Monday, May 16, 2016

WALCOTT AJIBU KUFUATIA KUACHWA KWAKE KATIKA KIKOSI CHA UINGEREZA.

WINGA wa Arsenal, Theo Walcott amejibu kuachwa kwake katika kikosi cha timu ya taifa ya Uingereza kwa ajili ya michuano ya Euro 2016, akisisitiza kuwa wakati akisononeshwa na hilo lakini amekubali uamuzi wa meneja Roy Hodgson. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 27 amekuwa akihangaika kupata nafasi katika kikosi cha kwanza mwishoni mwa kampeni za msimu wa 2015-2016 akiwa hajapata nafasi ya kuanza katika mechi yeyote ya Ligi Kuu toka Februari 28. Mara ya mwisho kuifungia Arsenal bao ilikuwa ni Aprili wakati waliposhinda mabao 4-0 na kufuatia kuachwa huko na Hodgson, Walcott amekubaliana na uamuzi huo na kuitakia timu kila la heri katika michuano hiyo itakayofanyika Ufaransa. Walcott alituma ujumbe katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter akidai kusikitishwa kwake kuachwa kwenye kikosi hicho lakini akikubaliana na uamuzi wa Hodgson.

KOCHA MPYA WA CHELSEA AONDOLEWA SHITAKA LA KUPANGA MATOKEO.

KOCHA wa timu ya taifa ya Italia, Antonio Conte ambaye anatarajiwa kuchukua mikoba ya kuinoa Chelsea kipindi hiki cha kiangazi, amefutiwa mashitaka ya upangaji matokeo yaliyokuwa yakimkabili. Conte alikuwa mmoja wa washitakiwa kadhaa katika kesi hiyo iliyokuwa ikisikilizwa huko Cremona ikihusisha wakati akiifundisha klabu ya Siena ambayo wakati huo ilikuwa ikicheza Serie B. Meneja huyo mwenye umri wa miaka 46 alikuwa akituhumiwa kwa kushindwa kutoa taarifa ya jinsi anavyofahamu suala la kupanga matokeo kwa wachezaji katika kipigo cha bao 1-0 walichopata kutoka kwa Albinoleffe Mei mwaka 2011. Mwendesha mashitaka Roberto Di Martino alikuwa amependekeza adhabu ya kifungo cha miezi sita jela na faini ya euro 8,000 kwa meneja huyo wa zamani wa Juventus lakini aliachiwa huru mapema leo. Conte anatarajiwa kuchukua nafasi ya meneja wa muda wa Chelsea Guus Hiddink baada ya kumalizika michuano ya Euro 2016.

ARTETA AAMUA KUTUNDIKA DARUGA ZAKE NA KUGEUKIA UKOCHA.

KIUNGO wa Arsenal, Mikel Arteta amethibitisha nia yake ya kustaafu soka siku moja baada ya kucheza mechi yake ya mwisho na klabu hiyo. Arteta mwenye umri wa miaka 34 alitokea benchi katika mchezo wa Arsenal walioshinda mabao 4-0 dhidi ya Aston Villa na kuwafanya kujihakikishia nafasi ya pili juu ya mahasimu wao Tottenham Hotspurs katika msimamo wa Ligi Kuu. Mkataba wa kiungo huyo wa kimataifa wa Hispania unatarajiwa kumalizika kiangazi hiki na anatarajiwa kustaafu soka ili aweze kujifunza masuala ya ukocha. Akihojiwa Arteta amesema ni jambo gumu kuacha lakini anataka kuondoka kwani anadhani wakati umefika kuangalia mustakabali mwingine katika maisha yake. Taarifa zinadai kuwa Arteta ambaye alisajiliwa Arsenal kwa kitita cha paundi milioni 10 kutoka Everton mwaka 2011 amepata ofa za kufundisha katika klabu za Manchester City na Spurs pamoja na Arsenal.

KOCHA WA UINGEREZA ATAJA SILAHA ZAKE ZA EURO 2016. WALCOTT ATEMWA.

KOCHA wa timu ya taifa ya Uingereza, Roy Hodgson ametaja kikosi chake cha awali cha wachezaji 26 kwa ajili ya michuano ya Euro 2016 huku akimjumuisha mshambuliaji chipukizi wa Manchester United Marcus Rashford. Winga wa Newcastle United Andros Townsend na kiungo wa Arsenal Jack Wilshere nao pia wamejumuishwa katika kikosi hicho kitakachoshiriki michuano hiyo itakayofanyika Ufaransa kuanzia Juni 10. Lakini Hodgson amewaacha nyota kadhaa katika kikosi hicho akiwemo winga wa Arsenal Theo Walcott, Phil Jagielka wa Everton na Mark Noble wa West Ham United. Muda wa mwisho kwa timu zote 24 kuwasilisha majina ya vikosi vyao vya wachezaji 23 ni Mei 31 mwaka huu. Uingereza imepangwa kundi B sambamba na Wales, Urusi na Slovakia ambapo mchezo wao kwnza unatarajiwa kuwa dhidi ya Urusi Juni 11 kabla ya kuivaa Wales Juni 16 na baadae Slovakia Juni 20.

Kikosi kamili ni
Makipa:
Joe Hart (Manchester City), Fraser Forster (Southampton), Tom Heaton (Burnley).

Mabeki: Gary Cahill (Chelsea), Chris Smalling (Manchester United), John Stones (Everton), Kyle Walker (Tottenham Hotspur), Ryan Bertrand (Southampton), Danny Rose (Tottenham Hotspur), Nathaniel Clyne (Liverpool).

Viungo: Dele Alli (Tottenham Hotspur), Ross Barkley (Everton), Fabian Delph (Manchester City), Eric Dier (Tottenham Hotspur), Danny Drinkwater (Leicester City), Jordan Henderson (Liverpool), Adam Lallana (Liverpool), James Milner (Liverpool), Raheem Sterling (Manchester City), Andros Townsend (Newcastle United), Jack Wilshere (Arsenal).

Washambuliaji: Wayne Rooney (Manchester United), Harry Kane (Tottenham Hotspur), Jamie Vardy (Leicester City), Daniel Sturridge (Liverpool), Marcus Rashford (Manchester United).

UPANDE MMOJA WA JUKWAA PARC DE PRINCES KUITWA JINA LA IBRAHIMOVIC.

RAIS wa Paris Saint-Germain-PSG, Nasser al-Khelaifi amebainisha kuwa mabingwa hao wa Ufaransa wanapanga kuupa jina la mshambuliaji anayeondoka Zlatan Ibrahimovic upande wa jukwaa la uwanja wa timu hiyo. Ibrahimovic mwenye umri wa miaka 34 alitangaza Ijumaa iliyopita kuwa anatarajiwa kuondoka mwishoni mwa msimu huu, ingawa PSG wamesema kuwa amekubali kurudi katika uongozi pindi atakapostaafu soka lake. Jumamosi iliyopita mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Sweden alifunga mabao mawili katika mchezo wa mwisho wa ligi ambao PSG walishinda mabao 4-0 dhidi ya Nantes. Kwa kufanya hivyo, Ibrahimovic aliipita rekodi iliyowekwa na carlos Bianchi ya kufunga mabao 37 katika msimu mmoja wa Ligue 1 hivyo kumaanisha kuwa sasa amefikisha mabao 154 katika mashindano yote toka ajiunge na klabu hiyo akitokea AC Milan 2012.

Friday, May 13, 2016

VARDY ATEULIWA KUWA MCHEZAJI BORA WA MSIMU.

MSHAMBULIAJI wa Leicester City, Jamie Vardy ameteuliwa kuwa mchezaji bora wa msimu wa Ligi Kuu baada ya kuiongoza vyema klabu hiyo mpaka kutwaa taji la Ligi Kuu. Klabu hiyo inayotoka East Midlands ambayo ilitangaza tuzo hiyo kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter leo, walitwaa taji hilo katika hali ya kushangaza kutokana na kutopewa nafasi kabisa mwanzoni mwa msimu. Vardy pia anafukuzia tuzo ya kiatu cha dhahabu inayotolewa kwa mfungaji bora wa ligi, akiwa amefunga mabao 24 mpaka sasa bao moja nyuma ya Harry Kane wa Tottenham Hotspurs huku kukiwa kumebaki mechi moja kabla msimu kumalizika. Leicester wanatarajia kuwafuata mabingwa wa msimu uliopita Chelsea wakati Spurs wao watakwenda kwa Newcastle United ambao tayari wameshashuka daraja.

VARDY ATEULIWA KUWA MCHEZAJI BORA WA MSIMU.

MSHAMBULIAJI wa Leicester City, Jamie Vardy ameteuliwa kuwa mchezaji bora wa msimu wa Ligi Kuu baada ya kuiongoza vyema klabu hiyo mpaka kutwaa taji la Ligi Kuu. Klabu hiyo inayotoka East Midlands ambayo ilitangaza tuzo hiyo kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter leo, walitwaa taji hilo katika hali ya kushangaza kutokana na kutopewa nafasi kabisa mwanzoni mwa msimu. Vardy pia anafukuzia tuzo ya kiatu cha dhahabu inayotolewa kwa mfungaji bora wa ligi, akiwa amefunga mabao 24 mpaka sasa bao moja nyuma ya Harry Kane wa Tottenham Hotspurs huku kukiwa kumebaki mechi moja kabla msimu kumalizika. Leicester wanatarajia kuwafuata mabingwa wa msimu uliopita Chelsea wakati Spurs wao watakwenda kwa Newcastle United ambao tayari wameshashuka daraja.