Monday, January 21, 2013

GALATASARAY YAMNASA SNEIJDER, MILAN YAMNYATIA KAKA.

KLABU ya Galatasaray imedai kuwa imemnasa kiungo mshambuliaji wa kimataifa wa Uholanzi, Wesley Sneijder kwa ada euro milioni 7.5 kutoka klabu ya Inter Milan ya Italia. Galatasaray yenye maskani yake nchini Uturuki imesema kuwa imesainisha nyota huuyo mkataba wenye thamani ya euro milioni kwa mwaka mpaka mwaka 2016 baada ya kushindwa kuafikiana suala la malipo na Inter. Sneijder alijiunga na Inter akitokea Madrid mwaka 2009 na kuisaidia klabu hiyo kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, Serie A na Kombe la Italia mwaka 2010. Wakati pazia la usajili wa dirisha dogo likielekea kufungwa Januari 31, klabu ya AC Milan ya Italia imepanga kumrejesha kiungo wake wa zamani wa kimataifa wa Brazil Kaka kutokea Madrid. Kaka mwenye umri wa miaka 30 aliondoka Milan mwaka 2009 baada ya misimu sita katika klabu hiyo na kushinda mataji ya Serie A, Ligi ya Mabingwa Ulaya na Klabu Bingwa ya Dunia.

FALACAO NJE WIKI TATU.

MATARAJIO madogo ya kuwafikia vinara wa Ligi Kuu nchini Hispania Barcelona, waliyokuwanayo Atletico Madrid yaliingia katika kikwazo Jumapili baada ya mshambuliaji wake tegemeo Radamel Falcao kupata majeruhi ya mguu ambayo yatamuweka nje ya uwanja kwa kipindi cha wiki tatu akijiuguza. Falcao alianza kuchechea wakati akikokota mpira na mara moja aliomba kutolewa katika dakika ya 57 wakati Atletico ilipopata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Levante na kupunguza pengo la alama na Barcelona ambao walifungwa mchezo wao wa Jumamosi dhidi ya Real Sociedad. Meneja wa Atletico Diego Simeone alithibitisha kuumia kwa mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Colombia na kudai kuwa anaweza kukaa kwa siku 20 au zaidi. Falcao ameifungia Atletico mabao 18 msimu huu na kuisaidia timu hiyo kukaa katika nafasi ya pili wakiwa alama nyuma ya Barcelona.

RAIS AWATEMBELEA CHIPOLOPOLO.

RAIS wa Zambia Michael Sata amewataka wachezaji wa timu ya taifa ya Zambia maarufu kama Chipolopolo kuwachaza wapinzani wao watakaokutana wakati watapoanza kampeni ya kutetea taji lao la michuano ya Mataifa ya Afrika baadaye leo. Rais huyo amewaambia wachezaji hao kuwa inabidi waweke katika mawazo yao watu wote wa Zambia wa nyuma yao hivyo watapoanza kampeni zao inabidi wapambane kama wapigania uhuru ili waweze`kuhakikisha wanarudi na kombe lao nyumbani. Rais Sata aliongozana na mkewe Dr Christine Kaseba, Waziri wa Michezo Chishimba Kambwili na maofisa wengine wa ngazi za juu wan chi hiyo wakati walipoitembelea Chipolopolo katika kambi yao nchini Afrika Kusini. Sata alikaribishwa na rais wa Shirikisho la Soka la Zambia Kalusha Bwalya, wajumbe wa kamati ya utendaji wa shirikisho hilo pamoja na viongozi wa jimbo la Mpumalanga ambao ndio wenyeji wao huko. Zambia inatarajia kuanza kampeni zake kwa kukwaana na Ethiopia katika Uwanja wa Mbombela jioni hii.

ATLETICO MADRID NA REALA MADRID ZAPUNGUZA PENGO NA BARCELONA.

KLABU za Atletico Madrid na majirani zao Real Madrid waliitumia vizuri nafasi ya kufungwa kwa Barcelona na Real Sociedad kupunguza pengo la alama wanazotofautiana katika La Liga kwa kushinda michezo yao ya jana. Madrid ambao walikuwa wakicheza kwa kiwango chao bora kabisa msimu huu walifanikiwa kuifunga Valencia kwa mabao 5-0 na kufanikiwa kupunguza pengo la alama kutoka alama 18 mpaka 15 walizotofautiana na vinara wa La Liga Barcelona. Barcelona walifungwa na Sociedad kwa mabao 3-2 katika mchezo uliochezwa Jumamosi na kutengua rekodi yao ya kutofungwa mchezo katika La Liga. Atletico nao walitumia vizuri rekodi yao ya kutofungwa nyumbani kwa kuifunga Lavante kwa mabao 2-0 mabao ambayo yalifungwa na Radamel Falcao na Adrian. Kocha wa Atletico Diego Simeone amesema amefurahishwa na matokeo hayo lakini amewataka wachezaji wake kutobweteka na kujipanga kwa ajili ya mchezo ujao wa robo fainali ya pili ya Kombe la Mfalme Alhamisi dhidi ya Real Betis ambapo timu hiyo itahitaji kulinda ushindi wake wa mabao 2-0 iliyopata katika mchezo wa kwanza.

Sunday, January 20, 2013

AFCON 2013: UHABA WA MABAO WATAWALA MECHI ZA UFUNGUZI.

HALI ya baridi kali, mvua, soka lisilovutia na uhaba wa mabao ndio mambo yaliyoonekana kuchukua nafasi katika ufunguzi wa michuano ya Mataifa ya Afrika-Afcon inayofanyika nchini Afrika Kusini jana. Michuano ya 29 inayoandaliwa na Shirikisho la Soka barani Afrika-CAF kuanzia mwaka 1957 ilishuhudia michezo miwili kuisha ya kundi A kumalizika huku hakuna timu iliyoona lango la mwenzake. Wenyeji wa michuano hiyo Afrika Kusini maarufu kama Bafana Bafana walishindwa kuwapa raha mashabiki wao wapatao 85,000 waliojitokeza katika Uwanja wa Soccer City jijini Johannesburg pale alipong’ang’aniwa na timu ngeni katika mashindano hayo ya Cape Verde. Baada ya mchezo ulifuatiwa na mchezo mwingine katika huohuo kati ya Morocco na Angola lakini mpaka dakika tisini zinamalizika hakuna timu iliyoona lango la mwenzake. Michuano hiyo inaendelea tena baadae leo kwa michezo miwili ya kundi B ambapo katika mchezo wa kwanza Ghana itacheza na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo-DRC ukifuatiwa na mchezo kati ya Mali na Niger katika Uwanja wa Nelson Mandela Bay jijini Port Elizabeth.

PETERHANSEL, DESPRES WATAMBA MBIO ZA DAKAR RALLY.

DEREVA nyota wa mashindano ya Dakar Rally, Stephane Peterhansel amefanikiwa kushinda taji la tano la mashindano hayo na kuweka rekodi kuwa dereva wa kwanza kufanya hivyo, wakati Mfaransa mwenzake Cyril Despres naye alishinda taji la tano kwa upande wa mbio za pikipiki. Peterhensel ambaye ameshinda mbio za magari za Dakar mwaka 2004, 2005, 2007, 2012 na mwaka huu, na pia kuwa bingwa katika mbio za pikipiki mara sita na kuvunja rekodi ya Ari Vatanen aliyewahi kushinda mbio hizo mara nne. 
Akihojiwa mara baada ya ushindi huo Peterhensel alidai kuwa hiyo ni siku muhimu kwake kwa kuweka rekodi hiyo na kushukuru kwakuwa ni mara ya kwanza anamaliza mbio za zilizochukua siku 15 bila kupata matatizo yoyote katika gari lake. Wapinzani wakubwa wa Peterhensel kwenye mbio hizo Carlos Sainz na Nasser al-Attiyah walijitoa mapema baada ya magari kupata matatizo ya kiufundi.

LIVERPOOL INAHITAJI KUONGEZA WACHEZAJI WAWILI AU WATATU ILI IWE MOTO - GERRARD.

KIUNGO nyota wa klabu ya Liverpool Steven Gerrard anaamini kuwa timu hiyo inaweza kucheza na timu yoyote chini ya meneja mpya Brandan Rogders lakini inahitaji kuongeza wachezaji wawili au watatu ili kusaidia kuongeza nguvu. Liverpool jana wakicheza kwa kiwango bora iliifunga Norwich mabao 5-0 katika Uwanja wa Anfield huku Daniel Sturridge aliyesajiliwa kwa paundi milioni 12 kutoka Chelsea akifunga bao lake la tatu katika michezo mitatu toka atue hapo. Lakini pamoja na ushindi huo mnono Gerrard anaamini kuwa bado wanahitaji wachezaji wawili au watatu wakubwa ili waweze kufukuzia mataji. Liverpool inakabiliwa na mchezo mgumu wa ligi dhidi ya Arsenal katika Uwanja wa Emirates mwishoni mwa wiki ijayo baada ya kucheza mchezo wao wa mzunguko wa nne wa Kombe la FA huko Oldham.