Monday, March 4, 2013
SIMBA KUTUA JUMANNE USIKU.
TIMU ya Smba inarejea nchini Tanzania kesho usiku ikitokea Angola ambako jana ilitolewa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Libolo ya hapa. Wachezaji wa Simba leo asubuhi wamefanya mazoezi katika Uwanja wa Libolo uliopo hapa ambako mechi hiyo ilichezwa na mchana itasafiri kwenda mji mkuu wa Angola, Luanda, itakapolala kusubiri safari ya kesho. Hali katika kambi ya Simba iliyopo katika Hoteli ya Ritz, ilikuwa ya huzuni kutokana na kipigo hicho kikubwa zaidi cha ugenini ambacho Simba imewahi kukipata katika kipindi cha miaka minne iliyopita. Mara ya mwisho Simba kupata kipigo kikubwa ilikuwa mwaka 2009 ilipofungwa mabao 5-1 na Harass Al Hadoud ya Misri katika michuano kama hii kwenye mechi iliyopigwa jijini Alexandria, Misri. Kwa ujumla, Simba ilicheza vizuri katika mchezo huo isipokuwa katika dakika 10 za mwisho ambazo iliruhusu mabao matatu kati ya manne iliyofungwa. Hata hivyo, matokeo hayo ya 4-0 hayatoi tathmini halisi ya mechi hiyo kwa vile katika sehemu kubwa ya mchezo huo, Simba na Libolo zilikuwa zimetoshana nguvu. Libolo walikuwa na faida ya kuwa na wachezaji wenye uzoefu mkubwa wa mechi za kimataifa kama vile kiungo Ruben aliyekuwa nyota wa mchezo huo ambaye pamoja na kufunga bao la tatu, ndiye aliyekuwa akiichezesha timu hiyo. Ruben ametoka kuichezea klabu ya Braga ya Ureno iliyokuwa ikishiriki katika Ligi ya Mabingwa Ulaya na tofauti za wachezaji kama hao na wale wa Simba ilionekana katika namna ambavyo wenyeji walitumia nafasi zao. Saa moja kabla ya mechi kuanza, mvua kubwa ilinyesha katika mji wa Calulo na kuathiri hali ya uwanja jambo lililosabisha mpira kuchezwa katika mazingira magumu.
RONALDO ATEGEMEA KUPOKEWA VYEMA OLD TRAFORD.
MSHAMBULIAJI nyota wa klabu ya Real Madrid, Cristiano Ronaldo anategemea kupokewa vyema na mashabiki wa Manchester United wakati atakaporejea tena katika Uwanja wa Old Traford toka alipoondoka lakini amekiri kuwa atajisikia vyema akifunga bao. Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutua Uingereza, Ronaldo amekiri angependa kufunga kufunga bao katika mchezo huo marudiano wa Ligi ya Mabingwa Ulaya hatua ya timu 16 bora. Ronaldo amesema atajisikia furaha kufunga bao katika uwanja huo ambao una kumbukumbu katika maisha yake ya soka lakini amedai hana uhakika kama atashangilia akifunga bao hilo. Nyota huyo pia anetegemea kupokewa vyema na mashabiki wa United baada ya kunyakuwa mataji matatu ya Ligi Kuu na moja la Ligi ya Mabingwa Ulaya katika miaka sita ambayo ameitumikia klabu hiyo.
PARK ATEMWA KOREA KUSINI.
MSHAMBULIAJI nyota kimataifa wa Korea Kusini, Park Chu-Young ametemwa katika kikosi cha wachezaji 23 wa nchi hiyo ambacho kitacheza mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Qatar baadae mwezi huu. Park mwenye umri wa miaka 27 ambaye anacheza klabu ya Celta Vigo ya Hispania kwa mkopo katika klabu ya Arsenal ya Uingereza ameshindwa kuonyesha cheche zake baada ya kutofunga bao lolote toka Novemba mwaka jana. Korea Kusini inashika nafasi ya pili katika kundi A ambalo linaongozwa na Uzbekistan na wataikaribisha Qatar Machi 26 katika mzunguko wa mwisho wa mechi za kufuzu michuano hiyo kwa upande wa bara la Asia. Kocha wa timu hiyo alitetea uamuzi wake wa kumuacha Park akidai kuwa ameteua kikosi chake kutokana na uwezo wa wachezaji na viwango vyao katika vilabu vyao. Park ambaye amecheza katika michuano ya Kombe la Dunia 2006 na 2010 amecheza misimu mitatu katika klabu ya AS Monaco ya Ufaransa kabla ya kujiunga na Arsenal mwaka 2011.
RENARD AWATAKA MAOFISA NA WACHEZAJI KUNG'AMUA VIPAJI KWA USAHIHI.
KOCHA wa timu ya taifa ya Zambia, Herve Renard amewataka wachezaji na maofisa wote wanaohusika na mpango ya kung’amua vipaji vya wachezaji kufanya kazi hiyo kwa usahihi muda wote. Renard alitoa kauli hiyo baada ya kumalizika kwa kipindi cha jana mchana na kusema wachezaji wote ambao watakuja kufanyiwa usaili wakiwa wamechelewa watakuwa moja kwa moja wamejiondoa kushiriki zoezi hilo. Kocha huyo amesema ili zoezi hilo lifanikiwe ni lazima kupata watu ambao wanaojali muda kwasababu kama kwenye usaili amechelewa hata ukimchagua ataendelea na tabia yake hiyo hivyo kushindwa kupata wachezaji sahihi wenye kujituma. Benchi la ufundi la timu ya taifa ya nchi hiyo pamoja na Renard wako katika msako wa kutafuta vipaji nchi nzima kwa ajili kuimarisha kikosi cha timu hiyo ambayo ilishindwa kutetea taji lake la michuano ya Mataifa ya Afrika-Afcon Januari mwaka huu.
Sunday, March 3, 2013
NADAL ANYAKUWA TAJI LAKE LA PILI MEXICO.
MCHEZAJI tenisi nyota Rafael Nadal amefanikiwa kumfunga David Ferrer katika fainali ya michuano ya wazi ya Mexico na kushinda taji lake la pili toka arejee uwanjani baada kupona majeraha katika mguu wake wa kushoto. Nadal ambaye ni raia wa Hispania alikuwa akijiuguzi kwa kipindi cha miezi saba lakini sasa ameonekana kupona na kurejea katika hali yake ya kawaida kwa kufanikiwa kushinda taji la pili katika kipindi cha wiki tatu baada ya kushinda pia taji la michuano ya wazi ya Brazil mwezi uliopita. Nadal mwenye umri wa miaka 26 alimfunga mhispania mwenzake Ferrer mwenye umri wa miaka 30 kwa 6-0 6-2 katika mchezo uliofanyika jijini Acapulco. Nyota huyo ambaye ameporomoka katika orodha za ubora duniani mpaka nafasi ya tano, aliishukuru familia yake na madaktari ambao walikuwa wakimhudumia katika kipindi chote ambacho amekuwa majeruhi na kudai kwamba anajisikia vyema.
PIQUE ALIA NA MWAMUZI.
BEKI wa klabu ya Barcelona, Gerard Pique amedai kuwa mahasimu wao Real Madrid huwa wanapata upendeleo kutoka kwa waamuzi baada ya timu yake kunyimwa penati katika dakika za lala salama katika mchezo waliofungwa mabao 2-1 na Madrid. Bao la kichwa lilifungwa na Sergio Ramos dakika tisa kabla ya mchezo kumalizika lilitosha kuipa ushindi timu hiyo baada ya Karim Benzema kufunga bao la kuongoza katika kipindi cha kwanza kabla ya kusawazishwa na Lionel Messi dakika chache baadae. Lakini Pique na wachezaji wenzake waliachwa wakilalamika baada ya Ramos kuonekana kumuangusha Adriano katika eneo la hatari malalamiko ambayo yalipelekea golikipa wa Barcelona Victor Valdes kupewa kadi nyekundu baada ya kipenga cha mwisho kupulizwa. Pique amesema walikuwa wakimwambia mwamuzi kwamba ni penati ya wazi lakini ilikuwa kinyume kwani mwamuzi aliamua vingine na sio jambo la kushangaza katika mchezo mkubwa kama huo. Nyota huyo aliendelea kusema kuwa matokeo ya sare yalikuwa sahihi katika mchezo huo kama wangepewa penati lakini hawawezi kufanya hilo likawa sababu kwakuwa timu hiyo ina ubora wa hali ya juu hivyo hawawezi kutegemea maamuzi ya mwamuzi.
SHABIKI MMOJA AFA KATIKA VURUGU HUKO ARGENTINA.
Subscribe to:
Posts (Atom)






