Wednesday, September 23, 2015

LEWANDOWSKI AUSHANGAZA ULIMWENGU KWA KUPIGA MABAO MATANO NDANI YA DAKIKA TISA.

MSHAMBULIAJI wa Bayern Munich, Robert Lewandowski jana ameweka rekodi ya kipekee Bundesliga kwa kufunga mabao matano ndani ya dakika tisa katika mchezo dhidi ya Vfl Wolfsburg. Katika mchezo huo Bayern walikuwa nyuma kwa bao 1-0 mpaka muda wa mapumziko, wakati Lewandowski alipoingia kuchukua nafasi ya Thiago. Dakika sita baadae, mchezaji huyo wa kimataifa wa Poland alifunga bao lake la kwanza katika dakika ya 51 kabla ya kuongeza mengine manne dakika za 52, 55, 57 na 60. Ushindi huo umeifanya Bayern kukwea kileleni mwa msimamo wa Bundesliga wakitofautiana kwa alama tatu na mahasimu wao Borussia Dortmund ambao leo wanaivaa Hoffenheim.

WAKALA WA POGBA AMJIBU FERGUSON.

WAKALA wa kiungo Paul Pogba, Mino Raiola amejibu vijembe kutoka kwa Sir Alex Ferguson akisisitiza kuwa meneja huyo wa zamani wa Manchester United hajui asemalo. Meneja huyo nguli ambaye alistaafu mwaka 2013 baada ya kuingoza United kwa mafanikio, alimlaumu wakala huyo kuwa ndio chanzo cha kuondoka kwa Pogba kwenda Juventus miaka mitatu iliyopita katika kitabu chake kipya. Raiola amejibu madai hayo akidai Ferguson hawezi kuelewa kuwa uamuzi alioufanya ni kwa faida ya nyota huyo wa kimataifa wa Ufaransa ambaye aliondoka United akiwa mchezaji huru mwaka 2012 lakini sasa thamani yake imepanda mpaka kufikia euro milioni 100. Wakala huyo aliendelea kudai kuwa maneno ya Ferguson hayaharibu kazi yake kwani yeye anayachukulia kama mfano wa jinsi gani anavyofanya kibarua chake vyema. Raiola amesema kazi kuwa ya wakala ni kufanya kilicho bora kwa maslahi ya wachezaji wake na kama angekuwa anafanya kwa maslahi yake Pogba angekuwa United mpaka leo.

BARCELONA KUMKOSA ALBA.

KLABU ya Barcelona imethibitisha kuwa itamkosa beki wake Jordi Alba katika mchezo wao wa leo dhidi ya Celta Vigo. Baada ya kucheza kila dakika katika mechi tatu za La Liga za mwanzo za Barcelona, beki huyo hakuwemo katika mchezo wa Jumapili iliyopita ambao timu hiyo ilishinda mabao 4-1 dhidi ya Levante. Na sasa klabu hiyo imebainisha kuwa nyota huyo wa kimataifa wa Hispania anasumbuliwa na maumivu ya shingo hivyo ataukosa pia mchezo dhidi ya Celta Vigo. Alba mwenye umri wa miaka 26, nafasi yake itachukuliwa na beki wa kulia wa Brazil Douglas ambaye alikuwa bado hajaitumikia klabu hiyo msimu huu kutokana na majeruhi.

DAKTARI WA CHELSEA EVA CARNEIRO AAMUA KUIKACHA KLABU HIYO.

DAKTARI wa Chelsea Eva Carneiro ameamua kuondoka rasmi katika klbu hiyo, wiki sita baada ya kukosolewa na meneja Jose Mourinho. Carneiro aliingia katika mzozo na Mourinho kufuatia tukio lake la kwenda kumhudumia Eden Hazard katika mchezo ambao ulimalizika kwa sare ya mabao 2-2 dhidi ya Swansea City Agosti 8 mwaka huu. Chelsea ilimtaka Carneiro mwenye umri wa miaka 42 kurejea kazini lakini mwanamama huyo mwenye ameamua kuacha kibarua huku akifikiria kuchukua hatua za kisheria. Chama cha Soka cha Uingereza kinapitia malalamiko kuwa Mourinho alitumia lugha za kudhalilisha na kijinsia kwa mwanamama huyo. Chelsea wamekataa kutoa kauli yeyote kuhusiana na suala hilo.

FA YAMPA DOZI COSTA, YAMUACHA HURU GABRIEL.

CHAMA cha Soka cha Uingereza-FA kimemlima adhabu ya kutocheza mechi tatu mshambuliaji wa Chelsea Diego Costa. Costa amelimwa adhabu hiyo kufuatia tukio lake la kumfanyia vurugu beki Laurent Koscielny katika ushindi wa mabao 2-0 waliopata dhidi ya Arsenal Jumamosi iliyopita, ingawa hata hivyo alikanusha makosa hayo. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 26 alionekana katika picha za video akimuwekea mikono Koscielny usoni kwake kwa makusudi kabla ya kuzozana na Gabriel aliyepewa kadi nyekundu katika mchezo huo. Hata hivyo, FA imeifuta kadi nyekundu ya Gabriel wakidai ilitolewa kimakosa huku wakimtetea mwamuzi kwa kutoona tukio alilofanya Costa dhidi ya Koscielny. Costa sasa anatarajiwa kuukoa mchezo wa Kombe la Ligi dhidi ya Walsall baadae leo sambamba na mechi za Ligi Kuu dhidi ya Newcastle United na Southampton.

Tuesday, September 22, 2015

FERGUSON AKIRI KUDAI KUONGEZWA MSHAHARA BAADA YA ROONEY KUONGEZWA.

MENEJA wa zamani wa Manchester United, Sir Alex Ferguson alitaka mshahara wake uongezwe mara mbili yake kufuatia nyongeza aliyopewa Wayne Rooney mwaka 2010.Rooney alikuwa akitaka kuondoka United kabla ya kusaini mkataba mpya ambao ulimfanya kukunja kitita cha paundi 250,000 kwa wiki.Katika kitabu chake kipya, Ferguson amesema aliuambia uongozi kuwa sio haki Rooney kulipwa fedha nyingi zaidi yake kwani katika makubaliano walishaelewana hakuna mchezaji anayepaswa kulipwa zaidi yake.Ferguson media kuwa hatua hiyo ilipelekea mshahara wake kuongezwa mara mbili ili kufikia lengo walilojiwekea.Koch huyo alistaafu soka mwaka 2013 baada ya kuinoa United kwa miaka 26 na kufanikiwa kushinda mataji 13 ya Ligi Kuu, matano ya Kombe la FA, manne ya Kombe la Ligi na mawili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

MAREKANI YAZIDI KUMNG’ANG’ANIA WARNER.

MWANASHERIA Mkuu wa Serikali ya Trinidad na Tobago ametoa kibali juu ya kesi iliyofunguliwa na Marekani dhidi ya aliyekuwa Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA Jack Warner.Warner anatuhumiwa kuhusika kupokea mamilioni ya dola za kimarekani kama rushwa alipokuwa madarakani.Warner pamoja na maofisa wengine kumi na watatu wa sasa na wa zamani wa FIFA walifunguliwa mashitaka hayo na mamlaka ya Marekani tokea mwezi Mei mwaka huu.Warner amekanusha mashitaka yanayomkabili na wiki iliyopita serikali ya Switzerland ilithibitisha kuachiliwa kwa kiongozi mwingine wa FIFA Eugenio Figueredo kutoka Uruguay.