Thursday, February 20, 2014

ROBBEN ALIZIDISHA CHUMVI - WENGER.

KOCHA wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger amemtuhumu Arjen Robben kwa kujirusha na kumponza kipa wa Wojciech Szczesny kutolewa nje kwa kadi nyekundu ambayo ilipelekea timu hiyo kulala kwa mabao 2-0 dhidi ya Bayern Munich jana. Mbali na kumlalamikia Robben, Wenger pia aliwalalamikia wachezaji wengine wa Bayern kwa kumtumia vibaya mwamuzi aliyechezesha mchezo huo Nicola Rizzoli. Wenger amesema hakuna shaka kwamba kipa wake alimgusa Robben lakini mchezaji huyo alizidisha chumvi kwa kujirusha zaidi hivyo kuharibu mchezo baada ya kadi nyekundu kutolea. Katika mchezo huo mabao ya Bayern yote yalipatikana katika kipindi cha pili kupitia kwa Toni Kroos na Thomas Muller baada ya timu zote kukosa penati katika kipindi cha kwanza ambapo Mesut Ozil alikosa penati kwa upande wa Arsenal huku David Alaba akikosa kwa upande wa Bayern. Kuna uwezekano kipa wa Arsenal akaadhibiwa zaidi na Shirikisho la Soka barani Ulaya, UEFA kwa kuonyesha ishara mbaya jukwaani wakati akitoka baada ya kupewa kadi nyekundu.

Wednesday, February 19, 2014

AL AHLY KUIVUTIA KASI YANGA.

WAPINZANI wa timu ya Yanga katika michuano ya Klabu Bingwa ya Afrika, Al Ahly ya Misri watakabiliwa na kibarua kigumu kesho wakati watakapokuwa wenyeji wa timu ya CS Sfaxien ya Tunisia katika mchezo wa kugombea taji la Super Cup utakaofanyika jijini Cairo. Al Ahly itabidi wasahau matokeo mabovu ambayo wamekuwa wakipata katika mechi za ligi ya nyumbani msimu huu kama wanataka kuweka rekodi ya kunyakuwa taji la Super Cup kwa mara ya sita. Mechi hiyo ambayo huwakutanisha mabingwa wa Ligi ya Mabingwa msimu uliopita ambao ni Al Ahly na mabingwa wa Kombe la Shirikisho ambao ni Sfaxien unatarajiwa kupigwa katika Uwanja wa Taifa wan chi hiyo uliopo jijini Cairo ambao una uwezo wa kubeba mashabiki 75,000. Kocha wa Al Ahly Mohamed Youssef amesema anaamini mechi hiyo ni muhimu kwao kwani itawasaidia wachezaji wake kuongeza kujiaminina kusahau matokeo mabovu yaliyowaandama katika wiki za karibuni. Yanga tayari imeshatuma shushu wake katika mchezo huo ambaye ni kocha msaidizi Charles Boniface Mkwasa kwa ajili ya kuwapeleleza wapinzani wao hao kabla ya mechi yao itakayochezwa Februari 28 mwaka huu jijini Dar es Salaam.

FLETCHER AITWA SCOTLAND.

KIUNGO mahiri wa klabu ya Manchester United, Darren Fletcher ameitwa katika kikosi cha timu ya Scotland kwa ajili ya mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Poland mwezi ujao. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 30 amerejea uwanjani hivi karibuni kufuatia kuugua na anategemewa kuwepo katika mchezo huo utakaochezwa jijini Warsaw Machi 5mwaka huu ikiwa ni mara ya kwanza kuvaa jezi za Scotland toka afanye hivyo mwaka 2012. Fletcher ambaye ameichezea Scotland mechi 61, alieleza nia yake ya kutaka kurejea katika majukumu ya kimataifa mara baada ya kupona. nYota huyo aligundulika kusumbuliwa na vidonda vya tumbo mwaka 2011 lakini amefanikiwa kurudi uwanjani baada ya kufanyiwa upasuaji kuondoa eneo lililoathirika.

NILITIMULIWA KWA BARU PEPE - LAUDRUP.

MENEJA wa zamani wa klabu ya Swansea City, Michael Laudrup amedai kuwa alitimuliwa kwa barua pepe saa chache baada ya kuambiwa kibarua chake kiko salama na kushikana mikono na mwenyekiti wa klabu hiyo Huw Jenkins. Laudrup mwenye umri wa miaka 49 aliiongoza klabu hiyo kunyakuwa Kombe la Ligi msimu uliopita likiwa ni taji la kwanza kubwa kwa timu hiyo katika hitoria yao ya miaka 102. Hata hivyo alitimuliwa mwezi huu baada ya matokeo mabovu ya timu hiyo na kutokuelewana kwa benchi lake la ufundi. Kocha huyo amesema jambo hilo la kutimuliwa kwa kupewa barua pepe lilimchanganya sana kwani lilitokea muda mchache baada ya kuhakikishiwa kibarua chake huku akipeana mkono na Jenkins. Laudrup ambaye pia amewahi kuinoa Real Mallorca ameendelea kudai kuwa alifanya mazungumzo na Jenkins na kumtaka kufukuza benchi lake la ufundi lakini alimkatalia hatua ambayo ilipelekea kutimuliwa siku moja baadae.

BAYERN HII SIO KALI KAMA BARCELONA YA PEP GUARDIOLA - WENGER.

MENEJA wa Arsenal, Arsene Wenger anaamini kuwa Bayern Munich bado haijafikia kiwango cha Barcelona iliyonyakuwa mataji mawili ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya chini ya kocha Pep Guardiola. Arsenal watakuwa wenyeji wa mabingwa hao wa Ulaya katika mchezo wa mkondo wa kwanza hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya leo usiku huku wakiwa na kumbukumbu ya kung’olewa katika hatua kama hiyo na Bayern msimu uliopita sambamba na Barcelona ya Guardiola mwaka 2010 na 2011. Ingawa Guardiola amekuwa kocha wa Bayern hivi sasa, Wenger bado anaamini Barcelona ya kipindi kile bado ilikuwa bora kuliko Bayern ambao msimu uliopita walishinda mataji matatu kwa mpigo. Wenger amesema alikuwa akivutiwa zaidi na Barcelona ya kipindi kile kutokana na kasi ya pasi na mchezo wao ni mategemeo yake hawatakutana na hilo watakapocheza na Bayern.

KWELI NILIKOSEA LAKINI SIKUFANYA NGONO - GIROUD.

MSHAMBULIAJI nyota wa klabu ya Arsenal, Olivier Giroud amejaribu kuweka wazi juu ya maisha yake binafsi kwa kusisitiza kuwa hakufanya uzinzi kama watu wanavyofikiria. Nyota huyo aliomba radhi baada ya picha yake iliyopigwa na mwanamitindo Celia Kay katika hoteli ya Four Seasons ambayo Arsenal walifikia kabla ya mchezo wao dhidi ya Crystal Palace uliochezwa Februari 2 kuonekana gazetini. Giroud aliandika tena katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter kuwa aliomba msamaha na kukiri kuwa alifanya kosa lakini hakufanya ngono na mwanamitindo huyo. Wenger alithibitisha kumchukulia hatua mchezaji huyo kwa tukio hilo lakini alikataa kuweka wazi adhabu atakayopewa kwa kudai kuwa ana heshimu mambo binafsi ya mchezaji huyo. Kulikuwa na tetesi kuwa Arsenal walikuwa wamepanga kumpa adhabu ya faini ya paundi 230,000 kwa tukio hilo lakini walisitisha baada ya mchezaji huyo kukana huku wakili wake akituma barua kuelezea kuwa mteja wake hakufanya chochote kibaya.

MIMI NI MGONJWA NA SIO CHAPOMBE - WILKINS.

KOCHA msaidizi Ray Wilkins aliyetimuliwa kibarua chake na Fulham mapema wiki hii amebainisha kuwa anasumbuliwa na ugonjwa kama uliokuwa ukimsumbua kiungo wa Manchester United Darren Fletcher. Wilkins mwenye umri wa miaka 57 ambaye amewahi kucheza katika timu za United na Chelsea amekuwa akipambana na ugonjwa wa vidonda vya tumbo toka mwaka 1990. Wilkins amelazimika kuweka wazi hali yake ya kiafya ili kuokoa kibarua chake kama mwalimu wa soka na kuzima tuhuma kuwa ni mlevi. Akihojiwa kocha huyo amesema amesikia tuhuma kuwa alionekana amelewa wakati wa mchezo dhidi ya Liverpool ambao walichapwa mabao 3-2 na kupelekea benchi zima la ufundi la timu hiyo likiongozwa na kocha mkuu Rene Meulensteen kutimuliwa. Wilkins alikana tuhuma hizo na kubainisha kuwa hali yake ya kiafya muda mwingine humfanya aonekane katika hali hiyo.