Wednesday, August 17, 2016

MAHREZ ASAINI MIAKA MINNE LEICESTER.

KLABU ya Leicester City imetangaza kuwa winga wao Riyad Mahrez amesaini mkataba mpya wa miaka minne na mabingwa hao wa Ligi Kuu. Mahrez mwenye umri wa miaka 25, amekuwa akihusishwa na tetesi za kuwindwa na Arsenal katika kipindi hiki cha usajili wa kiangazi. Lakini nyota huyo wa kimataifa wa Algeria amefuata nyayo za mshambuliaji Jamie Vardy kwa kusaini mkataba wa muda mrefu na klabu hiyo. Mahrez amefunga mabao 17 na kusaidia mengine 11 ambayo yaliisaidia kwa kiasi kikubwa Leicester kutwaa ubingwa msimu uliopita. Akihojiwa Mahrez amesema Ligi Kuu ni ligi nzuri na anataka kubaki hapo kwa kipindi kirefu iwezekanavyo.

BRAZIL YAPATA NAFASI YA KULIPA KISASI KWA UJERUMANI OLIMPIKI.

TIMU ya taifa ya Brazil inatarajiwa kukwaana na Ujerumani katika hatua ya fainali ya michuano ya soka ya Olimpiki kwa wanaume Jumamosi hii. Hiyo itakuwa nafasi ya kipekee kwa Brazil kulipa kisasi kufuatia kipigo kizito cha mabao 7-1 walichopata kutoka kwa Ujerumani katika nusu fainali ya michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2014 ambayo pia ilifanmyika Brazil. Brazil walifikia hatua hiyo kwa staili ya aina yake katika Uwanja wa Maracana kufuatia kuisambaratisha Honduras kwa mabao 6-0 na kuweka hai matumaini yao ya kutwaa medali yao ya kwanza ya dhahabu ya Olimpiki. Katika mchezo huo Neymar aliweka historia kwa kufunga bao la mapema zaidi katika michuano hiyo ambalo alifunga zikiwa zimepita sekunde 14 toka kuanza kwa mchezo. Kwa upande wa Ujerumani wao walitinga hatua hiyo baada ya kuibugiza Nigeria kwa mabao 2-0 ambapo wawakilishi hao wa Afrika watacheza na Honduras kwa ajili ya kugombea medali ya shaba ya mshindi wa tatu.

MASCHERANO KUKOSA MWANZO WA MSIMU.

BEKI wa Barcelona, Javier Mascherano anatarajiwa kukosa mchezo wa ufunguzi wa La Liga dhidi ya Real betis kutokana na majeruhi ya msuli wa paja aliyopata. Nyota huyo wa kimataifa wa Argentina alipata majeruhi hayo wakati wa mchezo wa Super Cup dhidi ya Sevilla jana. Mascherano alitolea nje na kupelekea Barcelona ambao walikuwa wameshamaliza wachezaji wote watatu wa akiba, kumaliza mchezo huo wakiwa na 10 uwanjani. Hata hivyo, mabao mawili ya Arda Turan na moja la Lionel Messi yalitosha kuwahakikishia ushindi wa mabao 3-0 na kuwafanya kutwaa taji hilo kwa jumla ya mabao 5-0 katika michezo miwili waliyokutana.

Tuesday, August 16, 2016

RAIS WA ZAMANI WA FIFA AFARIKI DUNIA AKIWA NA UMRI WA MIAKA 100.

RAIS wa zamani wa Shirikisho la Soka Duniani, Joao Havelange amefariki dunia jijini Rio de Janeiro akiwa na umri wa miaka 100. Havelange ndio rais wa kwanza asiyekuwa raia wa Ulaya kuliongoza shirikisho hilo kuanzia mwaka 1974 mpaka 1998, wakati nafasi yake ilipochukuliwa na Sepp Blatter nay eye kupewa urais wa heshima. Alijiuzulu nafasi hiyo ya urais wa heshima mwaka 2013 baada ya taarifa iliyotolewa na mwenyekiti wa kamati ya maadili ya FIFA Hans-Joachim Eckert kumtuhumu kupokea rushwa katika kipindi chake cha uongozi. Havelange aliwahi kushiriki michuano ya Olimpiki akiwa muogeleaji kutoka Brazil mwaka 1936 na alikuwa mmoja wa waogelaji katika timu ya polo huko Helsinki. Katika michuano ya Olimpiki iliyofanyika jijini Melbourne mwaka 1956, Havelange alikuwa kiongozi wa msafara wa Brazil kabla ya kujiunga na Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki-IOC mwaka 1963. Havelange ndio mjumbe wa IOC aliyedumu kwa miaka mingi zaidi kabla ya kujizulu mwaka 2011.

POGBA ATUMIA MUDA WAKE WA MAPUMZIKO KWA KUUZA ICE CREAM.

Mshambuliaji mpya wa Manchester United Paul Pogba akihudumia moja ya wateja waliokuja katika duka ambalo alikuwa akiuza ice cream.

YAYA TOURE KUPIGANIA NAFASI YAKE CITY.

WAKALA wa kiungo wa Manchester City, Yaya Toure amesema mteja wake huyo amepanga kuendelea kubakia na kupigania nafasi yake katika kikosi cha timu hiyo pamoja na kuachwa katika mchezo wao wa kwanza wa msimu. Nyota huyo wa kimataifa wa Ivory Coast ambaye alicheza chini meneja mpya Pep Guardiola wakati wakiwa Barcelona, aliondolewa katika kikosi kilichopata ushindi mwembamba wa bao 2-1 dhidi ya Sunderland katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu. Toure mwenye umri wa miaka 33 pia hatacheza katika mechi ya leo ya mtoano ya michuano ya Ligi Mabingwa Ulaya dhidi ya Steaua Bucharest ya Romania lakini wakala wake Dimitri Seluk amesema mteja amepania kubaki na kupigania nafasi yake. Akihojiwa Seluk amesema Guardiola ni kocha bora duniani na ana matumaini atampa Toure nafasi ya kuonyesha kuwa bado anaweza kuifanyia kitu City.

HATIMAYE MARCOS REUS APATA LESENI.

WINGA wa kimataifa wa Ujerumani, Marco Reus ambaye alipigwa faini ya euro nusu milioni mwaka 2014 baada ya kugundulika kuendesha gari miaka kadhaa bila kuwa na leseni hatimaye amefanikiwa kufaulu majaribio ya udereva. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 27, hakushiriki michuano ya Ulaya mwaka huu ambapo Ujerumani ilitolewa katika hatua ya nusu fainali na Ufaransa kutokana na majeruhi, hivyo aliutumia muda huo kujifunza sheria za barabarani na kujiandaa na jaribio la nadharia. Akihojiwa kuhusiana na hilo, Reus alithibitisha kuwa ni kweli amefaulu majaribio na kueleza furaha yake kuwa sasa suala hilo limepita salama. Reus ambaye ameicheza Ujerumani mechi 29, alifaulu majaribio ya nadharia na vitendo jana na alikabidhiwa leseni yake wakati akielekea mazoezini mapema leo.