Monday, July 22, 2013

MESSI AMPIGIA CHAPUO MARTINO KUCHUKUA MIKOBA YA VILANOVA BARCELONA.

MSHAMBULIAJI nyota wa klabu ya Barcelona, Lionel Messi amempigia chapuo kocha Gerardo Martino kuchukua nafasi ya kuinoa klabu hiyo. Nafasi imekuwa wazi kufuatia aliyekuwa kocha wa timu hiyo Tito Vilanova kulazimika kuachia ngazi kutokana na maradhi ya saratani yanayomsumbua. 
Martino ambaye aliiongoza timu ya Old Boys kushinda taji la Ligi Kuu chini Argentina msimu uliopita ni mmoja wa makocha wanaoewa nafasi ya kuchukua nafasi ya Vilanova na Messi ana imani kuwa kocha huyo anastahili nafasi hiyo. Messi alidai kuwa Martino ni mmoja wa makocha wenye kiwango cha juu na kila mtu anamheshimu hivyo haoni tatizo kama akikabidhiwa mikoba ya kuinoa Barcelona.

Sunday, July 21, 2013

WABUKINI KUCHEZESHA STAR, UGANDA.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limeteua waamuzi kutoka Madagascar kuchezesha mechi kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Uganda (The Cranes) itakayochezwa Jumamosi (Julai 27 mwaka huu) Uwanja wa Mandela ulioko Namboole nje kidogo ya Jiji la Kampala. Waamuzi wataongozwa na Kanoso Abdoul Ohabee wakati mwamuzi msaidizi namba moja ni Andirvoavonjy Pierre Jean Eric. Mwamuzi msaidizi namba mbili ni Jinoro Velomanana Ferdinand huku Andriamiharisoa Hubert Marie Bruno akiwa mwamuzi wa mezani (fourth official). Kamishna wa mechi hiyo ya marudiano ya raundi ya mwisho kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) ni Ismail Kamal kutoka Ethiopia. Mechi hiyo namba 38 itachezwa kuanzia saa 10 kamili jioni kwa saa za Afrika Mashariki. Taifa Stars ilipoteza mechi ya kwanza iliyochezwa Julai 13 mwaka huu jijini Dar es Salaam kwa bao 1-0. Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager iko kambini jijini Mwanza ikijiandaa kwa mechi hiyo itakayoamua ni timu ipi kati ya hizo mbili itacheza Fainali za CHAN mwakani nchini Afrika Kusini.

CHAPOMBE GAZZA ASHITAKIWA KWA ULEVI.

MCHEZAJI wa zamani nguli wa kimataifa wa Uingereza, Paul Gascoigne maarufu kama Gazza ameshitakiwa kosa la ulevi wa kupindukia na kusababisha usumbufu katika kituo cha treni. Gazza mwenye umri wa miaka 46 ambaye alitoka katika kituo cha tiba ya ushauri nasaha nchini Marekani mapema mwaka huu, alikamatwa kufuatia tuhuma hizo mapema mwaka huu huko Stevenage, Hertfordshire. Gazza pia ameshitakiwa na Polisi wa Usafirishaji nchini Uingereza kwa makosa mawili ya kushambulia. Mchezaji huyo wa zamani wa vilabu vya Newcastle United, Tottenham Hotspurs na Rangers anatarajiwa kusiamama mahakamani huko Stevenage Agosti 5 mwaka huu. 


JINAMIZI LA MAJERUHI LAANZA KUIANDAMA ARSENAL.

KLABU ya Arsenal imeendelea kuongeza majeruhi katika ukuta wake baada ya Laurent Koscilny kutolewa mazoezini kutokana na kuumia. Beki huyo wa kimataifa wa Ufaransa alitolewa dakika za mwisho za mazoezi ya klabu hiyo huku akichechemea kutokana na maumivu kifundo cha mguu wake wa kulia. Baada ya beki huyo kuumia mara alifanyiwa uchunguzi na timu madaktari wa klabu hiyo kabla ya kuhamishwa na kupelekwa ndani katika Uwanja wa Rugby wa Mizuho kwa uchuzi zaidi. Huyo anakuwa mchezaji wa pili kuumia katika kikosi cha Arsene Wenger toka watue nchini Japan kwa ziara yao ya maandalizi ya msimu mpya ambapo golikipa Wojciech Szczesny naye aliondolewa katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Nagoya utakaopigwa Jumatatu usiku baada ya naye kuumia mazoezini.

NAPOLI YAMSAJILI ALBIOL KUTOKA MADRID.

KLABU ya Napoli ya nchin Italia imetangaza kumsajili beki mahiri wa klabu ya Real Madrid ya Hispania Raul Albiol. Katika taarifa iliyotumwa katika mtandao wa klabu hiyo imeeleza kuwa beki huyo wa kati mwenye umri wa miaka 27 amesajiliwa kwa mkataba wa miaka minne ambapo taarifa hiyo haikufafanua thamani halisi waliyomnunulia mchezaji huyo. Napoli kwasasa iajipanga kuimarisha kikosi chake kwa ajili ya msimu mpya wa Ligi Kuu nchini Italia na Ligi ya Mabingwa Ulaya huku wakiwa na fedha za kutosha kutumia baada ya kumuuza mshambuliaji wa kimataifa wa Uruguay Edinson Cavani kwenda Paris Saint Germain kwa ada ya euro milioni 64. Albion ambaye ametoka katika shule ya soka ya Valencia akiwa kama mchezaji wa kiungo aliibuka katika kikosi cha kwanza cha klabu hiyo mwaka 2003 wakati huo ikifundishwa na kocha wa mpya wa Napoli Rafa Benitez kabla ya kuhamia Madrid mwaka 2009 ambako muda mwingi alitumika kama mchezaji wa akiba. Pamoja na kukosa namba klabuni kwake alifanikiwa kupata nafasi katika kikosi cha timu ya taifa ya Hispania katika michuano ya Kombe la Dunia 2010 na michuano ya Ulaya mwaka jana.

BINGWA WA ZAMANI WA OLIMPIKI ATAKA ADHABU YA WANARIADHA WADANGANYIFU KUONGEZWA MPAKA KUFIKIA MIAKA MINNE.

MWENYEKITI wa michuano ya olimpiki iliyofanyika jijini London mwaka jana, Sebastian Coe amedai kuwa adhabu ya kufungiwa wanariadha wanaogundulika kutumia dawa za kuongeza nguvu iongezwe kutoka miaka miwili hadi miaka minne. Kauli ya Coe ambaye amewahi kushinda medali mbili za dhahabu katika michuano olimpiki, imekuja baada ya wanariadha nyota wa mbio fupi Tyson Gay wa Marekani na Asafa Powell kugundulika kutumia dawa hizo katika vipimo walivyofanyiwa. Coe amesema hatua za haraka na makusudi za kuongeza adhabu hiyo kutoka miaka miwili mpaka miaka minne inabidi zichukuliwe ili kulinda heshima wa mchezo huo. Coe ambaye aliwahi kunyakuwa medali za dhahabu katika michuano ya riadha ya olimpiki mita 1,500 jijini Moscow mwaka 1980 na Los Angeles mwaka 1984 amedai kuwa bila kuchukua hatua kama hizo mchezo wa riadha utapoteza umaarufu wake kutoka na udanganyifu unafanyika.

SCHWARZER APANIA KUMNYANG'ANYA NAMBA CECH.

GOLIKIPA mkongwe aliyesajiliwa na klabu ya Chelsea katika kipindi cha usajili wa majira ya kiangazi, Mark Schwarzer ameibuka na kudai kuwa anapigania kupata namba katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo msimu ujao. Akihojiwa na waandishi wa habari katika ziara ya kujiandaa na msimu mpya ya klabu hiyo jijini Kuala Lumpur, Malaysia, Schwarzer amesema wakati akisajiliwa na timu hiyo alijua kwamba wana makipa bora na mpambano wa kutafuta nafasi ya kuanza utakuwa mgumu. Lakini alidai kuwa kwa juhudi na kiwango kizuri atakachoonyesha ana matumaini anaweza kupangwa katika kikosi cha kwanza timu hiyo msimu ujao. Meneja wa Chelsea Jose Mourinho amesema wiki iliyopita kuwa Schwarzer ataleta ushindani na hamasa kwa golikipa namba moja wa klabu hiyo Petr Cech baada ya kufanya usajili huo wa kushangaza. Schwarzer ambaye amecheza katika Ligi Kuu nchini Uingereza kwa zaidi ya miaka 15 ni mmoja ya wachezaji wachache waliocheza mechi zaidi ya 500 katika historia ya ligi hiyo.