Thursday, October 4, 2012

BLANC ANENA KUWA WAAJIRI WAKE WALIKUWA HAWAMTAKI.

ALIYEKUWA kocha wa timu ya taifa ya Ufaransa, Laurent Blanc amebainisha kuwa alijiengua katika nafasi hiyo kwasababu Shirikisho la Soka la Ufaransa lilikataa kumuongeza mkataba mwingine. Blanc aliacha kukinoa kikosi cha nchi hiyo baada ya kupoteza mchezo dhidi ya waliokuja kuwa mabingwa wa michuano ya Ulaya 2012 Hispania kwa mabao 2-0 katika mchezo wa robo fainali. Akihojiwa kocha huyo ambaye naye pia amewahi kucheza katika kikosi cha nchi hiyo amesema kuwa alikuwa akisubiri waajiri wake wamuongeze mkataba mwingine lakini walionekana kukaa kimya hivyo akaona bora aondoke mwenyewe kwa kuwa hawakuonekana kumuhitaji. Blanc alifafanua kuwa kuondoka kwake hakukutokana na wachezaji ambao baada ya michuano ya hiyo waliitwa na Kamati ya Nidhamu ya shirikisho hilo kutokana na tabia za utovu wa nidhamu walizozionyesha. Wachezaji ambao waliitwa na kamati hiyo ni pamoja na Samir Nasri, Jeremy Menez, Yann M’Vila na Hatem Ben Arfa ambapo kati ya hao Nasri alifungiwa michezo mitatu na Menez mchezo mmoja.

MANCINI ACHUKIZWA NA KIWANGO CHA MAN CITY.

MENEJA wa klabu ya Manchester City, Roberto Mancini amekiri kuwa kikosi chake bado kinahitaji marekebisho makubwa ili kiweze kurejesha makali yake kama ilivyokuwa msimu uliopita. Penati iliyokuwa na utata ambayo ilipigwa Mario Balotelli ndio pamoja na kiwango bora alichokionyesha Joe Hart kwa kuokoa michomo mingi ya Borussia Dortmund ndio iliwaokoa City wasipate kipigo kingine nyumbani baada ya kufungwa na Real Madrid katika mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Ulaya. City ambao ambao walifanikiwa kutoka sare ya bao 1-1 katika mchezo huo wamefanikiwa kushinda michezo mitatu pekee kati ya tisa walioyocheza katika mashindano yote msimu huu. Akihojiwa Mancini amesema kuwa tatizo la kikosi chake analijua na atajitahidi kulitafutia ufumbuzi kabla timu hiyo haijapata madhara zaidi katika kampeni zake msimu huu. Mancini aliendelea kusema kuwa katika mchezo wa jana Dortmund walionekana bora kuliko wao na kama wanahitaji kusonga mbele katika michuano hiyo hawana budi kuongeza jitihada na kucheza katika kiwango cha juu.

Wednesday, October 3, 2012

TAARIFA KUTOKA TFF LEO.

TWFA YATANGAZA KIPINDI CHA PINGAMIZI
Kamati ya Uchaguzi ya Chama cha Mpira wa Miguu cha Wanawake (TWFA) imetangaza kipindi cha pingamizi kwa waombaji uongozi katika uchaguzi wa chama hicho utakaofanyika mwezi ujao. Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati hiyo Ombeni Zavala, kipindi cha pingamizi ni kuanzia Oktoba 5 hadi 9 mwaka huu, na pingamizi ziwasilishwe ofisi za TWFA. Mwisho wa kupokea pingamizi ni saa 10 kamili jioni, na hakuna ada kwa ajili ya pingamizi. Pia amesema usaili kwa wagombea utafanyika kati ya Oktoba 12 na 14 mwaka huu kuanzia saa 3 asubuhi kwenye ofisi za TWFA zilizopo Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam. Kila mgombea anatakiwa kufika kwenye usaili akiwa na vyeti vyake halisi (original) vya kitaaluma. Waombaji wa uongozi kwenye uchaguzi huo ni Lina Paul Kessy, Isabellah Hussein Kapera na Joan Ndaambuyo Minja (Mwenyekiti) wakati mwombaji wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti ni Roseleen Kissiwa. Nafasi ya Katibu Mkuu imevutia wagombea wawili; Amina Ali Karuma na Cecilia Oreste Makafu. Mark Raghton Mhango ni mgombea pekee wa nafasi ya Katibu Msaidizi kama ilivyo kwa Rose Msamila anayewania nafasi ya Mhazini. Wagombea wanne wameomba nafasi ya ujumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Wagombea hao ni Furaha Emily Francis, Zena Suleiman Chande, Jasmin Badar Soud, Juliet Edwin Mndeme. Wanaowania ujumbe wa Kamati ya Utendaji ni Rahim Salum Maguza, Triphonia Ludovick Temba na Sophia James Charles.

BRAZIL YAENDELEA KUBAKIA NJE YA KUMI BORA ORODHA ZA FIFA.

NCHI za Ulaya zimeendelea kutamba katika orodha za juu za ubora zinazotolewa kila mwezi na Shirikisho la Soka Duniani-FIFA huku Hispania ikiendelea kuwa king’ang’anizi na kubakia katika nafasi ya kwanza katika orodha hizo huku Tanzania ikibakia katika nafasi yake ya 132 waliyokuwepo mwezi uliopita. Nafasi ya pili inashikiliwa na Ujerumani huku nafasi ya tatu ikishikwa na Ureno ambao wamepanda kwa nafasi moja, nafasi ya nne inashikiliwa na Argentina ambao wamepanda kwa nafasi tatu na tano bora inafungwa na Uingereza ambao mwezi uliopita walikuwa nafasi ya tatu. Nafasi ya sita inashikiliwa na Uholanzi ambao wamepanda nafasi mbili, Uruguay wako katika nafasi ya saba wakiwa wameporomoka nafasi mbili huku Italia nao wakidondoka mpaka nafasi ya nane kutoka ya sita waliyokuwa mwezi uliopita. Colombia ambao mwezi uliopita walikuwa katika nafasi ya 22 wamepaa mpaka nafasi ya tisa na 10 bora inafungwa na Ugiriki ambao wamepanda nafasi moja wakati mabingwa mara tano wa Kombe la Dunia Brazil bado wanasuasua baada ya kuanguka kwa nafasi mbili mpaka ya 14. Kwa upande wa tano bora ya Afrika nafasi ya kwanza bado inashikiliwa na Ivory Coast ambao wako nafasi ya 16, nafasi ya pili inashikiliwa na Algeria ambao wamepanda kwa nafasi nne mpaka ya 24, nafasi ya tatu wapo Mali ambao wamepanda kwa nafasi tano mpaka nafasi ya 27. Nafasi ya nne inashikiliwa na Misri wakiwa wameporomoka mpaka nafasi tatu mpaka ya 40 wakati mabingwa wa Afrika Zambia ndio wanakamilisha tano bora ya Afrika wakiwa katika nafasi ya 41.

AFRICAIN YATAKA HUDUMA YA SHEHATA.

KLABU ya Africain ya nchini Tunisia imeonyesha nia kutaka kumuajiri kocha wa zamani wa Zamalek ya Misri, Hassan Shehata ili kukinoa kikosi cha timu hiyo. Mapema klabu hiyo ilikatisha mkataba na aliyekuwa kocha wake Bernard Casoni ambaye ni raia wa Ufaransa kwa kile walichodai matokeo mabaya ambayo imekuwa ikipata timu hiyo katika michezo yake ya karibuni. Taarifa kutoka nchini Tunisia zinasema kuwa mbali na Shehata lakini pia kocha wa zamani wa klabu ya Al Ahly Manuel Jose aliwekwa katika orodha lakini Shehata ndiye aliyeibuka kidedea. Wakati Shehata akikataa kutoa kauli kuhusiana na hilo, kuna taarifa kuwa tayari ameshaanza mazungumzo na klabu hiyo kwa ajili ya kuchukua kibarua hicho.

FIFA YAMSIMAMISHA OFISA WA BIN HAMMAM.

KAMATI ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Duniani-FIFA limemsimamisha ofisa mmoja ambaye alikuwa akifanya kazi na Mohamed Bin Hammam baada ya kugoma kutoa ushirikiano katika uchunguzi dhidi ya bosi wake huyo wa zamani. Najeeb Chirakal ambaye alikuwa anafanya kazi katika Chama cha Soka nchini Qatar amefungiwa na kamati hiyo kwa miezi miwili au mpaka hapo atakapoamua kutoa ushirikiano katika uchunguzi huo. Katika taarifa yake waliyotuma katika mtandao kamati hiyo imesema kuwa Chirakal atafungiwa kwa miezi miwili au mpaka atapoamua kutoa ushirikiano kwa baadhi ya taarifa zinazohitajika katika uchunguzi huo. Bin Hammam anachunguzwa kutokana na tuhuma za utoaji rushwa wakati wa kampeni za kugombea kiti cha urais wa FIFA mwaka jana nafasi ambayo alishinda Sepp Blatter. Mbali na uchunguzi huo pia Bin Hammam mwenye umri wa miaka 63 raia wa Qatar pia anachunguzwa na Shirikisho la Soka barani Asia juu ya tuhuma za matumizi mabaya ya fedha wakati akiwa rais wa shirikisho hilo.

PUYOL KUIKOSA EL CLASICO.

BEKI wa kimataifa wa Hispania na klabu ya Barcelona, Carles Puyol amekimbizwa hospitali baada ya kuteguka kiwiko cha mkono wake wa kulia wakati timu yake iliopibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Benfica katika mchezo wa kundi G wa Ligi ya Mabingwa Ulaya jana. Kuumia kwa mchezo huyo ambaye ndio alikuwa akicheza kwa mara ya kwanza toka apone maumivu ya mguu yaliyokuwa yakimsumbua kutapelekea kukosa mchezo dhidi ya mahasimu wao Real Madrid utakaochezwa Jumapili katika Uwanja wa Nou Camp. Puyol mwenye umri wa miaka 34 alidondoka vibaya na kuumiza kiwiko chake wakati akiwa katika harakati ya kuwania mpira wa kona ambapo alitolewa nje katika dakika ya 78 na nafasi yake kuchukuliwa na Alex Song. Meneja wa Barcelona Tito Vilanova amesema kuwa wanasubiri vipimo vya madaktari ili kujua mchezaji huyo atakaa nje ya uwanja kwa muda gani lakini inavyoonekana atakosa mchezo wa Jumapili dhidi ya Madrid. Barcelona imekuwa ikiyumba katika safu yake ya ulinzi katika siku za karibuni baada ya mabeki wake tegemeo kuumia mara kwa mara ambapo Gerard Pique bado yuko nje ya uwanja kutokana akijiuguza kutokana na majeraha waliyopata.