 |
Andriy Shevchenko. |
MSHAMBULIAJI wa zamani wa Chelsea Andriy Shevchenko ametangaza kustaafu kucheza soka rasmi ili aweze kujishughulisha na nmasuala ya siasa. Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ukraine mwenye miaka 35 alithibisha taarifa hizo ambazo zilitolewa katika mtandao wa klabu ya Dynamo Kiev ambayo alikuwa akicheza. Shevchenko amecheza mechi 111 kwa nchi yake ambapo mara ya mwisho ilikuwa katika michuano ya Ulaya iliyomalizika mapema mwezi huu ambapo Ukraine ilifungwa bao 1-0 na Uingereza. Mshambuliaji huyo aliibukia katika klabu ya Dynamo mwaka 1994 na baadae kuhamia klabu ya AC Milan mwaka 1999 ambapo alifanikiwa kushinda taji la Ligi ya mabingwa ya Ulaya mwaka 2003 na klabu hiyo huku yeye akiwa ndio nyota wa mchezo baada ya kushinda penati ya mwisho. Akiwa na miaka 29 Shevchenko alihamia katika klabu ya Chelsea ambayo ilikuwa ikifundishwa na Jose Mourinho mwaka 2006 kwa ada paundi milioni 30 lakini hakupata mafanikio katika misimu miwili aliyochezea klabu hiyo na kuamua kurejea AC Milan ambapo nako hakukaa sana kabla ya kuamua kurejea Dynamo mwaka 2009. Shevchenko amefunga mabao 48 na kurekodi ya mchezaji aliyefunga mabao mengi zaidi katika timu ya taifa ya nchi hiyo huku akikiongoza kikosi cha nchi hiyo kilichofika hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2006 na pia aliwahi kutunukiwa tuzo ya mchezaji bora barani Ulaya mwaka 2004.
 |
Roger Federer. |
WACHEZA tenisi nyota Roger Federer na Serena Williams wameanza vyema kampeni zao za kuhakikisha wanaondoka na medali ya dhahabu katika michuano ya Olimpiki baada ya kushinda michezo yao ya kwanza. Federer kutoka Switzerland ambaye anashikilia namba moja katika orodha za ubora za mchezo huo duniani kwa upande wa wanaume alifanikiwa kumfunga Alejandro Falla kutoka Colombia kwa 6-3 5-7 6-3. Kwa upande wa wanawake Williams ambaye anashika nafasi ya nne katika orodha za ubora alifanikiwa kumfunga kirahisi Jelena Jankovic kutoka Serbia kwa 6-3 6-1 na kufanikiwa kutinga raundi ya pili. Kim Clijsters kutoka Ubelgiji ambaye amepanga kustaafu mchezo huo mwishoni mwa mwaka huu alifanikiwa kumfunga Roberta Vinci kutoka Italia kwa 6-1 6-4 ambapo sasa anatarajiwa kukutana na Carla Suarez wa Hispania katika mzunguko wa pili wakati Serena atakutana na Urszula Radwanska wa Poland. Federer atacheza na Julien Benneteau kutoka Ufaransa ambaye alimfunga kwa seti tano katika michuano ya Wembledon iliyopita.
 |
Ye Shiwen. |
MUOGELEAJI Ye Shiwen kutoka China amevunja rekodi ya dunia ya mita 400 katika mchezo huo na kunyakuwa medali ya dhahabu katika michuano ya Olimpiki inayoendelea jijini London, Uingereza. Shiwen mwenye miaka 16 aliweka rekodi hiyo akitumia muda bora wa dakika 4:28:43 mbele ya bingwa wa dunia kutoka Marekani Elizabeth Beisel na Li Xuanxu ambaye pia anatoka China. Muogeleaji huyo alivunja rekodi ya muda wa dakika 4:29:45 ambayo ilikuwa imewekwa na Stephanie Rice kutoka Australia katika michuano ya olimpiki iliyofanyika Beijing mwaka 2008. Muogeleaji kutoka Uingereza Hannah Miley ambaye alishinda medali ya fedha katika mashindano ya dunia mwaka jana na kutegemewa kufanya vizuri katika mashindano hayo alishindwa kutamba baada ya kumaliza katika nafasi ya tano. Mara baada ya mashindano hayo Miley aliomba radhi mashabiki wake ambao walitarajia atafanya vizuri ambapo kwasasa amesema anahamishia nguvu zake katika mbio za kuogelea za mita 200 kuhakikisha anafanya vyema.
KLABU ya Tottenham Hotspurs imekubali kumuuza kiungo wake Luka Modric kwa ada ya paundi milioni 36 kwenda klabu ya Real Madrid ya Hispania. Kiungo huyo wa kimataifa wa Croatia tayari alishasema kuwa atajiunga na Madrid lakini alikuwa akisubiria klabu hizo kufikia makubaliano. Modric kidogo apoteze nafasi yake ya kwenda Madrid baada ya kukataa kusafiri na Spurs katika ziara huko nchini Marekani lakini viongozi wa Madrid walimlazimisha kuomba msamaha na kwenda kwenye ziara hiyo. Mkataba huo utamaliza utata wa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26 ambaye alianza kushinikiza kuondoka kwenda Chelsea mwaka uliopita lakini alikataliwa na klabu yake hiyo.
 |
Usain Bolt. |
MWANARIADHA nyota wa mbio fupi kutoka Jamaica, Usain Bolt amekiri kuwa maumivu ambayo yalikuwa yakimsumbua yaliathiri kiwango chake kwa kiasi fulani. Bolt amesema kuwa maumivu hayo ya mgongo kwasasa yamepona na yuko tayari kutetea taji lake wakati atakapopeperusha bendera ya nchi yake katika sherehe za ufunguzi wa michuano hiyo baadae leo. Nyota huyo ambaye anashikilia rekodi ya dunia ya sekunde 9.58 katika mbio za mita 100 alishindwa kutamba mbele ya mjamaica mwenzake Yohan Blake katika mbio za majaribio zilizofanyika jijini Kingston na baadae kukosa mbio za Diamond League zilizofanyika jijini Monaco. Akihojiwa Bolt amesema kuwa katika mbio hizo alikuwa yuko sawa lakini hakuwa katika kiwango chake ambacho amekizoea lakini anashukuru baada ya mapumziko na mazoezi aliyokuwa akifanya anaamini anaweza kutete taji lake kwenye michuano hiyo. Bolt pia alishukuru kwa kupewa heshima ya kubeba bendera ya nchi yake katika sherehe za ufunguzi wa michuano hiyo ambayo inatarajiwa kufanyika baadae usiku.