Sunday, June 2, 2013
MO FARAH ACHEMSHA MICHUANO YA DIAMOND LEAGUE YA MAREKANI.
MWANARIADHA nyota wa Uingereza, Mo Farah ameshindwa kutamba katika mbio za mita 5,000 za Diamond League zilizofanyika jijini Eugene, Oregon nchini Marekani. Farah mwenye umri wa miaka 30 alishika nafasi ya pili mbele ya Edwin Soi wa Kenya ambaye alishinda mbio hizo kwa kutumia muda wa dakika 13 na sekunde 4.75. Mwanariadha huyo ambaye ni bingwa wa medali mbili za dhahabu za olimpiki alichagua kukimbia mbio za mita 5,000 badala ya mita 10,000 baada ya kupata maambukizi ya tumbo. Farah alianza kuibuka katika michuano ya riadha ya Dunia iliyofanyika jijini Daegu mwaka 2011 ambapo alinyakuwa medali ya fedha katika mbio za mita 10,000 na dhahabu katika mbio za mita 5,000 kabla ya kunyakuwa medali zote za dhahabu katika mbio hizo mbili kwenye michuano ya olimpiki iliyofanyika London mwaka jana.
BAYERN YAFANIKIWA KUSHINDA MATAJI MATATU MFULULIZO.
WINGA machachari wa klabu ya Bayern Munich, Franck Ribery ameonyesha furaha yake baada ya klabu yake kuifunga Stuttgart kwa mabao 3-2 katika fainali ya DFB-Pokal na kuweka historia ya kuwa klabu ya kwanza nchini Ujerumani kushinda mataji matatu kwa mkupuo. Bayern walifanikiwa kuweka kibindoni taji la Ligi Kuu ya Ujerumani mapema mwezi uliopita kabla ya kufanikiwa kuwafunga mahasimu wao Borussia Dortmund katika mchezo wa fainali ya kufanikiwa kunyakuwa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya. Winga huyo wa kimataifa wa Ufaransa amesema kuwa anajisikia furaha na mafanikio hayo ya kihistoria waliyopata ni kutokana na juhudi pamoja na malengo waliyojiwekea. Ribery aliwashukuru wachezaji wenzake pamoja na mashabiki ambao wamekuwa nao katika kipindi chote na kuahidi kuwa ataendelea kuwepo klabuni hapo kwa kipindi kirefu kijacho. Naye nahodha wa klabu hiyo Philipp Lahm aliongeza kuwa juhudi zao za ndani na nje ya uwanja ndizo zilizowafikisha hapo.
Saturday, June 1, 2013
SIMBA, YANGA HATARINI KUIKOSA MICHUANO YA KAGAME.
SERIKALI imesema italiangalia upya suala la vilabu vya soka vya Tanzania vya Simba, Yanga na Falcon kwenda nchini Sudan kushiriki katika michuano ya Kombe la Kagame ambayo inaandaliwa na Baraza la Michezo kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati-CECAFA. Hatua hiyo imefikiwa baada ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bernand Membe kuulizwa juu ya usalama wa timu hizo zitakapokwenda jijini Darfur ambako michuano hiyo imeandaliwa. Membe amesema mpaka sasa hali ya kiusalama katika mji huo bado haijakaa vizuri kwani wageni wote wanaofika huko hupokelewa kwa magari maalumu ya kuzuia risasi pamoja na nguo ngumu za kuzuia risasi. Waziri huyo aliendelea kusema kuwa pia hakuna hoteli nzuri na zenye usalama na kuonyesha kushangazwa na watu waliokubali michuano hiyo ifanyike huko wakati wanajua hali ya kiusalama sio shwari. Membe amesema kama wizara kwa kushirikiana na vyombo vinavyohusika vitatoa taarifa za awali kabla ya hawajatoa mapendekezo kinyume chake ili kuzuia uwezekano wa kuzitosa timu zetu sehemu ambayo inaweza kuhatarisha usalama wao. Michuano ya Kagame safari hii imepangwa kufanyika katika miji ya Darfur ya Kaskazini pamoja na Gordofan ya Kusini Kuanzia Juni 18 mpaka Julai 2 mwaka huu ambapo kutakuwa na makundi matatu huku Kundi A likiwa na timu za Merreikh-Elfasher ya Sudan, APR ya Rwanda, Simba ya Tanzania na Elman ya Somalia. Wakati kundi B litakuwa na timu za Al-Hilal-Kaduugle ya Sudan, Tusker ya Kenya, Al Nasir ya Sudan Kusini, Falcon ya Zanzibar na Al Ahly Shandi ya sudan huku kundi C likiwa na timu za Yanga ya Tanzania, Express ya Uganda, Ports ya Djibouti na Vital O ya Burundi.
MADRID YAFIKIRIA KUUZA HAKI ZA JINA LA UWANJA WAKE.
KLABU ya Real Madrid inafikiria kuuza haki za jina la uwanja wake wa Santiago Bernabeu ikiwa ni sehemu ya kutafuta njia mpya za kujiongezea mapato. Alhamisi iliyopita klabu hiyo ilitangaza kuwa kampuni ya Emirates ndio watakaochukua nafasi ya Bwin wakiwa kama wadhamini wapya wa fulana zao kuanzia msimu ujao katika mkataba ambao una thamani ya euro milioni 125 kwa kipindi cha miaka mitano. Rais wa Madrid Florentino Perez amesema wanataka kutengeneza timu iliyo imara na sehemu ya hilo itakuja kupitia ushirikiano na makampuni makubwa na kwasasa wana ushirikiano na kampuni hiyo kubwa ya ndege duniani. Rais huyo aliendelea kusema kuwa uwekezaji wa kifedha hauwezi kuishia hapo kwani klabu hiyo sasa inaangalia mwekezaji mwingine ambaye atafaa kwa ajili ya uwanja wao wa Santiago Bernabeu. Kama suala hilo likifanikiwa Madrid itakuwa imeungana na vilabu vingine ambavyo viwanja vyao vinatumia majina ya wadhamini kama Bayern Munich wanaotumia Uwanja wa Allianz Arena, Borussia Dortmund wanaotumia Uwanja wa Signal Iduna Park, Manchester City wanaotumia uwanja wa Etihad na Arsenal wanatumia uwanja wa Emirates.
MOURINHO ATUME UJUMBE WA SHUKRANI KWA MASHABIKI WA MADRID.
MENEJA wa klabu ya Real Madrid, Jose Mourinho ametuma ujumbe wa kuishukuru klabu hiyo pamoja na mashabiki wake katika kuelekea mchezo wake wa mwisho wa Ligi Kuu nchini Hispania utakaochezwa baadae usiku. Mourinho na Madrid walifikia makubaliano ya kusitisha mkataba mwishoni mwa msimu, ikimaanisha kuwa kocha huyo yuko huru kurejea klabu ya Chelsea katika kipindi hiki cha majira ya kiangazi. Mechi ya mwisho ya Mourinho akiwa kocha wa Madrid itakuwa dhidi ya Osasuna ambapo katika ujumbe wake aliitakia klabu hiyo mafanikio katuika siku zijazo. Katika ujumbe aliotuma katika mtandao wa klabu hiyo Mourinho amesema anamtakia kila mmoja ambaye anahusiana na klabu hiyo furaha tele katika zijazo na kuwashukuru mashabiki wengi kwa kumuunga mkono na kuwaheshimu wale waliokuwa hawamuungi mkono. Kocha wa Bayern Munich, Jupp Heynches ambaye anamuachia nafasi hiyo Pep Guardiola na Carlo Ancelotti wa Paris Saint-Germain ndio wanaopewa nafasi kubwa ya kurithi mikoba ya Mourinho.
FIFA YACHAGUA MWANAMKE WA KWANZA KATIKA KAMATI YAKE YA UTENDAJI.
RAIS wa Shirikisho la Soka nchini Burundi, Lydia Nsekera amechaguliwa na kuwa mwanamke wa kwanza katika Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Duniani-FIFA katika miaka 109 ya historia ya shirikisho hilo. Nsekera mwenye umri wa miaka 46 atakuwa mjumbe ndani ya kamati hiyo kwa kipindi cha miaka minne baada ya kushinda uchaguzi wa mkutano mkuu wa FIFA uliofanyika nchini Mauritius. Mwanamama huyo alijikusanyia kura 95 kati ya kura 203 zilizopigwa akiwagaragaza Moya Dodd wa Australia na Sonia Bien-Aime aliyekuwa akiiwakilisha Uturuki na Visiwa vya Caicos. Nsekera amekuwa rais wa BFF kuanzia mwaka 2004 na pia alikuwa mjumbe wa kamati ya maandalizi ya FIFA katika michuano ya soka ya Olimpiki mwaka 2008 na 2012.
Akihojiwa mara baada ya kuchaguliwa Nsekera amesema kuchaguliwa kwake huko kutahamasisha wanawake wengi kujiamini kwamba wanaweza.
Akihojiwa mara baada ya kuchaguliwa Nsekera amesema kuchaguliwa kwake huko kutahamasisha wanawake wengi kujiamini kwamba wanaweza.
WAZIRI APIGILIA MSUMARI WA MWISHO KUHUSU "VUVUZELA" ZA BRAZIL.
WAZIRI wa Sheria wa Brazil, Jose Eduardo Cardozo amesema vifaa vya plastini aina ya caxirola ambavyo mashabiki wa soka wa nchi hiyo hutumia kushangilia timu zao havitaruhusiwa katika viwanja wakati wa michuano ya Kombe la Shirikisho baadae mwezi huu na Kombe la Dunia mwakani kwasababu za kiusalama. Cardozo amesema sekretarieti inayosimamia matukio muhimu imeamua kuwa kwasababu za usalama wa watu wengi, itakuwa si vyema kuuhusu vifaa hivyo ndani ya viwanja. Waziri huyo aliendelea kusema kuwa adhabu ya kufungia vifaa vyovyote vya muziki ikiwemo caxirola itaanza kutekelezeka katika mchezo wa kirafiki wa kirafiki wa kimataifa kati ya Brazil na Uingereza utakaofanyika katika Uwanja wa Maracana jijini Rio de Janeiro. Caxirola ni aina vifaa vya plastiki ambavyo hutoa sauti mbalimbali kama ilivyokuwa kwa vifaa vya vuvuzela ambavyo mashabiki nchini Afrika Kusini walikuwa wakivitumia katika michuano ya Kombe la Dunia 2010. Uamuzi wa kufungia vifaa unatokana na tukio la April 28 ambapo mashabiki waliohudhuria mechi kati timu ya Bahia na Vitoria kuvurumisha mamia ya caxirola uwanjani baada ya kukasirishwa na matokeo.
Subscribe to:
Posts (Atom)





