwemo Sergio Aguero, Kevin de Bruyne na Vincent Kompany lakini alimuanzisha chipukizi wa miaka 19 Kelechi Iheanacho katika mchezo huo na kufunga mabao mawili.

XAVI AMKINGIA KIFUA MESSI.

KIUNGO wa zamani wa Barcelona, Xavi amemkingia kifua Lionel Messi akidai kuwa sio aina ya mchezaji anayedanganya pindi awapo uwanjani. Messi alituhumiwa kudanganya baada ya Filipe Luis kutolewa katika ushindi wa Barcelona dhidi ya Atletico Madrid Januari mwaka huu, huku Mbrazil huyo akidai baadae kuwa Messi anapewa kipaumbele maalumu na waamuzi. Hata hivyo, Xavi amemtetea Messi na ana uhakika kuwa Messi ana tabia za kipekee pindi anapokuwa uwanjani kulingana na wachezaji wengine. Xavi amesema Messi ni mzuri kwani siku zote amekuwa mkweli na hana tabia za kudanganya ili aweze kupata faulo pindi anapokuwa uwanjani.