Friday, October 16, 2015

MESSI NI BORA ZAIDI YA MARADONA - MENOTTI.

MCHEZAJI nyota wa zamani wa kimataifa wa Argentina na klabu ya Barcelona, Cesar Luis Menotti amesisitiza Lionel Messi ni bora zaidi katika kikosi cha timu ya taifa kuliko ilivyokuwa kwa Diego Maradona. Maradona amewahi kushinda Kombe la Dunia akiwa na Argentina mwaka 1986, jambo ambalo Messi hajalifikia katika soka lake la kimataifa baada ya mwaka jana Argentina kufungwa katika hata ya fainali ya michuano hiyo. Hata hivyo, Menotti hana shaka kuwa Messi mshindi mara nne wa tuzo ya Ballon d’Or ameonyesha ubora wa hali ya juu kwa Argentna kuliko Maradona, akisisitiza kikosi kizima kilishindwa kumsaidia nyota huyo kucheza katika ubora wake. Menotti ambaye naye amewahi kuingoza Argentina kunyakuwa Kombe la Dunia mwaka 1978, amesema katika mita 20 za mwisho wako sawa lakini wako tofauti kutokana na jinsi walivyoendelezwa. Menotti aliendelea kudai kuwa jambo kubwa alilokuwa akifanya Maradona ni kufunga mabao lakini Messi yeye anatoa zaidi ya kufunga mabao kwani anawasaidia na wenzake.

MARTIAL, POCHETTINO WALAMBA TUZO ZA MWEZI UINGEREZA.

MSHAMBULIAJI wa Manchester United, Antony Martial na meneja wa Tottenham Hotspurs Mauricio Pochettino wametunukiwa tuzo ya mchezaji na kocha bora wa mwezi Septemba nchini Uingereza. Martial alijiunga na United kwa kitita cha paundi milioni 36 katika siku za mwisho kabla ya kufungwa dirisha la usajili majira ya kiangazi na nyota huyo mwenye umri wa miaka 19 amefunga mabao matatu katika mechi za ligi msimu uliopita. Kwa upande wa Spurs wao wameshinda mechi zao tatu za Ligi Kuu walizocheza mwezi uliopita ukiwemo ushindi mnono wa mabao 4-1 dhidi ya vinara Manchester City. Hiyo inakuwa tuzo ya kwanza kwa meneja huyo raia wa Argentina toka atue Spurs ingawa pia amewahi kunyakuwa tuzo hiyo akiwa na Southampton Januari mwaka 2013.

HAYATOU AANZA RASMI KUKAIMU NAFASI YA BLATTER.

RAIS wa muda wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA, Issa Hayatou amesema ni jambo muhimu kwa shirikisho hilo kurejea imani kwa jumuiya. Hayatou aliwasili makao makuu ya FIFA yaliyopo jijini Zurich, Uswisi jana ikiwa ni mara ya kwanza toka alipochaguliwa kuwa kiongozi wa muda baada rais Sepp Blatter kusimamishwa. FIFA ilimsimamisha kwa siku 90 Blatter sambamba na makamu wa rais wake Michel Platini na katibu mkuu Jerome Valcke ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za rushwa zinazowakabili. Akizungumza na wanahabari Hayatou amesema anafahamu kuwa hali sio nzuri lakini wamejipanga vyema kuhakikisha hatua za msingi ili kulijenga upya shirikisho zinafanyika. Hayatou aliendelea kudai kuwa kwasasa shirikisho hilo limejikita zaidi katika uchunguzi mkuu wa rais na kutoa ushirikiano katika uchunguzi unaoendelea.

Thursday, October 15, 2015

MASHABIKI BAYERN KUANDAMANA KUPINGA BEI KUBWA YA TIKETI EMIRATES.

KUNDI la mashabiki wa Bayern Munich wamepanga kuandamana wakati wa mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Arsenal kutokana na gharama kubwa za tikeni kwa timu pinzani kwenye Uwanja wa Emirates. Mashabiki hao wamesema hawataingia uwanjani katika dakika tano za mwanzo katika mchezo wao wa wiki ijayo kutokana na kuuziwa tiketi kwa bei ya juu ya paundi 64. Hatua inakuja kufuatia BBC kutoa ripoti ya Gharama za Soka ambayo ilikuwa ikizichambua klabu 227 Uingereza na Ulaya. Akijibu hoja hiyo, meneja wa Arsenal Arsene Wenger amesema kazi yeye ni kutengeneza thamani.


PISTORIUS KUACHIWA JUMANNE IJAYO.

BODI ya misamaha nchini Afrika Kusini imedai kuwa mwanariadha nyota mlemavu wa nchi hiyo, Oscar Pistorius ataachiwa kutoka gerezani na kwenda kutumikia kifungo cha nje Jumanne ijayo. Pistorius alifungwa miaka mitano jela mwaka jana baada ya kukutwa na hatia ya kuua bila kukusudia. Mwanariadha huyo alimfyatulia risasi na kumuua mpenzi wake Reeva Steenkamp kupitia mlango wa bafuni akidhania kuwa ni mwizi aliyevamia nyumbani kwake. Waendesha mashitaka wamekata rufani, wakidai kuwa Pistorius alipaswa kuhukumiwa kwa kosa la mauaji na kesi hiyo imepangwa kusikilizwa Novemba 3 mwaka huu.

MAN CITY YATANGAZA FAIDA KWA MARA YA KWANZA TOKA INUNULIWE NA SHEIKH MANSOUR.

KLABU ya Manchester City ambao walifungiwa mwaka jana na Shirikisho la Soka la Ulaya-UEFA kwa kukiuka sheri ya matumizi, wametoa faida ya mwaka kwa mara ya kwanza toka timu hiyo iliponunuliwa na Sheikh Mansour bin Zayed mwaka 2008. Klabu hiyo ya Ligi Kuu ilitoa taarifa yake ya mwaka kwa msimu wa 2014-2015 jana. Taarifa hiyo iliyotolewa imeonyesha kuwa klabu hiyo imepata faida ya paundi milioni 10.7 huku mapato yake kwa mwaka yakipanda na kufikia rekodi ya paundi milioni 352. Taarifa hiyo iliyotolewa na mwenyekiti wake Khaldoom Al Mubarak iliendelea kudai kuwa sasa City imeanza kuingiza faida huku wakiwa hawana deni lolote. Mwaka jana klabu hiyo ilitozwa faini ya paundi milioni 60 kwa kukiuka sheria hiyo ya UEFA huku pia kikosi chao kikipunguzwa kwa ajili ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

BARCELONA KUMKATIA RUFANI CAS ARDA TURAN.

KLABU ya Barcelona imedai kujiandaa kupeleka malalamiko yao ya kutaka kumsajili kiungo wa kimataifa wa Uturuki, Arda Turan katika Mahakama ya Michezo ya Kimataifa-CAS. Mabingwa hao wa Hispania na Ulaya wameshindwa kumtumia kiungo huyo mwenye umri wa miaka 28 kutokana na kutumikia adhabu yao ya kufungiwa na Shirikisho la Soka Duniani-FIFA kwa kuvunja sheria za usajili. Lakini baada ya kuumia kwa Rafinha, Barcelona wameomba FIFA na Shirikisho la Soka la nchi hiyo kama wanaweza kubadilisha ili Arda aweze kuchukua nafasi ya Rafinha. Kama wakikataliwa kufanya hivyo Barcelona watakata rufani CAS. Barcelona walifungiwa kutosajili mchezaji yeyote kwa vipndi viwili vya usajili na adhabu yao ilimalizika rasmi pindi lilipofungwa dirisha la usajili la majira ya kiangazi Septemba mwaka huu.