Saturday, March 10, 2012

DROGBA KUCHANGISHA ZA MFUKO WAKE.

MFUKO wa Didier Drogba, leo utafanya hafla ya uchangishaji fedha katika hoteli ya Dorchester Hotel mjini London, lengo likiwa ni kukusanya kiasi cha pauni Milioni 3 kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa hospitali nchini kwao Ivory Coast. Zoezi hilo la tatu kufanyika katika mradi huo, linatarajiwa kuhusisha watu kibao maarufu, wakiwemo wanasoka nyota duniani na wanasiasa. Mazagazaga kibao, zikiwemo jezi za mchezaji huyo, za rafiki zake na wachezaji wenzake, viatu, soksi na kadhalika vitauzwa kwenye zoezi hilo la hisani. Nahodha huyo wa kimataifa wa Ivory Coast amesema kuwa ushirikiano ambao amepata katika mfuko wake huo ni kubwa na akasisitiza kuwa bado wana kazi kubwa huko ya kufanya katika siku zijazo. Kituo cha afya cha Gigantic kinajengwa katika wilaya ya Attecoube mjini Abidjan, eneo la watu fukara ambalo linakosa hadi zana za kisasa za tiba na huduma hospitalini hapo zitakuwa zikitolewa bure.

Mfuko huo uitwao-Didier Drogba Foundation ulianzishwa mwaka 2007, kwa lengo la kushughulika na masuala ya kiafya na elimu Afrika.

Thursday, March 8, 2012

ZAMALEK, AL AHLY KUCHEZA MCHEZO WA HISANI KUWAKUMBUKA WALIOPOTEZA MAISHA.

MWENYEKITI wa klabu ya Zamalek, Mamdouh Abbas ametangaza kwamba mechi ijayo dhidi ya wapinzani wao wa jadi, Al Ahly itafanyika baadaye mwezi huu. Abbas ameaimbia SuperSport kwamba amekubaliana na Mwenyekiti wa Al Ahly, Hassan Hamdy na ofa hiyo imekubaliwa, sasa wanasubiria Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi hiyo kuwaunga mkono ili kuidhinisha mchezo huo ambao wamepanga ufanyike Machi 23 au 27 mwaka huu. Abbas amesema kuwa katika mchezo huo, kila timu itavaa jezi za mpinzani wake ili kuonyesha umoja, hiyo ikiwa ni mara ya kwanza katika historia ya upinzani wa timu hizo. Mechi hii inakuja siku chache baada ya kutokea janga la mauaji ya watu 74 lililotokea kwenye mji wa Port Said wakati wa mechi ya Ligi Kuu ya Misri kati ya Al Masry na Al Ahly.

BEKI WA ZAMANI WA REAL MADRID AFARIKI.

BEKI wa zamani wa klabu ya Real Madrid Marcos Alonso Imaz ambaye aliisaidia klabu hiyo kushinda kombe la Ulaya mara tano mfululizo amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 78. Mchezaji huyo ambaye alikuwa akijulikana kwa jina la utani la Marquitos amewahi pia kuichezea timu ya taifa ya Hispania mara mbili lakini mafanikio alipata wakati akikipiga katika klabu ya Real Madrid ambapo aliiwezesha timu hiyo kushinda michuano ya Ulaya mfululizo kuanzia mwaka 1956 mpaka 1960. Mzee huyo pia aliiwezesha klabu hiyo kombe la mabara 1960 na Kombe la Ligi Kuu nchini Hispania mara sita kuanzia mwaka 1954 mpaka mwaka 1962 baada ya kujiunga na klabu hiyo akitokea klabu ya Racing Santander. Akitoa salamu zake za rambirambi mchezaji mwenzake ambao wote walicheza enzi hizo Alfredo di Stefano amesema kuwa Marquitos alikuwa ni moja kati mabeki bora kabisa kuwahi kutokea enzi hizo.

RONALDO ATETEA KAULI YA VALCKE.

MCHEZAJI nguli wa zamani wa Brazil Ronaldo de Lima amekiri kuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA Jerome Valcke alikuwa yuko sahihi kuhusiana na matatizo yaliyopo katika maandalizi ya michuano ya Kombe Dunia 2014 nchini Brazil. Valcke aliingia katika mzozo na Wziri wa Michezo wa nchi hiyo Aldo Rebelo kufuatia kauli yake aliyotoa ambayo waziri huyo alisema ni ya kuudhi hivyo kuiandikia barua FIFA kwamba hawatafanya kazi na katibu huyo kwenye tena. Akihojiwa kuhus suala hilo Ronaldo amesema kuwa Valcke tayari ameomba msamaha kutokana na kauli yake hiyo lakini hilo haliwezi kuficha ukweli kwamba alikuwa yuko sahihi alitoa kauli hiyo. Ronaldo ambaye ni mmoja wa wajumbe wa kamati ya maandalizi ya michuano hiyo aliendelea kusema kuwa ni ukweli kwamba nchi hiyo iko nyuma ya muda kuhusiana na suala la miundo mbinu na pia vitu vingi vipo nyuma ya wakati.

BALOTELLI ALIMWA MSHAHARA.

KLABU ya Manchester City imemkata mshahara wa wiki moja mshambuliaji wake Mario Balotelli kutokana na tabia za utovu wa nidhamu. Kocha wa City Roberto Mancini aliwaambia waandishi wa habari kabla ya mchezo wa kwanza wa timu hiyo dhidi ya Sporting ya Ureno wa michuano wa Ligi ya Ulaya mchezo ambao unatarajiwa kuchezwa jioni. Mchezaji huyo alivunja amri ilimkataza kuzurura Ijumaa asubuhi ikiwa ni siku moja kabla City kucheza mchezo wa Ligi dhidi ya Bolton Wanderers mchezo ambao mshambuliaji huyo wa kimataifa kutoka Italia alifunga bao. Balotelli amekuwa akikumbwa na matatizo ya mara kwa mara akiwa ndani ya uwanja na nje kutokana na utukutu wake toka alipojiunga na klabu hiyo mwaka 2010.

MESSI APIGA TANO BARCA IKISHINDA MABAO 7-1.

MSHAMBULIAJI wa Barcelona Lionel Messi ameweka historia mpya katika michuano ya Klabu Bingwa Ulaya baada ya kufanikiwa kufunga mabao matano wakati timu yake ikiibuka na ushindi wa wa mabao 7-1 dhidi ya Bayer Liverkusen. Mabingwa hao watetezi walifanikiwa kushinda mchezo huo na kufanikiwa kutinga hatua ya robo fainali kwa kishindo kwa jumla mabao 10-2 huku Messi akiweka historia ya kuwa mchezaji wa kwanza kushinda idadi hiyo ya mabao katika michuano hiyo. Akihojiwa mara baada ya mchezo huo kocha wa Leverkusen Robin Dutt alisifia kiwango cha timu ya Barcelona akisema kuwa timu inapocheza bila Messi inakuwa bora lakini kama anakuwepo uwanjani timu inakuwa ni kama imetoka sayari nyingine. Kocha wa Barcelona Pep Guardiola pia alimsifu mshambuliaji wake huyo kwa kiwango alichokionyesha akisema kuwa hakutawahi kutokea mchezaji huko siku za mbele mwenye kiwango cha kipekee kama Messi. Mshambuliaji huyo bora wa dunia mara tatu alifunga mabao yake katika dakika 25, 42 na 49 na kutimiza idadi ya kufunga mabao matatu mfululizo-Hat Trick mara 17 akiwa na klabu ya Barcelona kabla ya kuongeza mengine mawili dakika ya 58 na 84 ya mchezo huo.

Tuesday, March 6, 2012

KAKA AANZA KUREJESHA MAKALI YAKE.

KIUNGO wa Kimataifa kutoka Brazil, Kaka anaonekana kurudi katika kiwango chake na mashabiki wa klabu ya Real Madrid wanaamini kiungo huyo amerejesha makali yake kama aliyokuwa nayo alipokuwa akiichezea klabu ya AC Milan ya Italia. Kaka alionekana akicheza kwa kiwango cha juu Jumapili iliyopita wakati kikosi chake cha Madrid kilipofanikiwa kushinda mabao 5-0 dhidi ya Espanyol ambapo mchezaji huyo alifunga bao moja huku akitengeneza mawili kwa mshambuliaji Gonzalo Higuain. Lakini mbali ya kushinda bao hilo na kutengeneza mengine kikubwa mchezaji huyo alichokionyesha ni jinsi alivyokuwa na kasi na nguvu kwenye mchezo huo mpaka watu kukumbuka enzi zake wakati akiwa katika kiwango cha juu kwenye kusakata kabumbu. Maisha nchini Hispania hayakuwa rahisi kwa mchezaji huyo kwa sababu kubwa tatu ya kwanza ikiwa ni usajili wake ambao ulikuwa ukisubiriwa kwa hamu na muda mrefu sababu ya pili ni kiasi ambacho mchezaji huyo alinunuliwa na tatu majeraha yaliyokuwa yakimsumbua na kusababisha kushindwa kucheza katika kiwango ambacho kilitegemewa na wengi.