Sunday, March 3, 2013

MWEKEZAJI KUTOKA MASHARIKI YA KATI ATAKA KUINUNUA ARSENAL.

M’BIA kutoka Mashariki ya Kati anajipanga kuweka zabuni ya kiasi cha paundi bilioni 1.5 kwa ajili ya kuimiliki moja kwa moja klabu ya Arsenal ya nchini Uingereza. Katika taarifa zilizochapishwa katika gazeti la Telegraph la nchi hiyo wawekezaji hao kutoka Mashariki ya Kati hawakutaka kujitambulisha kwanza mpaka mchakato huo utakapoanza rasmi. Taarifa katika gazeti hilo iliendelea kuelezea mipango ya wabia hao kuwa wataweka fungu la kutosha kwa ajili ya usajili ili kuigeuza klabu hiyo kubwa kuwa tishio barani Ulaya na Duniani kwa ujumla. Zabuni hiyo inatarajiwa kuweka wiki chache zijazo, wakiwa na nia ya kununua hisa zote za mmiliki wa sasa klabu hiyo Stan Kroenke kutoka Maekani ambaye anamiliki kampuni ya vifaa vya michezo. Pia wabia hao wamepanga kupunguza bei ya tiketi katika Uwanja wa Emirates na kuejesha heshima ya klabu hiyo waliokuwa nayo kipindi wanacheza katika uwanja wao wa kihistoria wa Highbury. Wawekezaji kutoka Mashariki ya kati wamekuwa wakimiminika kwa wingi barani Ulaya kuwekeza katika soka ambapo tayari klabu kama Manchester City inamilikiwa na mmoja wa wanafamilia ya kifalme ya Abu Dhabi.

KOMBE LA DUNIA KUCHEZWA MAJIRA YA BARIDI INAWEZEKANA - VALCKE.

Moja viwanja vitakavyotumika kwa ajili ya michuano ya Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar.
KATIBU mkuu wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA, Jerome Valcke amesema kuwa michuano ya Kombe la Dunia itakayofanyika nchini Qatar mwaka 2022 inaweza kuhamishwa kutoka kipindi cha kiangazi na kuchezwa katika kipindi cha baridi kama kutakuwa na ushahidi wa kitabibu ambao utaonyesha joto katika nchi hiyo ya jangwa linaweza kuwaathiri wachezaji. Kauli hiyo imekuja kufuatia rais wa Shirikisho la Soka barani Ulaya-UEFA, Michel Platini kutaka michuano hiyo ibadilishwe kutokana na joto kali katika majira ya kiangazi ambalo hufikia hadi nyuzi joto 40. Akijibu kauli hiyo mbele ya waandishi wa habari mara baada ya kumaliza mkutano wa bodi ya kimataifa nchini Scotland, Valcke amesema suala la kuandaa michuano ya Kombe la Dunia katika kipindi cha baridi linawezekana kama kukiwepo ushahidi wa kitabibu kwamba haitawezekana kuchezwa katika majira ya kiangazi kutokana na joto kali. Wanachosubiri FIFA ni barua rasmi ya maombi kutoka Qatar ya kuhamisha michuano hiyo katika kipindi cha baridi kama watakuwa wamemaliza uchunguzi wao na kuona haitawezekana kwa wachezaji kucheza soka katika hali ya joto kali katika majira ya kiangazi.

Real Madrid vs Barcelona 2 - 1 / All Goals & Full Highlights (El Clasico...

Saturday, March 2, 2013

TFF YAAMUA KUIANGUKIA SERIKALI.

SAKATA la uchaguzi wa Shirikisho la Soka nchini-TFF limechukua sura mpya baada ya shirikisho hilo kuamua kuiangukia serikali kuhusu tamko lake ililotoa hivi karibuni. Serikali kupitia Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Fenera Mukangara iliamua kuingilia kati sakata hilo kwa kuifuta katiba mpya ya mwaka 2012 iliyokuwa ikitumika katika uchaguzi huo pamoja na kumsimamisha msajili huku akiliamuru shirikisho hilo kutumia katiba ya zamani katika mchakato wake wa uchaguzi. Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kikao cha kamati hilo, rais wa shirikisho hilo Leodgar Tenga amesema marekebisho ya katiba yaliyofanyika yalikuwa ni halali kwakuwa walifuata taratibu zote zinazofaa. Tenga amesema kabla ya kufanya chochote walienda kwa msajili na baada ya siku 15 walikabidhiwa fomu na msajili ya kuendelea na mchatakato wao hivyo kama kuna makosa yalifanyika kwa msajili haoni kwanini iwaathiri wao. Amesema sio nia ya TFF kubishana na waziri ila wanaamini wakati anatoa tamko hilo hakujua ugumu wa utekelezaji wake na waliomshauri hawakuwa makini kuona madhara yanayoweza kujitokeza huko mbele. Kikao hicho pia kimeamua kutotuma barua Shirikisho la Soka Duniani-FIFA kuwaelezea mabadiliko hayo kwa hofu ya kufungiwa mpaka watakapokaa na waziri kuangalia uwezekano wa kutafuta suluhu ya suala hilo.

PLATINI ATAKA KOMBE LA DUNIA 2022 LIFANYIKE KIPINDI CHA BARIDI.

RAIS wa Shirikisho la Soka barani Ulaya-UEFA, Michel Platini amesema michuano ya Kombe la Dunia itakayofanyika Qatar 2022 italazimika kufanyika katika kipindi cha baridi ili kuwalinda wachezaji na mashabiki na joto kali. Qatar ilipewa nafasi ya kuwa mwenyeji wa michuano hiyo na Shirikisho la Soka Duniani-FIFA mwaka 2012 na inatarajiwa kufanyika katika kipindi cha kiangazi ambapo nyuzi joto hufikia kiasi cha sentigredi 40. Platini ambaye aliipigia kura Qatar ipewe nafasi ya kuandaa michuano hiyo amesema kwasababu ya joto kali nchini humo michuano hiyo itabidi ichezwe katika kipindi cha baridi ambacho huwa katika miezi ya Desemba na Januari. Platini ambaye pia aliipigia kura Urusi kupata nafasi ya kuandaa michuano hiyo mwaka 2018 aliendelea kusema kuwa kucheza soka katika joto kali linalofikia nyuzi joto 40 ni suala lisilowezekana kwa wachezaji. Suala hilo limezua mjadala mkubwa katika soka wadau wakihoji kwamba itakuwa ni suala lisilowezekana kusimamisha ligi zote kwa ajili ya kucheza Kombe la Dunia katika kipindi cha Desemba na Januari.

FIFA YAIMWAGIA SIFA LEBANON.

SHIRIKISHO la Soka Duniani-FIFA limeipongeza Lebanon kwa hatua walizochukua dhidi ya suala la upangaji matokeo na kuhitaji maelezo zaidi juu ya wachezaji na waamuzi waliofungiwa kwa tukio hilo. Chama cha Soka cha nchi hiyo kimewapa adhabu tofauti wachezaji 24 ikiwemo adhabu ya kifungo cha maisha kwa beki Ramez Dayoub na mshambuliaji Mahmoud El-Ali kufuatia tuhuma za matokeo katika mechi za nyumbani na kimataifa. Uchunguzi wa miezi miwili uliofanyika na kuwahusisha mashahidi wapatao 60 ulikuwa ukiongozwa na katibu mkuu wa Shirikisho la Soka la Asia Magharibi-WAFF, Fadi Zreiqat uligundua kuwa baadhi mechi za vilabu na kimataifa zilikuwa zimepangwa. Katika taarifa yake FIFA ilipongeza shirikisho hilo kwa hatua walizochukua huku ikiwataka kuwatumia taarifa zaidi ili ziweze kuwasilishwa katika kamati ya nidhamu kuangalia uwezekano wa kuongeza adhabu. Soka barani Asia limekuwa ilikikumbwa na matukio ya upangaji matokeo katika siku za karibuni ambapo nchi za Korea Kusini na China nazo zimekumbwa na matukio kama hayo.

REDKNAPP AWAKINGIA KIFUA WACHEZAJI WAKE KUHUSU KASHFA YA KUJIRUSHA KAMBINI DUBAI.

MENEJA wa klabu ya Queens Park Rangers-QPR, Harry Redknapp amekanusha taarifa kuwa baadhi ya wachezaji wake walikuwa wakijirusha sana wakati timu hiyo ilipokuwa katika kambi nchini Dubai mwezi uliopita. Gazeti la Daily Mirror la Uingereza liliwanukuu wachezaji watatu ambao hawakutajwa majina wakidai kwamba walikuwa wakitoka mara kwa mara kwenda kujirusha nyakati za usiku. Redknapp ambaye kikosi chake hicho kiko katika mstari wa kushuka daraja msimu huu alithibitisha kuwa alikuwa akikaa hoteli tofauti na wachezaji wapokuwa wakikaa lakini amekanusha vikali madai hayo. Kocha amesema kama kweli wachezaji wake walikuwa wakifanya hivyo basi walikuwa wakifanya pasipo yeye kujua lakini aliwatetea wachezaji wake akidai hawawezi kufanya hivyo. QPR ambayo inamilikiwa na mjasiria mali milionea kutoka Malaysia, Tony Fernandez imeanza vibaya msimu huu chini ya kocha Mark Hughes aliyetimuliwa lakini bado imeendelea kusuasua hata baada ya kumpata Redknapp.