Monday, October 17, 2016

KAULI KUMPONZA MOURINHO

CHAMA cha Soka cha Uingereza-FA kinafanya uchunguzi kuhusiana na kauli aliyotoa meneja wa Manchester United Jose Mourinho kuelekea mchezo wao wa Ligi Kuu dhidi ya Liverpool baadae leo. Mourinho alikaririwa akidai kuwa mwamuzi Anthony Taylor ambaye ni mwenye wa Manchester, hataweza kuchezesha vyema pambano hilo kutokana na uteuzi wake kukosolewa. Taratibu za FA huwa hazitaki makocha kujadili suala lolote kuhusiana na mwamuzi kabla ya mchezo. FA inataka kuchunguza matamshi hayo kabla ya kuamua ni hatua gani kama ipo inaweza kuchukuliwa.

PETIT AICHANA ARSENAL.

KIUNGO wa zamani wa Arsenal, Emmanuel Petit anaamini kuwa klabu hiyo bado inahitaji mshambuliaji wa daraja la juu ili waweze kushindania taji la Ligi Kuu msimu huu. Arsenal kwasasa wanashika nafasi ya pili wakitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa na Manchester City waliopo kileleni. Petit ambaye enzi zake amewahi kucheza sambamba na kina Ian Wright, Dennis Bergkamp na Thierry Henry, anadhani Arsenal wanahitaji kuwa na mshambuliaji mwenye nja zaidi ya mabao ili waweze kuwa mabingwa wa ligi. Akihojiwa Petit ambaye pamoja na kwamba anaipenda Arsenal lakini ukweli ni kwamba hawataweza kushinda taji la ligi kama hawatakuwa na mashambuliaji mwenye wa kufunga mabao 40 kwa msimu kama ilivyo kwa Sergio Aguero.

Thursday, October 13, 2016

SPURS KUMUWANIA ISCO JANUARI.

KLABU ya Tottenham Hotspurs inadaiwa kuwa tayari kuvunja rekodi yao kwa kutoa kitita paundi milioni 40 kwa ajili ya kumsajili Isco kutoka Real Madrid Januari mwakani. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 24 amekuwa akihangaika kupata nafasi katika kikosi cha Zinedine Zidane, akianza katika mechi mbili pekee msimu huu na alikuwa akihusishwa na tetesi za kwenda Spurs kipindi cha kiangazi. Madrid wanadaiwa kuwa tayari kumuuza, huku chaguo la kumnasa kwa mkopo na nafasi ya kumnunua moja kwa moja pia vikiwepo. Isco aliyenunuliwa na Madrid akitokea Malaga miaka mitatu iliyopita tayari ameshaeleza nia yake ya kuindoka kama atakosa nafasi katika kikosi cha kwanza.

MARADONA ATAKA KUZICHAPA NA VERON KATIKA MCHEZO WA HISANI.

NGULI wa soka wa Argentina, Diego Maradona na Juan Sebastian Veron jana ilibaki kidogo wazichape katika mchezo wa hisani uliofanyika jijini Rome, Italia. Wawili hao walikuwa wakibadilishana maneno mpaka kufikia hatua ya kutaka kushikana wakati wakielekea nje ya uwanja wakati wa mapumziko. Mchezo mahsusi kwa ajili ya kuhamasisha amani ulioandaliwa na Pope Francis ulihusisha nyota kadhaa waliostaafu na ambao bado wanacheza akiwemo Ronaldinho, Francesco Totti, Edgar Davids, Hernan Crespo na Bojan Krkic. Kisa cha sakata hilo ni Maradona kuonyeshwa kutofurahishwa na jinsi Veron alivyokuwa akimchezea ambapo ilibidi azuiwe na beki wa zamani wa kimataifa wa Brazil Cafu pamoja na watu wa usalama wakati akitaka kwenda kumvaa Veron.

BALE KUONGEZWA MIAKA SITA MADRID.


VYOMBO vya habari nchini Hispania, vimeripoti kuwa Gareth Bale amekubalia kusaini mkataba mpya wa miaka sita na Real Madrid na mabingwa hao wa Ulaya pia wanajipanga kutangaza miakataba mipya ya Cristiano Ronaldo, Pepe na Luka Modric. Taarifa hizo zinadai kuwa Bale ambaye alijiunga na Madrid kwa ada iliyovunja rekodi ya euro milioni 100 mwaka 2013, anatarajiwa kusaini mkataba mpya ambao utamalizika mwaka 2022 katika kipindi cha wiki mbili zijazo. Beki wa kati Pepe ambaye mkataba wake wa sasa unamalizika mwakani, naye ataongezewa mkataba mwingine utakaokwisha mwaka 2018. Ronaldo ambaye ni mfungaji wa wakati wote wa klabu hiyo, yeye anatarajiwa kupewa mkataba utakaomalizika mwaka 2020 sambamba na kiungo mchezeshaji Modric.

WILLIAN ATHIBITISHA KIFO CHA MAMA YAKE.

WINGA mahiri wa Chelsea, Willian amethibitisha katika ukurasa wake wa mtandao wakijamii wa Facebook, kifo cha mama yake mzazi aliyekuwa akisumbuliwa na maradhi ya saratani. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 28 amebainisha kuwa mama yake alianza kusumbuliwa na maradhi hayo Septemba mwaka huu na alikuwa akipatiwa matibabu nchini kwao Brazil. Willian alirejea jijini London tayari kwa ajili ya mchezo wa Jumamosi hii dhidi ya Leicester City baada ya kutoka kuitumikia Brazil na kufunga bao katika ushindi wa mabao 2-0 waliopata dhidi ya Venezuela Jumapili iliyopita. Salamu za pole kwa nyota huyo zimeendelea kumiminika kutoka sehemu mbalimbali ikiwemo klabu yake ya Chelsea ambayo imesema kuwa wako pamoja na Willian na familia yake katika kipindi hiki kigumu.

BELLERIN KUONGEZWA MKATABA ARSENAL.

MENEJA wa Arsenal, Arsene Wenger amethibitisha mipango ya kumuongeza mkataba mpya Hector Bellerin wakati ambao Barcelona nao wanamuwinda beki huyo wa kimataifa wa Hispania. Bellerin alijiunga na akademi ya Arsenal akitokea ile ya Barcelona ya La Masia mwaka 2011 na kuibukia katika kikosi cha kwanza mwaka 2014. Msimu uliopita Bellerin alicheza mechi zote za Ligi Kuu za Arsenal huku mwaka huu pia akiendelea kupata nafasi katika klabu hiyo ambayo imepelekea kuitwa katika kikosi cha Hispania. Barcelona walishawahi kumrejesha Cesc Fabregas Camp Nou baada ya kupitia uelekeo kama wa Bellerin na wamekuwa wakihusishwa na tetesi za nyota huyo mwenye umri wa miaka 21 katika kipindi hiki ambacho wanataka kuziba nafasi ya Dani Alves. Akihojiwa Wenger ameshangazwa na taarifa hizo kwani beki huyo bado ana miaka mitatu katika mkataba wake Emirates na kubainisha kuwa klabu hiyo inajipanga kumuongezea miaka mingine zaidi.